ASEMA BILA MUAFAKA CHAMA CHAKE KITATAFUTA NJIA MBADALA

Waandishi Wetu, Dodoma, Dar
WAKATI mjadala wa Muswada wa Sheria ya Kuunda Katiba Mpya ukizidi kuitikisa Serikali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ameonya kwamba kama suala hilo litachezewa, chama chake kitatafuta njia mbadala kwa wananchi ya kupata Katiba. Mjadala kuhusu muswada huo unakabiliwa na upinzani mkali kutoka ndani na nje ya Bunge na jana wabunge wengi wa CCM waliochangia, waliwashambulia wenzao wa Chadema.
Wabunge hao wa CCM, juzi walifanya kikao cha chama hadi saa 6:00, pamoja na mambo mengine kujadili namna ya kupitisha muswada huo. Kamati Kuu ya Chadema nayo ikikutana kwa dharura kujadili suala hilo. Zitto ambaye amerejea siku tatu zilizopita akitokea India alikokuwa akipatiwa matibabu, alisema jana katika mahojiano maalumu na gazeti hili kwamba, njia mwafaka ya kutafuta suluhu ni kwa viongozi wa Serikali kukubali kukaa meza moja na Chadema.
Alionya kuwa endapo itaendelea na mchakato huo wa Katiba bila mwafaka, mchakato huo utakuwa umekosa uhalali wa kisiasa kitu ambacho alisema ni hatari kwa nchi. Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni alionya kuwa bila kufikiwa kwa hatua hiyo, jambo hilo litazua mtafaruku kwa sababu Chadema nacho kitaandaa mchakato wake wa kuunda Katiba Mpya.
“Si lazima yote wanayoyataka Chadema yakubaliwe na wala siyo lazima yote wanayokataa upande wa Serikali ya CCM yakubaliwe. Ni lazima pande zote zikubaliane. Ni lazima ifahamike kwamba mchakato wa Katiba Mpya ni muhimu sana hivyo maridhiano ya namna ya kuipata ni jambo ambalo halipaswi kupuuzwa.”Zitto alisema tukio la wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi kususia muswada huo bungeni, linaonyesha kuwa wabunge wa vyama hivyo vya upinzani hawako tena tayari kushiriki kwenye mchakato huo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiupigania hasa baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu uliopita.
Alisema suala la kuunda Katiba Mpya ni la wananchi na wala siyo la kisiasa kama linavyopotoshwa na baadhi ya wanasiasa nchini.Kuhusu malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya wanasiasa hasa wa CCM kuwa Chadema kina ajenda ya siri ambayo inaweza kuipeleka nchi kwenye matatizo, Zitto alisema kinachoonekana kwenye mvutano huo ni kwamba makundi mbalimbali hayaaminiani kwenye mchakato huo.

Alisema katika mchakato huo:
“CCM wao wanataka kujenga mazingira ambayo yatawapa nafasi ya kuendelea kuwapo madarakani na wakati huo upinzani nao unataka yawapo mabadiliko yatakayojenga uwiano ulio sawa na unaoweza kuwapa nafasi ya kuingia madarakani.”Katika mazingira ya namna hiyo, Zitto alisema linaweza likaundwa baraza la kitaifa ambalo litashirikisha wajumbe kutoka makundi mbalimbali, hasa Serikali na viongozi wa vyama.

