Baraza la mawaziri la Ugiriki limeunga mkono mpango wa Waziri Mkuu George Papandreou(PICHANI KUSHOTO) wa kupiga kura ya maoni kuhusu mpango wa kuuokoa uchumi wa Ugiriki.

Aliliambia baraza la mawaziri katika mkutano wa dharura kuwa kura ya maoni ambayo huenda ikapigwa mwezi December itatoa ruhusa iliyowazi ya kutekeleza hatua za kubana matumizi zinazopendekezwa na wanachama wa Muungano wa Ulaya.

Hisa katika masoko zilishuka kwa kiasi kikubwa na hii inafuatia tangazo la kura ya imani ya Ugiriki.

Bw Papandreou anakutana na viongozi wa Ulaya nchini Ufaransa.

Katika mkutano na baraza la mawaziri Jumanne usiku Bw Papandreou aliwaambia mawaziri kuwa serikali inahitaji idhini ya watu wa Ugiriki.

Katika taarifa iliyotolewa na afisi yake Bw Papandreou amesema"Kura ya maoni itakuwa ni idhini na ujumbe uliowazi ndani na nje ya Ugiriki kuhusu mpango wa Ulaya na vile vile kushiriki katika muungano huo."

Bw Papandreou pia amesema uchaguzi wa haraka kutokana na madabiliko ama maamuzi ya bunge utaitumbukiza nchi hiyo katika hali ya kushindwa kulipa madeni yake.


Serikali ya Ugiriki inakabiliwa na kura muhimu ya imani siku ya ijumaa.

Mbunge mmoja kutoka chama kinachotawala cha Pasok amejiuzulu na kupunguza idadi ya wabunge wa chama cha Papandreou kwa watu wawili na kuna wanachama wengine sita kutoka chama hicho wanaomtaka ajiuzulu.

Kufuatia mkutano uliochukuwa saa saba, msemaji wa serikali Elias Mossialos alisema:"Baraza la mawaziri limeonesha kuunga mkono."

"Kura hiyo ya maoni itapigwa hivi karibuni, mara tu baada ya kukamilika mpango wa kuunyayua uchumi wa Ugiriki."

Akizungumza katika televisheni ya taifa siku ya Jumatatu, waziri wa mashauri ya ndani Haris Kastanidis amesema kuna uwezekano kura ya maoni itapigwa mwezi December.

Tangazo la kura ya maoni la Jumatatu lilisababisha bei za hisa kushuka vibaya sana katika masoko ya ulimwengu siku ya Jumanne.

Mpango huu mpya wa kura ya maoni unatishia kuvuruga mpango ulioafikiwa katika kikao cha viongozi wa Muungano wa Ulaya wiki jana unaonuiwa kutatua mzozo wa madeni wa Ulaya.

Viongozi wa Ulaya walikubaliana kuipa Ugiriki mkopo wa euro bilioni 100 na kufutilia mbali nusu ya madeni yake.

Lakini kwa upande wake nayo Ugiriki inapaswa ipunguze matumizi ya umma, ipunguze marupurupu na mishahara na kuwafuta kazi maelfu ya watumishi wa umma.

Kumekuwa na maandamano ya wengi Ugiriki dhidi ya hatua hizo za kubana matumizi.