Shughuli ya upigaji kura katika uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, inatarajiwa kuanza asubuhi leo.
Uchaguzi huo wa rais na wabunge ni wa pili kufanyika nchini humo baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka minane iliyopita.
Kulikuwa na wasiwasi kuwa upigaji kura ungechelewa kwa sababu ya matatizo ya miundombinu na ghasia kati ya wafuasi wa wagombea wenye upinzani.
Lakini jana Tume ya Uchaguzi imesema 99% ya vituo vya kupigia kura vilikuwa tayari kwa shughuli hiyo kuanza na kufanikiwa kwake ni ushindi wa demokrasia.
vifaa vya kura
Malori yamekuwa yakisambaza karatasi za kupigia kura katika mji mkuu Kinshasa, wakati ambapo majeshi ya Umoja wa Mataifa na helikopta za jeshi hilo zilisaidia kusambaza vifaa vya uchaguzi katika maeneo ya pembezoni mwa nchi hiyo.Rais anayetetea kiti hicho, Joseph Kabila anakabiliwa na wapinzani wengine kumi katika kinyang'anyiro cha kuingia Ikulu, huku mpinzani wake mkuu akiwa mwanasiasa mkongwe Etienne Thisekedi.
Zaidi ya wagombea 18,000 nao wanawania viti 500 vya ubunge.
0 Comments