Aidha, wabunge wametaka waliokubali kuchangia fedha za kusaidia upishaji wa bajeti ya madini pamoja na watumishi wengine waliohusika katika ubadhilifu huo waondolewe katika utumishi wa umma na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Hali kadhalika, wametaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima, kuwajibika kuhusiana na ubadhirifu huo.
Waliyasema hayo wakati wakichangia katika taarifa ya Kamati Teule iliyoundwa na Bunge kwa ajili ya kuchunguza sakata la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwezesha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ipite.
Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli, alisema nchi inanuka rushwa na kwamba tatizo hilo limepiga hodi hadi Ikulu. Alisema haiwezekani anachomoka mtu kutoka Ikulu na kuita vyombo vya habari ili kumsafisha mtu ambaye ni mwizi. “Haiingii akilini unamsafisha mtu ambaye ni mwizi kwa msingi gani hii ni kansa, ni ukimwi nchi hii imebaki mifupa tu minofu yote imeliwa na wakubwa,” alisema Lembeli.
Alishangazwa na hatua ya Ngeleja kumpokea kwa shangwe Jairo siku aliporejeshwa kazini na Luhanjo. “Ngeleja alipopelekewa sh. milioni 4 aliuliza zimetoka wapi?...Busara kulinda heshima yako, familia yako, chama chako cha CCM, aliyekuteua, Bunge, Wizara ya Nishati na Madini mimi nitakuwa wa kwanza kukushauri kuachia ngazi,” alisema na kuongeza: Kama huku ndani tunalindana basi hatupaswi kuwa huku ndani PM (Waziri Mkuu), mueleze mheshimiwa Rais kuwa hawatoshi wizara zote…usiposafisha mji wako unasubiri nani akusafishie?”
Alimtaka Ngeleja kutumia busara zake na kujiuzulu kama ilivyofanyika kwa mawaziri waliotangulia Mwinyi ( Rais wa Awamu ya Pili Alli Hassan Mwinyi), na Dk. Juma Ngasongwa.
Mbunge wa Singida Mashariki, (Chadema), Tundu Lissu, alisema Jairo na Luhanjo wametenda uhalifu washughulikiwe kama wahalifu. Alisema pia wakuu wa taasisi zilizohusika na uchangiaji wa fedha kwa wizara hiyo, wakati serikali imekataza kufanya hivyo nao washughulikiwe kama wahalifu wengine.
Alisema Ngeleja na Malima walipokea fedha hizo shilingi milioni nne, kama fedha za honoralia wakati Bunge limekuwa likiwalipa posho za kujikimu.
Alisema katika mgao wa fedha hizo, Mbunge wa Igunga (CCM), Dk Dallay Kafumu, wakati akiwa Kamishna wa Nishati na Madini, alipata mgawo wa sh. 540,000.
Alimtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kumshauri Rais Jakaya Kikwete, ili kumwajibisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), na kumuundia Tume ya kumchunguza.
Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango, aliikosoa serikali yake kuwa imetoa mwanya kwa makatibu wakuu kuwa na mamlaka yote ya fedha na kuwaweka kando mawaziri ambao ndio wakuu wa wizara.
Alisema amekuwa akishangaa kwanini makatibu wakuu na mawaziri wengi hawaelewani lakini alipochunguza alibaini linasababishwa na mfumo mbovu uliowekwa na serikali kuhusiana na masuala ya fedha.
“Waziri Mkuu kakae na Rais ili muangalie tatizo hili. Serikali wekeni mifumo ambayo itafanya fedha zilindwe vizuri…Mnatakiwa kuyapa umuhimu mambo haya tunayoyazungumza na msije mkatuzungusha hapo,” alisema Kilango.
Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo, alipinga mawaziri hao kuwajibika. Alisema kuwa mfumo umewapa mamlaka makubwa makatibu wakuu na hivyo kufanya kutokuwa na ulazima kwa waziri kujua kinachoendelea wizarani kuhusiana na masuala ya fedha.
“Mnajua mimi sibembelezeki, si hongeki sifanyiki, sishauriki lakini lazima niseme ukweli taratibu zetu si nzuri kuwataka wajiuzulu ni kuwaonea bure,” alisema.
Mbunge wa Karatu (Chadema), Israel Natse, alitaka serikali kujitafakari upya na kutaka kuangalia wizara nyingine kwa sababu zimeoza. Alisema serikali ambayo inasimamiwa na Bunge ifike mahali iwajibike na waziri awajibike kwa kuwa ndiye msimamizi mkuu wa wizara. “Inasikitisha kuona kuwa muhimili wa Bunge unatumiwa na serikali katika matumizi mabaya ya fedha,” alisema.
Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed, alisema mfumo wa bajeti una matatizo na kushauri kufanyiwa marekebisho. Alisema hali hiyo inafanya fedha za umma kutumiwa bila kufuata utaratibu.
