RAIS Barack Obama wa Marekani ametuma salamu za pongezi na za kuitakia baraka Tanzania
wakati itakapoadhimisha miaka 50 ya Uhuru Ijumaa wiki ijayo.
Aidha, Rais Obama ameihakikishia Tanzania kuwa Marekani itaendelea kuwa rafiki na mshirika wa kuaminika katika jitihada za kuhakikisha Watanzania wanajiletea maisha bora kwa amani.
Katika salamu zake jana kwa Rais Jakaya Kikwete, Rais huyo wa Marekani alitumia lugha ya Kiswahili kuitakia baraka Tanzania: “Mungu awabariki” na kufuatiwa na tafsiri ya maneno hayo kwa Kiingereza.
Rais Obama aliongeza kuwa umbali mkubwa wa kijiografia kati ya Tanzania na Marekani unazidi kupungua kwa sababu ya uhusiano wa karibu kati ya Wamarekani na Watanzania.
“Hali ya kuwa anuwai ya Taifa lako, kama ilivyo ya kwetu, ni chimbuko na msingi wa nguvu zitakazoipitisha Tanzania katika mabadiliko mengi na changamoto nyingi zinazoikabili nchi yenye demokrasia inayopanuka,” alisema Rais Obama katika salamu hizo.
Tanzania na Marekani zimekuwa marafiki wa muda mrefu tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais John Kennedy wa Marekani katika miaka ya sitini.
Viongozi wa nchi hizo mbili wamekuwa wakitembeleana ambapo wa Tanzania walishafanya ziara mbalimbali nchini humo, huku Rais wa zamani wa nchi hiyo George W. Bush akifanya ziara ya kwanza nchini mwaka 2008.
Pia Rais Bill Clinton alitembelea Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 2000, akaja tena mwaka 2005, 2007 na mwaka jana akiwa ameshastaafu.
Mwaka 2008 Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa Sullivan uliofanyika kwa mafanikio makubwa mkoani Arusha ambapo raia wenye asili ya Afrika waishio Marekani walihudhuria.
Katika kuonesha uhusiano na mshikamano uliopo baina ya Marekani na Afrika hususan Tanzania, Rais Bush kuanzia leo hadi Desemba 5 atakuwa na ziara Afrika ambapo akifuatana na
mkewe Laura, atazuru Tanzania, Zambia na Ethiopia.
Kwa mujibu wa taarifa ya kituo chake kilichoko Dallas, Texas, safari hiyo inalenga kuendelea kujitolea kwake kwa watu wa Afrika kwa njia ya kazi ya mpango maalumu unaoendeshwa na
taasisi yake ya GWBI hususan katika sekta ya afya.
Hata hivyo, mbali na uhamasishaji, pia taarifa hiyo ilieleza kwamba, Bush atawasilisha ujumbe maalumu kwa kushirikiana na wadau wengine wanaojihusisha na mapambano dhidi ya saratani, Ukimwi, malaria na magonjwa mengine chini ya usimamizi wa Serikali ya Marekani.
0 Comments