Said Mohamed Kapita akimwonyesha mwandishi wetu (hayupo pichani) tumbo lake linalodaiwa kuwa na mimba.
Na Dunstan Shekidele, Morogoro
UNAAMINI katika miujiza? Kilombero, Morogoro kuna mtikisiko mkubwa kufuatia habari kwamba kuna mwanaume aliyenasa mimba ya ajabu.
Mwanaume ana mimba! Habari zinadai kuwa Said Mohamed Kapita, 40, ametundikwa mimba kishirikina, ikiwa ni adhabu baada ya kile kinachodaiwa ni kumpa ujauzito mwanafunzi (jina kapuni).
Inadaiwa kuwa Kapita ambaye ni fundi ujenzi wa nyumba anayejitegemea, alimpa mimba denti, hivyo kuibua mtafaruku mkubwa kati yake na wazazi wa mwanafunzi huyo.
MADAI YALIYOPO
Inaelezwa kuwa hivi karibuni, Kapita akiwa amekaa kibarazani, jirani na nyumbani kwake, alifuatwa na baba mzazi wa denti huyo na kumhoji kuhusu ujauzito uliomo kwenye tumbo la bintiye.Rafiki wa Kapita (jina tunalo) ambaye ni mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema: “Ulitokea mvutano mkubwa. Baba wa yule mwanafunzi ni babu kabisa na siku ile aliongozana na mwanaye ambaye tumbo lake lilishachomoza. Mimba ilikuwa inaonekana wazi.
“Mwanafunzi alimtaja Kapita kwamba ndiye mhusika wa ule ujauzito, baba naye akasisitiza ni lazima akubali kuhudumia. Kapita akakataa kata kata. Unajua haya mambo, hata kama ni kweli huwezi kukubali mimba, yule ni mwanafunzi, miaka 30 jela nani anataka?
“Alipokataa baba mtu akawa mbogo. Mwisho akamwambia kuwa hawezi kumshtaki polisi, isipokuwa adhabu yake ni kuihamisha mimba kutoka kwenye tumbo la binti yake kwenda kwa Kapita.
“Sisi tulidhani utani lakini baada ya siku mbili tukaona mabadiliko. Ndugu yetu akavimba tumbo kama mjamzito. Hii ikasababisha gumzo lipae, kila mtu Kilombero akapata habari kwamba ndugu yetu ni mjazito.”HEKAHEKA HOSPITALI YA MIKUMI
Katikati ya wiki iliyopita, Kapita alipelekwa Hospitali ya Mikumi, lengo likiwa ni kupata tiba juu ya matatizo ya tumbo lake.
Hata hivyo, baada ya kufika hospitali na kufanyiwa uchunguzi, tumboni hakuonekana mtoto, badala yake ilibainika kuwepo na kiasi kikubwa cha maji.Kutokana na hali hiyo, madaktari walimnyonya maji yote ambayo yalijaa ndoo mbili lakini baada ya muda tumbo lilirudi vile vile.
Uwepo wa Kapita hospitalini hapo, ulisababisha vurugu nzito kutoka kwa wananchi waliomiminika wakitaka kumuona ili wajue kama ameshajifungua au la!
Zikawepo habari kuwa Kapita amejifungua mtoto kwa njia ya upasuaji, kitendo ambacho kilizidi kukusanya umati wa watu hususan wakazi wa Mikumi, waliofika hospitalini hapo kutaka kumuona.
Kutokana na vurugu hizo ambazo zilisababisha shughuli za kutoa huduma hospitalini hapo kusimama, madaktari waliamua kumkabidhi Kapita kwa ndugu zake na kupitishiwa mlango wa nyuma kumrudisha nyumbani kwake, Kilombero.
NENO LA DAKTARI
Ofisa muuguzi wa hospitali hiyo, Dk. Joseph Masenga alilithibitishia gazeti hili kumpokea mgonjwa huyo lakini akafafanua kuwa uchunguzi wa kitaalamu haujabaini kuwepo kwa mtoto ndani ya tumbo lake.
“Alilazwa hapa, alifika hapa akiwa na tumbo kubwa kama la mama mjamzito lakini baada ya kumfanyia uchunguzi tukabaini tumbo lile lilijaa maji. Tulimtoa maji mengi zaidi ya ndoo mbili.
“Alikuwa amepungukiwa maji mwilini, tukamuongezea. Tumeambiwa kwamba ana ujauzito, eti huko kwao alikorofishana na watu ndiyo wakamfanyia mambo ya ushirikina, sisi hatuamini ushirikina, tulichoona tumboni ni maji, hatukuona kiumbe chochote,” alisema Dk. Masenga.
USO KWA USO NA KAPITA
Baada ya kutoka Mikumi, Uwazi lilivuka mitaa, likapanda milima na kuteremka kwenye mabonde hadi Kilombero, ndani kabisa katika Kijiji cha Kidogi, lilikoelekezwa ndiyo anakoishi Kapita.Hata hivyo, baada ya kufika nyumbani kwake, lilielezwa amepelekwa kwa mganga wa tiba za asili anayeitwa Lungu.
Uwazi lilimkuta Kapita kwa Dk. Lungu na baada ya utambulisho alisema: “Bora umekuja wewe mwandishi, nimezushiwa eti nimejifungua mtoto wa kike. Kuna watu hawanitakii mema na nawajua, hao ndiyo wanatangaza.”
KUHUSU KUMPA MIMBA DENTI
Kapita alisema: “Ni kweli nilifuatwa na mzee mmoja akiwa na binti yake mjamzito, wakasema mimi ndiye mhusika. Nafikiri lengo lao ni kunitafutia kesi, kwa maana mimi sihusiki kabisa.
“Nilipokataa, yule mzee akaniambia atahamishia ujauzito wa mwanaye kwangu. Hayo mambo siamini. Nachoamini mimi ni kwamba sina mimba na huyo mwanafunzi sihusiki naye kabisa. Mimi nina mke wangu na watoto, najiheshimu. Wanafunzi wa nini?
“Nimeshafuatwa mpaka na walokole, wananiambia waniombee nipone eti nina mimba, hiyo si kweli.”
DOKTA LUNGU
Kwa upande wa Dk. Lungu, alisema kuwa Kapita ametupiwa vitu vya kishirikina ambavyo vimemfanya ajae maji tumboni.
HII NI AJABU!
MOSI: Kwa nini imetokea baada ya kuambiwa atahamishiwa mimba ya mwanafunzi?
PILI: Kama ni mimba iweje vipimo vya hospitali visioneshe?
TATU: Ikiwa siyo mimba ni maji, mbona tumbo limezidi kukua hata baada ya kunyonywa? (Uwazi lilimshuhudia akiwa na tumbo kubwa hata baada ya kufyonzwa maji Hospitali ya Mikumi.”NNE: Watu wakaacha shughuli zao na kujaa hospitali, eti mwanaume amejifungua.
TANO: Majibu ya kitaalamu kuhusu matatizo ya Kapita hayajelezwa, zaidi ya kusemwa kwamba tumbo limejaa maji.
0 Comments