KILA Mtanzania atakuwa na kitambulisho cha Taifa kufikia mwaka 2015 ambacho kitatolewa bure na Serikali, na tayari watumishi wa umma wameanza kujaza fomu za utambuzi na usajili na ifikapo Aprili mwakani, watakuwa na vitambulisho hivyo, imefahamika.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), baada ya wafanyakazi wa Serikali, watafuatiwa wanafunzi, wafanyabiashara na hatimaye umma kwa ujumla utafikiwa na kazi hiyo muhimu kwa Taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali
vya habari Dar es Salaam jana kuhusu maendeleo ya mradi wa vitambulisho vya Taifa, alisema
ingawa vitatolewa bure, kwa ye yote atakayepoteza atalazimika kuvilipia.
Mradi mzima unatarajiwa kugharimu kiasi cha Sh bilioni 350.
Maimu alisema ni lengo la Serikali kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na kitambulisho cha
Taifa ifikapo mwaka 2015 na hilo litasaidia kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura, na hivyo kuipunguzia mzigo mkubwa Serikali katika kuboresha daftari hilo kila wakati wa uchaguzi unapowadia.
“Kwa kuwa zoezi la utambuzi na usajili litafanyika kwenye maeneo yenu nawaomba mtoe
ushirikiano wa kutosha kwa wananchi wote na niwakumbushe kuwa huduma hii ni bure
kwa mujibu wa maagizo ya Baraza la Mawaziri, na hivyo Serikali haitarajii mtendaji yeyote kuomba au kupokea chochote au kuweka tozo.
“Tunawasihi wananchi na wageni, wasikubali kudanganywa au kulipa fedha zozote kwani
kitambulisho ni bure na huduma zote zinazoambatana na zoezi hili ni bure. NIDA haitasita
kuchukua hatua za kisheria kwa ye yote atakayebainika kukiuka uratatibu huu.”
Alisema wameanza na wafanyakazi wa Serikali kwa sababu vitambulisho kwao si tatizo kwa maana ya mfumo walionao una urahisi katika kuwashughulikia, lakini zaidi, itasaidia katika kudhibiti watumishi hewa.
“Hawa kwao kitambulisho kwao kidogo si tatizo, kwani wana mifumo mizuri na hawa tunataka kuwatumia kama majaribio kwa mradi huo. Lakini zaidi, itasaidia katika kudhibiti tatizo la watumishi hewa serikalini,” alisema Maimu na kuongeza kuwa watafuata wanafunzi kwa sababu ya kusaidia katika suala la mikopo ya elimu ya juu na kwa wafanyabiashara ili kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi na kusaidia kuongeza mapato.
“Kutokana na ratiba yetu ya utekelezaji, tutaanza kutoa vitambulisho kwa awamu ya kwanza
mwezi Aprili 26, 2012 wakati wa maadhimisho ya sherehe za Muungano kwa watumishi wa
Serikali ambao tayari usajili umeanza,” alieleza Maimu na kuongeza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, Mamlaka itatoa vitambulisho katika makundi matatu; Watanzania, wageni wakazi na wakimbizi.
“Tutatoa vitambulisho hata kwa mwizi, kwa sababu moja ya faida kuu za mradi huu ni kudhibiti
suala la usalama wetu kwa kila pointi. Ndiyo maana dhana kuu ya mfumo huu inatakiwa ijibu maswali makuu manne; nani ni nani; yuko wapi; anamiliki nini na anafanya nini”alieleza mkurugenzi huyo.
Aliongeza kuwa vitambulisho hivyo katika eneo la usalama, vitasaidia kuimarisha usalama
wa raia na mali zao na kupunguza vitendo vya uhalifu na hasa unaofanywa na raia kutoka
nchi jirani na wafungwa waliomaliza adhabu zao au kuachiwa huru kwa msamaha wa Rais.
“Ni wazi kuwa udhibiti wao umekuwa mgumu kutokana na kushindwa kuwatambua. Pia itasaidia kuweka kumbukumbu za matukio ya uhalifu katika daftari,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa NIDA.
Alisema baada ya usajili kukamilika, jukumu kubwa litakalofuatia ni uhakiki wa taarifa za makazi, umri na uraia wa mwombaji aliyesajiliwa ili kupata uhakika wa taarifa zake kwa lengo la kumpatia kitambulisho kinachowiana na kundi lake.
Katika udahili, mwombaji atatakiwa kuthibitisha kama amekuwa akiishi Tanzania kwa kipindi kisichopungua miezi sita; uthibitisho wa umri wa miaka 18 na uthibitisho wa uraia wake.
Aidha, viambatanisho muhimu vitahitajika ambavyo ni cheti cha kuzaliwa; cheti cha ubatizo/falaki; kitambulisho cha Mpigakura; pasipoti ya Tanzania na cheti cha kuhitimu elimu ya msingi.
“Jukumu hili ni la muhimu sana na linatakiwa kufanywa kwa umakini mkubwa bila kuharakishwa kwani uharaka kidogo tu unaweza kabisa kuharibu zoezi zima,” alifafanua
mkurugenzi huyo.
Alisema ili kufanikisha kazi hiyo, wanashirikiana kwa karibu sana na Serikali za Mitaa kwa
lengo la kutambua makazi halali ya mwombaji; Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa lengo la kutambua umri wa mwombaji na Idara ya Uhamiaji kutambua na kubaini uraia wa
mwombaji.
Aidha, alisema katika mkutano ujao wa Bunge, wanatarajiwa utapelekwa muswada wa
mabadiliko ya sheria ambayo itakuwa ni lazima kwa kila mtu anayeishi nchini, kuwa na kitambulisho hicho cha kudumu ambacho kadi yake itakuwa ni ya miaka 10.
NIDA imeingia mkataba na mkandarasi wa vitambulisho hivyo, Kampuni ya IRIS Corporation
Berhad ya Malaysia tangu Aprili 21, mwaka huu.
Mshauri mwelekezi wa mradi huo ni Kampuni ya Gotham International Ltd (GIL), na tayari Mamlaka hiyo imepata viwanja katika wilaya zote nchini kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya ofisi za usajili wilayani wakati kituo kikuu cha kuhifadhi takwimu zote za nchi kitakuwa Kibaha, Pwani.
Maimu alisema kulikuwa na uchelewaji wa kutoa fedha kwa mkandarasi kuanza kazi, lakini
tayari Oktoba mwaka huu amekabidhiwa fedha hizo baada ya kuidhinishwa na Bunge na tayari
ameleta mashine kuanza kazi ya mradi huo uliosubiriwa kwa zaidi ya miaka 15 sasa na kugubikwa na maneno mengi katika mchakato wake.
|
0 Comments