SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF) limesema halikuridhishwa na kiwango cha timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) katika mchezo wa juzi dhidi ya Chad licha ya timu hiyo kufanikiwa kuingia katika hatua ya makundi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 Brazil.

Katika mchezo huo wa marudiano uliochezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Taifa Stars ilifungwa bao 1-0 na kufanikiwa kufuzu kwa kuwa na uwiano mzuri wa mabao ya ugenini kwani katika mchezo wa kwanza uliochezwa N’djamena Ijumaa iliyopita, Stars ilishinda kwa mabao 2-1.

Kutokana na matokeo hayo Taifa Stars sasa itakuwa kundi moja na miamba ya soka barani Afrika timu za Moroco, Ivory Coast na Gambia ambayo nayo si ya kubeza katika kampeni za kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza mwakani.

Akizungumzia mchezo huo mbele ya waandishi wa habari katika makao makuu ya shirikisho hilo Karume Ilala jana Rais wa TFF Leodegar Tenga alisema pamoja na kufanikiwa kufuzu kuingia katika hatua ya makundi lakini lazima wawe wa wazi kuwa timu hiyo ilionesha kiwango cha chini katika mchezo huo.

“Tulitarajia wangecheza vizuri zaidi kuliko walivyocheza jana, lakini kwa bahati mbaya hawakucheza vizuri, lakini ndio kawaida ya mpira,” alisema Tenga.

Tenga alisema kwamba timu iliingia mashindanoni ikiwa na lengo moja tu la kufuzu kuingia katika hatua ya makundi lengo alilodai kuwa limetimia lakini aliwataka makocha na wachezaji wa timu ya Taifa kufanyia tathmini kiwango walichoonesha katika mchezo wa jana.



“Ni wazi hata mchezaji mwenyewe ukitoka uwanjani unagundua kuwa leo sikucheza vizuri, ni nafasi yao kujifanyia tathmini na kubadilika,”alisema.

Alisema ukiangalia mchezo huo utaona ni kama watu wazima walikuwa wakicheza na watoto wadogo kwani timu ya taifa ilionekana kukosa nguvu na kupoteza mipira mingi ya kugombania, hasa ya juu.

Aliongeza kuwa tatizo kubwa lililokuwa likiwasumbua wachezaji wa Stars ni kukosa nguvu na kwamba hilo ni tatizo kwa wachezaji wa Tanzania hata kwa klabu hivyo ni kitu ambacho benchi la ufundi na klabu halina budi kuliangalia kwani nguvu hazijengwi kwa siku mbili.

Tenga alisema hata hivyo kuwa bado wana imani kubwa na timu hiyo kwani inaundwa na wachezaji wengi chipukizi ambao wanahitaji kupewa muda kabla matunda yake hayajaanza kuonekana.

“Angalia wachezaji kama Kapombe (Shomari), Samatta (Mbwana) na Ulimwengu (Thomas) wote hao ni chipukizi na wanaohitaji kupewa muda,” alisema Tenga.

Aliwataka watu kuacha tabia ya kulaumu makocha peke yao bali kuangalia sababu nyingi ambazo zinasababisha timu kufanya vibaya katika mashindano.

Wakati Tenga akisema hayo kocha Mkuu wa Taifa Stars Jan Poulsen aliwalaumu wachezaji wake kwa kushindwa kutumia nafasi walizopata hasa kipindi cha kwanza.

Akizungumza baada ya mechi hiyo juzi Poulsen alisema: “Tulitengeneza nafasi kama saba hivi katika kipindi cha kwanza lakini hatukuweza kuzitumia,”alisema Poulsen.

Alisema kipindi cha pili karibu chote hawakucheza vizuri lakini wakaja kuzinduka katika dakika za mwisho za kipindi hicho wakati tayari walikuwa nyuma kwa bao moja.

Poulsen alisema mchezo ulikuwa mgumu kama alivyoutarajia lakini wana furaha kwa sababu lengo lao la kuingia katika makundi limetimia.