Rais Bashir(mwenye suti kushoto) alisema watateka mji huo.
Jeshi la Sudan limetwaa makao makuu ya waasi huko Blue Nile baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka katika jimbo hilo miezi miwili iliyopita.
Mrengo wa kaskazini wa waasi wa SPLM ambao walipigania uhuru wa Sudan Kusini wanapambana na serikali katika jimbo la Blue Nile na pia Kusini mwa Kordofan.
Majeshi ya serikali ya Sudan yaliingia mji wa Kurmuk Alhamisi kama saa sita mchana Hii ni kulingana na taarifa ya msemaji mmoja wa serikali.
Katika hali isiyoeleweka, majeshi hayo yaliuteka mji huo ambao walikuta wakaazi wake wamehama.
Majeshi ya SPLM eneo la kaskazini, walikuwa wameondoka mjini humo lakini wameiambia BBC kuwa vita hivyo bado havijamalizika.
Hata hivyo, huu ni ushindi mkubwa kwa Rais Omar al Bashir ambaye hapo awali alitangaza kuwa mji huo wa Kurmuk utatekwa na kuwa mikononi mwa utawala wake kabla ya sikukuu ya Idd-al-Adha ambayo inatarajiwa kufanyika Jumapili.
Walioshuhudia tukio hilo wanasema watu wengi walimiminika barabarani kusheherekea baada ya wanajeshi wa Sudan kuingia katika jimbo hilo.
Kwa wakati huu wanajeshi wa Rais Bashir wanakalia sehemu nyingi katika jimbo hilo Blue Nile.
Waasi wa SPLM- mrengo wa kaskazini bado hawana uwezo wowote wakukabiliana na jeshi la Sudan. Lakini vita hivyo vinavyo endelea katika majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile vinavuruga uhusiano kati ya Sudan Kusini na Khartoum.
0 Comments