Alisema kamwe suala hilo haliwezi kupata mwafaka kwa kuangalia wingi wa wabunge bungeni kwa sababu hali hiyo itachukua mkono wa itikadi za kisiasa.Zitto alisema kwa mazingira ya sasa ambayo CCM ndicho chama tawala na chenye idadi kubwa ya wabunge ni rahisi suala la Katiba kutekwa kwa maslahi ya chama hicho na kusahau kuwa ni jambo linalomgusa kila Mtanzania.
Alisema mabadiliko ya Katiba ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho viongozi wengi wa Serikali wamekuwa hawatekelezi wajibu wao ipasavyo na inakuwa vigumu kuwaondoa kwenye nafasi zao.Zitto alitoa mfano kuwa katika hatua za mwanzo za Kenya kutumia katiba yao mpya, imezuia uteuzi holela wa viongozi kushika nyadhifa nzito kama vile jaji mkuu na kuwaondoa baadhi ya viongozi ambao wanatuhumiwa kwa rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Kuhusu maandamano ya Chadema kwamba ni agenda za siri zinazotaka nchi iingie kwenye migogoro na isitawalike, alisema suala la maandamano yamekuwa wakiyafanya pale kunapokuwa na ajenda maalumu ambayo inatokana na kunyimwa haki katika jambo linalowagusa wananchi wengi.Zitto alisema maandamano hayo hayafanywi ovyo kwa misingi binafsi, ila kinachotakiwa ni viongozi kutenda haki kwa mujibu wa sheria za nchi.
Mjadala bungeni
Wakati wabunge wawili wa NCCR Mageuzi wakiendelea kususia mjadala huo, Mbunge wa Kasulu Mjini kupitia chama hicho, Moses Machali alishiriki na kusema kwamba watakaoupitisha laana ya Watanzania itakuwa juu yao.Machali aliweka hadharani msimamo wake wa kutounga mkono muswada huo huku akitaja sababu za kutotoka nje ya kikao hicho kuwa ni kuwaeleza ukweli.

“Mimi sina tatizo na wenzangu wa Chadema waliotoka nje, nimebaki ndani ya kikao hiki ili kuwaeleza ukweli kuwa muswada huu ulipaswa kusomwa kwa mara ya kwanza ili tuweze kutoa fursa kwa wananchi kutoa maoni yao,” alisema Machali.Alisema kama muswada huo ungesomwa kwa mara ya kwanza ungetoa fursa kwa wananchi wengi kutoa mchango wao wa maoni ambayo yangechangia kutungwa kwa Katiba Mpya inayokidhi matakwa ya Watanzania.“Haiwezekani kukusanya maoni katika vituo vya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar tukasema hayo ndiyo mawazo ya Watanzania wote. Nchi hii ni kubwa na hata ninyi wenyewe husema nchi kubwa kwani tuna haraka gani?” alisema Machali.
Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa alisema: “Namshukuru Rais, juhudi hii aliyoifanya, naamini ana nia nzuri nawaomba wabunge wenzangu na Watanzania wenzangu tumsaidie kwa hili kwa sababu mwisho wa siku historia ya Katiba Mpya itaandikwa wabunge walio ndani ya Bunge hili pamoja na Rais wa Tanzania wa Awamu ya Nne.”Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema alisema asingeweza kutoka nje ya Bunge kwani hapo ni mahali sahihi pa kuzungumza kwa niaba ya wananchi wa Vunjo. “Nimejaribu kuangalia kinachotufanya tugombane ni nini, tufarakane ni nini, tuelewane vibaya ni nini?

