Mtoto wa ajabu amezaliwa akiwa na viungo vinne vya uzazi vya kiume, sehemu za kutolea haja kubwa mbili moja ikiwa mgongoni pamoja na mguu mkubwa wenye vidole sita ambao nao umeota kati kati ya mgongo.
Mtoto huyo ambaye mzazi wake Naishooki (23), anatoka kijiji cha Injok, Wilayani Arumeru, mkoani Arusha, alizaliwa juzi usiku kwa njia ya upasuaji katika hospitali ya Olturumet.
Akizungumza huku akilia kwa uchungu, mama mzazi wa binti aliyejifungua mtoto, Naishiye Logolie, alisema hawajawahi kuona kitu cha ajabu na kutisha kama yaliyotokea kwa mtoto wao.
“Mwanangu alipokuwa mjamzito hajawahi kuonyesha dalili za tatizo lolote. Tumechachanganyikiwa kuona kitu kama hiki. Tunaomba madaktari watusaidie kujua ni nini hiki. Ni huzuni kwa jamii yangu,” alisema Mama Logolie katika wodi namba mbili alikolazwa mama wa kichanga hicho.
Alisema mtoto wake alianza kupata uchungu juzi na walipompeleka katika kituo cha afya karibu na nyumbani kwao, walishangaa kupewa rufaa kwenda Olturumet, ambapo walipofika mdaktari walimwambia ni lazima afanyiwe upasuaji haraka kumwokoa mtoto na mama pia.
Aidha, alisema baada ya mwanaye kupelekwa chumba cha upasuaji, walianza kusali kuombea upasuaji huo uwe salama, lakini baada ya upasuaji waliitwa na daktari na kuambiwa kuwa mzazi yuko salama isipokuwa kuna tatizo kwa mtoto.
“Kwa haraka hatukudhani ni kile ambacho kimetokea tulifikiri labda mtoto amechoka sana au ana tatizo la kiafya ambalo lingekuwa la kawaida, baada ya kuona maumbile yake nilizimia, sikuamini na hata sasa siamini mwanangu kazaa mtoto wa aina hii,” alisema Naishiye.
Mganga wa Halmashauri ya Arusha, Dk. Thobias Mkina, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa wanajaribu kufanya linalowezekana kuokoa maisha ya mtoto huyo ambaye hajaweza kunyonya maziwa ya mama yake tangu azaliwe juzi usiku.

“Matukio ya kuzaliwa watoto wakiwa na matatizo yanatokea, lakini hili kidogo linaonekana kuwa la kipekee sana kutokana na maumbile ya mtoto,” alisema Dk. Mkina.
Alisema sababu za kitaalamu zinazoweza kusababisha matukio ya aina hii ni matumizi ya dawa zenye kemikali na wakati mwingine kuna matukio ya kurithi kutoka kwa kizazi cha muhusika.
Hata hivyo, alisema uchunguzi unaendelea na wakimaliza watampatia rufaa kwenda katika hospitali kubwa zaidi.
Baada ya taarifa za kuzaliwa kwa mtoto huyo, watu wamekuwa wakifurika katika familia ya mwanamke huyo kujua kilichotokea huku wengine wakisafiri kwa mwendo wa kilomita zaidi ya 20 kufika katika hospitali hiyo kumwona mtoto huyo.
Kuzaliwa kwa mtoto huyo mwenye uzito wa kilo nne, kunatokea siku chache baada ya tukio la ajabu kutokea katika siku za karibuni mkoani Arusha la kondoo aliyezaa kondoo mwenye kichwa cha binadamu katika eneo la Kiserian, Wilayani Arumeru.