TAIFA Stars leo itacheza staili ya kushambulia mwanzo-mwisho dhidi ya wenyeji wao timu ya taifa ya Chad katika pambano muhimu la awali kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia. Mechi inapigwa kwenye Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya jijini N’Djamena.
Kocha wa Stars, Jan Poulsen amekumbushia falsafa yake ya kucheza kwa kushambulia, ambapo atawatumia viungo wawili na kujaza washambuliaji mbele Abdi Kassim, Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa na Mbwana Samata.
Stars iliyoingia jijini N’dJamena saa saba usiku juzi kwa ndege ya shirika la ndege la Kenya itaingia uwanjani ugenini kusaka matokeo bora katika pambano hilo la awali kabla ya kurudiana na wenyeji wao katika uwanja wa taifa Jumanne jioni.
Kabla ya pambano la leo, jana Stars walifanya mazoezi yao jioni katika uwanja wa Idriss Mahamat Ouya huku wakimkosa mlinzi wa kulia wa timu hiyo, Erasto Nyoni ambaye alianza kusumbuliwa na malaria tangu alipotua jijini N’Djamena.
Kwa mujibu wa Poulsen, kiungo chipukizi, Shomari Kapombe anatazamiwa kuziba nafasi ya Nyoni huku winga mahiri Mrisho Ngassa akitazamiwa kuanza pambano hilo baada ya kukosekana katika vikosi vya kwanza vya kocha Poulsen katika mechi za karibuni.
Kurudi kikosini kwa Ngassa kunatokana na kujitoa kwa mshambuliaji Danny Mrwanda ambaye amekuwa akianza katika mechi za karibuni kama mshambuliaji anayesaidia mashambulizi kuanzia upande wa kushoto.
Poulsen ameimbia Mwananchi, haifahamu timu ya Chad lakini akaahidi kubadili fomesheni ya Stars dakika kadhaa baada ya kuanza kwa pambano hilo kutokana na jinsi atakavyowasoma wapinzani wake.
“Siijui vizuri Chad. Nitawaangalia katika dakika 20 za mwanzo na kama kuna uwezekano wa kubadili fomesheni basi nitafanya hivyo. Lakini kama ilivyo kawaida yangu, asilimia 95 ya mchezo wa timu yangu unategemea zaidi na jinsi tunavyocheza wenyewe kuliko ambavyo mpinzani wetu anacheza.” alisema Poulsen.
Hata hivyo, Poulsen alisema atafurahi zaidi kucheza soka la kushambulia kwa ajili ya kupata matokeo mazuri badala ya kucheza soka la kujihami ambalo haliisaidii timu.
Naye kocha wa Chad ambaye kikosi chake kilifanya mazoezi ya mwisho katika uwanja wa Idriss Mahamat Ouya, Mohamed Omary alisema dakika tisini ndio zitaaamua mshindi wa leo na si vinginevyo.
“Sichezi mpira nje ya uwanja. Nacheza ndani ya uwanja. Dakika tisini ndio zitaamua matokeo ya mechi ya kesho (leo).” Alisema Omary
Endapo Stars itapata matokeo mazuri katika mechi zake mbili dhidi ya Chad ambazo zinachezwa ndani ya siku nne, itapata nafasi ya kucheza kundi la kufuzu kwenda kombe la dunia ikipangwa pamoja na Gambia, Ivory Coast na Morocco
Mwamuzi wa pambano la leo ni Ogunkolade Bunmi wa Nigeria akisaidiwa na Abidoye Tunde na Baba Abel ambao wote pia ni Wanigeria.
Kwa mujibu wa Poulsen kikosi kamili cha Stars leo ni Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Juma Nyoso, Idrisa Rajab, Shaabani Nditi, Henry Joseph,
Abdi Kassim, Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa na Mbwana Samata
0 Comments