RAIS Jakaya Kikwete amekataa kumpokea balozi mpya kutoka nchi moja ya kigeni baada ya kubainika kuwa amefunga ndoa na shoga.

Siri hiyo iliwekwa wazi jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe(PICHANI KULIA) alizungumza na waandishi wa habari kuelezea msimamo wa Tanzania kuhusiana na kauli ya Uingereza ya kuzitaka nchi zinazopokea misaada kutoka nchini humo kuhalalisha vitendo vya ushoga.

Membe alisema tukio hilo lililomshtua Rais lilitokea mwanzoni mwa mwaka huu, pale alipopokea barua kutoka nchi moja (hakuitaja) ikimtaka wampokee balozi wao mpya na mkewe, lakini walipobaini kuwa mke huyo ni mwanaume Rais Kikwete alikataa.
Alisema baada ya kugundua hali hiyo, Kikwete akiwa haamini kile alichokisia alitamka maneno mawili “Toba Yarabi” na kuagiza balozi huyo asikubaliwe kabisa.

Waziri huyo alisema hata baada ya nchi hiyo kukataliwa, ilibembeleza sana kwa siku kadhaa ikidai kuwa kusingekuwa na madhara yoyote kwa balozi huyo kufika nchini na mke wake (shoga) na kwamba angetimiza wajibu wake kikamilifu.

“Waling’ang’ania msimamo wao, lakini baada ya siku nne walituelewa na kusema kuwa sisi ni marafiki wao na hivyo waliheshimu msimamo wa Tanzania na kuahidi kuwa wasingemleta tena balozi huyo na mkewe,” alisema.

Membe alisema amelazimika kusema jambo hilo kuonyesha kuwa Tanzania inapinga kwa nguvu zote tabia za ushoga na kueleza kuwa haiko tayari kutunga sheria ya kuruhusu ushoga nchini.





Akizungumza kwa mkazo, Membe alisema Tanzania iko tayari kwa lolote na hata kubaki na umaskini wake kuliko kupokea misaada yenye masharti ya hovyo.

“Tunataka kutunza heshima yetu. Kama wanadhani misaada itatolewa kwa masharti hayo wakae na fedha zao, hatukubali kutekeleza jambo hilo,” alisema.

Akiungana na viongozi wa dini walioitaka serikali isikubali wala kutishwa na nchi hiyo, Membe alisema Tanzania haiwezi kutekeleza sharti hilo hata kama ni maskini na itaendelea kuheshimu misingi ya maadili ya taifa inayokataza mambo ya ushoga.

“Hii ni nchi inayofuata maadili na haiko tayari kupokea ushauri katika suala hilo...hata nchi ikiwa kubwa kiasi gani, linapokuja suala la utaifa, hatutakubali kuyumbishwa hata kidogo,” alisisitiza Waziri Membe.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, hivi karibuni alitishia kusimamisha misaada kwa nchi zinazopinga haki za mashoga na kuzitaka zile zinazopokea misaada kutoka nchini humo ikiwamo Tanzania zikubali sharti hilo.

Membe alisema kuwa staili ya sasa ya kuunganisha misaada na suala la ushoga ni tamko hatari ambalo linaweza kuvunja uhusiano na nchi nyingine.

“Tamko hili linaweza kuvunja Jumuiya ya Madola na ikitokea ikawa hivyo, Waziri Mkuu wa Uingereza anapaswa kuwajibika,” alisema Waziri Membe.
Aliongeza kuwa kati ya nchi 54 za jumuiya hiyo, 13 pekee ndizo zinazounga mkono suala hilo na kuonya kuwa suala hilo si la kushabikia hata kidogo.

Hata hivyo, waziri huyo alisema suala hilo halikuwa ajenda katika mkutano uliomalizika hivi karibuni nchini Australia, bali Waziri Mkuu huyo aliibua katika vikao vya viongozi wakuu wa nchi.

“Suala la ushoga halikuwa ajenda na wala halikuzungumzwa kwenye mkutano ule; alichofanya Waziri Mkuu huyo ni kuibua suala hilo katika vikao vya viongozi walipokuwa wakijadili haki za binadamu. Hii ndiyo sera ya chama chake cha Conservative.

“Hata hivyo jambo hilo lilikataliwa na lilipofika kwenye mkutano walizungumza kwa mafumbo, lakini tulikataa,” alisema.

Alisema sheria za nchi za mwaka 1971 ambazo Tanzania imeziridhia kutoka kwa Waingereza zinakataza suala hilo na kutamka kuwa linapofika suala la ndoa au mahusiano ya kimapenzi linahusisha watu wa jinsia tofauti.



“Wote tunajua msingi wa familia ni mume na mke ambao wanaweza kuzaa watoto...pia sheria ya makosa ya jinai inaeleza msimamo ndio huo, hivyo kwenda kinyume ni makosa ambayo mtu anaweza kufungwa kifungo kisichopungua miaka 30 jela,” alisema na kuongeza kuwa kwa msimamo huo serikali haivitambuia vikundi vya kishoga vilivyoko nchini.