Nimeangalia hii Tume inayotaka kuundwa, Tume ya Rais, siyo mara ya kwanza nchi hii kuundwa Tume ya Rais na watu hawakufanya maandamano,” alisema akitaja Tume Jaji Francis Nyalali ya 1991 ya kuratibu maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba na mfumo wa vyama vingi au chama kimoja na ya mwaka 1998 ya Jaji Robert Kisanga kutafuta maoni kuhusu muundo wa Muungano. Alisema kwa jinsi mchakato unavyopendekezwa, hana shaka na Katiba itakayopatikana kwani watu zaidi ya 500 watakaounda Bunge Maalumu la Katiba hawawezi kwenda kinyume cha matakwa ya umma.
Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed alisema wabunge wa Chadema wameonyesha moyo wa ubinafsi kwa kuwadharau wabunge kutoka Tanzania Visiwani. Mbunge huyo ambaye alipata kuwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni alikuwa akikosoa hotuba ya Msemaji wa Upinzani kuhusu Katiba na Sheria, Tundu Lissu ambayo ilionyesha wasiwasi kwamba wingi wa wabunge wa CUF katika Bunge Maalumu la Katiba linakipa chama hicho nafasi ya kuwa chama kikubwa cha pili katika Bunge hilo.
Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage alilishambulia Jukwaa la Katiba Tanzania akisema limejivika uwakilishi wa wananchi na kusahau kwamba wabunge ndiyo wenye nafasi hiyo. “Hawa watu wanasema eti wao ni wawakilishi wa wananchi, tangu lini? Wamesahau kwamba sisi ndiyo wawakilishi wa wananchi, hawa wanataka kutupokonya mamlaka tuliyopewa na wananchi,” alisema Rage.
Spika awashangaa
Kitendo cha wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi kususia mjadala wa muswada huo, kimemshangaza Spika wa Bunge, Anne Makinda akisema kimewanyima haki wapigakura waliowachagua kwa lengo la kuwawakilisha.

“Siyo sawa, muswada ndiyo kwanza unajadiliwa na hapo ndipo Bunge linapotunga sheria, mimi nilikuwa natarajia kwamba kutokana na hoja zao hizo, wakati tutakapokaa kama Kamati ya Bunge zima basi kungekuwa na majedwali ya marekebisho ya sheria hii mengi, ili turekebishe lakini sasa sijui sasa hawa (Chadema) wanafanyaje mambo yao,” alihoji Makinda.
Makinda alipuuza tuhuma zilizotolewa dhidi yake kwamba aliingilia utendaji wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheri na Utawala na kuhoji kwamba kama tuhuma hizo ni za kweli kwa nini Lissu aliyesoma maoni ya kambi yake hakuziweka tuhuma hizo katika hotuba yake kimaandishi?
Waziri achangia Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Ummy Mwalimu alielezea kushangazwa kwake na wanaopinga muswada huo kwa kile alichodai wanaipotosha jamii.Mwalimu alitoa kauli hiyo bungeni alipopata fursa ya kuchangia mjadala huo wa kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.“Ninasikitika sana kuona wanasheria wenzangu na watu wanaojiita wanaharakati wanaohoji madaraka ya Rais.
Hawa wanaharakati na sisi wanasheria tunawajibu wa kuilinda Katiba, mnahoji Rais kuunda tume mnataka aunde nani?”“Rais ni mkuu wa nchi, siyo Mwenyekiti wa CCM tu, siyo mtu wa kawaida ndiyo maana tunasema tupitishe huu muswada na tujadili ndipo tuone.”Mwalimu ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), alisema Rais akiteua tume kuna makundi atakayoyaangalia yakiwamo masuala ya jinsia ambayo yako chini ya wizara yake na kuhamasisha wanawake kujitokeza kuunga mkono juhudi hizo.
NCCR Mageuzi
Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema kitendo cha Serikali na wabunge wa CCM kulazimisha muswada huo kusomwa kwa mara ya pili, ni kuwapuuza wananchi na kusema kwamba kama wataupitisha chama hicho kitawashitaki kwa wananchi.“Ule muswada uliletwa kwa mara ya kwanza ukakatiliwa, sababu za kuukataa ni kutaka ufanyiwe marekebisho na uandikiwe kwa Lugha ya Kiswahili kisha urudishwe kwa wananchi ili watu wengi waweze kuuelewa na kutoa mchango wao wa maoni.

Kama wataupitisha watakuwa wamewanyima haki Watanzania na sisi tutakwenda kuwaambia wananchi kuwa wamewapuuza.”Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alisema jana kwamba kupitishwa kwa muswada huo ni kuwasaliti wananchi.“Hili ni tukio la kusikitisha hapa kwetu Tanzania. Inaonyesha sauti ya wengi siyo sauti ya Mungu, bali wachache.”
Imeandikwa na Leon Bahati, Geofrey Nyang’oro Dar na Neville Meena, Dodoma