Aidha, alisema kuwaleta watumishi wa wizara hiyo zaidi 230 kupitisha bajeti ni suala la matumizi mabaya ya fedha za umma na kutaka Mhasibu Mkuu wa wizara hiyo naye kuwajibishwa kwa jambo hilo.
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, alimtaka Rais kuwaondoa watu wanaoichafua taswira ya Ikulu. Alisema kwa kasi hiyo hiyo aliyonayo Rais anatarajia atawatendea haki Watanzania kwa kuwaondoa watu wanaochafua taswira nzuri ya uongozi wake.
Alisema Rais awaondoe watendaji hao na watendaji waadilifu wapate nafasi za uongozi katika nchi. Alisema awamu ya nne imekuwa ikiwashughulikia watu wasio waadilifu na kumtaka Rais Kikwete kumweka pembeni Luhanjo. “ Rais amtendee haki kwa kumfikisha mahakamani Jairo….Kuacha kuwapeleka Mahakamani ni kutowatendea haki Watanzania,” alisema Sendeka na kuongeza kuwa:
“Wahujumu wakubwa wa Tanzania, wawajibike na wakabidhi barua zao leo hii wawasubiri Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini)…Na nyie Takukuru nategemea mtawatendea haki Watanzania kuhusiana na suala hili,”alisema.
Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe, alitaka watu wanaohusika na ubadhirifu huo wachukuliwe hatua. “Hadi leo watu bado wako serikalini wanafanya kazi huku mtu mmoja akisimamishwa na kama atashtakiwa huyu basi na wale wengine waliohusika washtakiwe,” alisema.
Alihoji ni serikali gani ambayo inashindwa kuwawajibisha watu waliotenda makosa hayo. Alisema semina imekuwa chanzo cha ubadhirifu wa fedha na kuitaka serikali kutoa tamko kuhusiana na semina zinazoiendeshwa wizara pamoja na taasisi za umma.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Mosses Machali, alisema serikali inapaswa kutoa hati ya kukamatwa mara moja kwa watumishi wote waliohusika na ubadhirifu huo. “Kama wezi wa kuku wanashtakiwa na kufungwa kwanini hawa wezi wa mamilioni wasikamatwe na kushtakiwa. Kama hamtawakamata hawa laana ya Watanzania itakuwa juu yenu,” alisema.
Aidha, alisema Katibu Mkuu Kiongozi, Philimon Luhanjo, anatakiwa kushtakiwa na kufukuzwa kazi kwa kosa la kuingilia haki na madaraka ya Bunge. Pia alitaka mawaziri wa Nishati na Madini, kuwajibika kwa kukubali kuchukua shilingi milioni nne kila mmoja bila kuhoji zilikotoka.
Kuhusu kughushiwa kwa malipo ya fedha ya semina ya wabunge iliyofanywa na wizara hiyo, Machali alihoji serikali inasubiri nini kuwashtaki watu waliogushi malipo.
Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje, alitaka waziri kuwajibika kwa kuwa yeye ndiye msimamizi mkuu wa shughuli zote zinazoifanyika wizarani. Alisema hatua hiyo inataka kuelewa kinachoendelea kila siku katika wizara yake na pia kukubali kusaini shilingi milioni nne alizopewa na Katibu Mkuu wa wizara yake.
“Ngeleja amepokea shilingi milioni nne, anajua lazima awajibike, wanajua ama mawaziri hawaelewi waraka wa serikali,” alisema. Alihoji kuhusiana na wizara hiyo kuwaleta watumishi 243 kwa ajili ya bajeti ambapo alisema hata kipofu lazima agundue kuwa huo ni wizi.
Aliwataka mawaziri wa Nishati na Madini, kujifunza kufanya maamuzi magumu na kwamba hata kama wana ndoto za kuwa Rais wanaweza kukipata cheo hicho katika siku zijazo.
Mbunge wa Kasulu Vijijini (NCCR-Mageuzi), Agripina Buyogela, alisema Waziri Mkuu amezidi kuwa mpole na kwamba utamfikisha mahali pabaya. Alimtaka Waziri Mkuu kukaa na washauri wake wenye mapenzi mema na nchi, ili waweze kuzipitia wizara zote nchini.
“Watendaji wapo tofauti na mawaziri, Waziri Mkuu uwe mkali ili watendaji wabadilike,” alisema Buyogela.
Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi, alisema watu wanapotoa taarifa kuhusiana na ufisadi hiyo ni dalili ya watu kuchoshwa na yanayoendelea serikalini. Alitaka waliohusika na ubadhirifu huo kukatwa fedha zote katika mishahara yao na kurejeshwa serikalini kabla ya kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, alisema kutokana na ukubwa wa suala hilo ni vigumu kulitolea uamuzi jana bungeni na kutaka serikali ipewe muda wa kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na kamati hiyo.
Alisema katika Bunge lijalo la sita, serikali itawasilisha taarifa ya maazimio yaliyotekelezwa.
0 Comments