Majeruhi wa ajali hiyo, Anitha Julius akiwa katika hospitali ya Rufaa jijini Mbeya akipatiwa matibabu huku akiwa amemshikilia mwanae wa umri wa siku saba.
…
Bajaji yenye namba za usajili T 840 BPT baada ya kugongwa na lori.WATU sita wamenusurika kufa huku mmoja akifariki dunia papo hapo, baada ya kugongwa na Lori walipokuwa wakisafiri na bajaji jijini Mbeya.
Tukio hilo limetokea jana majira ya saa nane mchana eneo la Magege-Mapelele ambapo lori hilo lilitokea eneo la Makunguru barabara ya kutoka Mwanjelwa kuelekea Isanga.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliokuwa wamefika eneo la tukio, mashuhuda wa ajali hiyo walisema kuwa lori hilo lilipoteza mwelekeo na kuivamia bajaji iliyokuwa na abiria watano na mtoto mdogo mwenye umri wa siku saba.
Walisema kuwa; baada ya lori hilo lenye namba za usajili T 851 AEK Isuzu FTS linalomilikiwa na Stephano Mahenge wa mkoani Mbeya, kuparamia bajaji yenye namba za usajili T 840 BPT iliyokuwa ikiendeshwa na Daud Sanga (28) ndipo likaenda kujikita mtaloni.
Baada ya ajali hiyo kutokea, mtu mmoja alibainika kufa papo hapo baada ya kuvuja damu nyingi na kupata majeraha makubwa mwilini mwake.
Marehemu huyo ametambulika kwa jina la Monica Jimmy mkazi wa Shamwengo wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani hapa.
Majeruhi wa ajali hiyo wametambulika kuwa ni pamoja na Mwalimu Loveness Kibona (26), mkazi wa Iganzo anayefundisha shule ya Sekondari Wigamba, Mwalimu Joyce Kamwela mkazi wa Iganzo, Izack Mwakilelele (30) mkazi wa Ilemi na Festo Noah mkazi wa Lyoto.
Wengine ni Anitha Julius ambaye alikuwa na mtoto mchanga mwenye umri wa siku saba ambapo papo hapo marehemu aliyefariki dunia imeelezwa kuwa ni Mama mkwe wake.
Kufariki kwa marehemu Monica Jimmy, kumethibitishwa na Muuguzi wa zamu wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambaye hata hivyo ameomba jina lake lisitajwe.
0 Comments