Jukwaa la Katiba Tanzania, limeitisha maandamano ya amani Jumamosi wiki hii kote nchini, kwa lengo la kumshawishi Rais Jakaya Kikwete, asisaini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2011 kuwa sheria kamili, baada ya kupitishwa na Bunge, Ijumaa wiki iliyopita.
Tamko la maandamano hayo, lilitolewa na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba, katika mkutano na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, uliohudhuriwa pia na viongozi wa asasi za kiraia, ambazo ni jumuiko la Jukwaa hilo, kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Kibamba alisema wanataka Rais Kikwete asisaini muswada huo kwa vile kusainiwa kwake kutawafanya wananchi wengi kukosa fursa ya kushiriki mchakato wa kupata Katiba mpya kuanzia hatua ya msingi.
Alisema pia wengi wanaweza kujikuta wako jela, hali inayoweza kujenga chuki baina ya serikali na wananchi na hivyo kuvunja amani.
Jijini Dar es Salaam, alisema maandamano hayo yataanzia katika viwanja vya Mnazi Mmoja hadi katika Viwanja vya Jangwani.
“Tunawahamasisha wananchi wote wanawake na wanaume, vijana na wazee, wakulima, wafugaji, wafanyakazi na viongozi wa taasisi zote, zikiwamo za kiimani, kujitokeza katika maandamano ya amani siku ya Jumamosi, ambayo lengo lake ni kujenga msingi mzuri kwa ajili ya kujenga muafaka wa kitaifa kupitia ushiriki wa Watanzania wote katika kuandika Katiba mpya,” alisema.
Alisema tayari wamekwisha kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, kuomba ulinzi kote, ambako maandamano hayo yatafanyika.
Msemaji wa Jeshi hilo nchini, Advera Senso, hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi, mara zote ilikuwa ikiita bila kupokelewa. Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Hezron Kaaya, alisema iwapo Rais Kikwete atawapuuza na kusaini muswada huo, watachukua hatua nyingine ya mchakato mbadala ya kukusanya maoni ya wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya, alisema muswada huo ulipaswa kusomwa mara ya kwanza ukiwa katika lugha ya Kiswahili na baadaye wananchi kushiriki kutoa maoni akisema ndio msingi wa Katiba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya, alisema ushiriki wa wananchi katika suala hilo, ni jambo muhimu kwa vile kinachotaka kufanyika, ni kutengenezwa sheria mama, ambayo ni tofauti na sheria nyingine za kawaida.
0 Comments