Na Luqman Maloto(global publishers0 HABARI za kusikitisha ambazo Uwazi peke yake limezipata kutoka India ni kwamba ugonjwa unaomsumbua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe umemtesa kwa muda mrefu.
Kutokana na hali halisi ya ugonjwa huo na historia ya jinsi Zitto alivyoanza kuumwa, ni wazi kuwa hata uzima wake leo ni Mungu tu.
Zitto, anaumwa Sinusitis lakini ugonjwa huo umekomaa na kufikia kiwango cha juu ambapo kitaalamu unaitwa Chronic Sinusitis.
Mbunge huyo ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, anakiri kuwa Sinusitis imemtesa kwa muda mrefu na alikuwa hajui na kufafanua kwamba ameshapoteza fahamu mara nne.
“Nimekuwa nikisumbuliwa na kichwa kwa zaidi ya miaka 10, kipindi hicho, nimepoteza fahamu na kuanguka mara nne,” alisema Zitto.
Kaka wa Zitto, Salum Mohamed ambaye ndiye anamuuguza nchini India, ameliambia Uwazi kuwa mdogo wake anasumbuliwa na tatizo la kichwa kwa miaka mingi.
“Najua kuna mengi yanasemwa, watu wanatafuta mchawi, hapa hakuna mchawi, Zitto anaumwa kichwa kutokana na kipimo maalum alichofanyiwa na imegundulika hivyo,” alisema Salum.
Uwazi lina picha ya Zitto akifanyiwa kipimo kinachoitwa CT Scan ambacho ndicho kilibaini ugonjwa huo.
KUHUSU SINUSITIS
Kwa mujibu wa daktari mtaalamu wa magonjwa ya kichwa nchini India, Ramendra Mukhesh, Sinusitis ni ugonjwa hatari ambao unaweza kumsababishia mtu kuchanganyikiwa na akili au pengine kuwa kipofu na baadaye kifo.
Dokta huyo alisema kuwa Sinusitis ni ugonjwa unaoshambulia vinafasi wazi (sinus) vilivyomo katika fuvu la kichwa cha binadamu kando ya pua ambavyo kazi yake ni kumfanya mtu akimudu kukibeba kichwa chake bila kukiona ni mzigo.
“Vijinafasi hivi vikishambuliwa na bakteria au wadudu wengine wowote huvimba (inflammation) na kukosa hewa hali ambayo hufanya mtu kupata maumivu makali ya kichwa na muda wote kusikia pua zake zimeziba (congestion),” alisema Dk. Mukhesh na kuongeza:
“Mtu yeyote mwenye dalili hizi anatakiwa kutibiwa haraka kwa kupewa dawa za kuua wadudu na kupunguza uvimbe, kama ugonjwa huu ukipuuzwa huingia katika hatua mbaya iitwayo Chronic Sinusitis, hapo ugonjwa unakuwa umekaa muda mrefu kwenye kichwa cha binadamu.”
Dokta huyo alisema, vijinafasi hivyo ambavyo kitaalamu huitwa Sphenoid, Frontal na Ethmoid, vimetenganishwa na ukuta mwembamba sana katikati ya ubongo wa binadamu.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Mukhesh alisema, mgonjwa asipotibiwa mapema wadudu wanaweza kupenya na kuingia kwenye ubongo na kusababisha jipu (Abscess) kushambulia ukuta wa ubongo (meningtis).
Athari nyingine ambayo ilitajwa na daktari huyo ni kwamba ugonjwa usipodhibitiwa haraka unaweza kusababisha mishipa ya damu kuziba (thrombosis) na hatimaye mgonjwa kupatwa kiharusi.
NI MUNGU TU
Kwa mujibu wa maelezo ya Dk. Mukhesh, ni wazi kwamba Mungu amempigania kwa muda mrefu Zitto ambaye ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
Uwazi linazo ‘data’ kuwa Sinusitis ilishafikia hatua mbaya ndani ya kichwa cha Zitto kiasi cha kuifanya mishipa ya damu kuziba Salum (kaka wa Zitto) alimueleza mwandishi wetu akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, kitengo cha dharura kuwa madaktari walifupisha maelezo kwa kusema, mishipa ya damu imevuja.
“Hili tatizo litasababisha kupelekana nje. Madaktari baada ya kumfanyia CT Scan wanasema mishipa ya damu imeziba,” alisema Salum.
KUZIMIA MARA NNE
Katika taarifa yake aliyoitoa kwa Watanzania wikiendi iliyopita, Zitto alisema kuwa mara ya kwanza alizimia mwaka 2000.
“Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2000, nilipoteza fahamu nikiwa Mwanza nilipokuwa kwenye Mkutano wa Vijana wa National Youth Forum.
“Nilipoteza tena fahamu kwenye mkutano kama huo wa vijana mwaka 2001 mjini Dodoma lakini ilikuwa usiku, mara ya tatu ilikuwa Dar es Salaam mwaka 2002.
“Mara ya nne ni mwaka 2010, nilikuwa bungeni. Nilipoteza fahamu siku ya kupitisha muswada wa madini,” alifafanua Zitto.
0 Comments