Akizungumza katika mahojinao na NIPASHE juzi, Magoba alisema kimsingi siyo kosa kwa wabunge kuongezewa posho kwani kiwango wanacholipwa kilikuwa kidogo mno ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Magoba ambaye pia aligombea ubunge Jimbo la Rungwe Magharibi katika uchaguzi wa mwaka jana na kushika nafasi ya pili katika mchakato wa kura za maoni, alisema nchi kama Kenya wabunge wanalipwa mshahara Shilingi milioni nane kwa mwezi wakati wabunge wa Tanzania wanalipwa Sh. milioni 2.5 tu.
Alisema madai yaliyotolewa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, kwamba gharama za maisha zimepanda Dodoma ni kweli kwa sababu hivi sasa mji wa Dodoma umekuwa na vyuo vingi ambapo idadi ya watu imeongezeka hivyo ni lazima gharama za vitu zipande maradufu.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake TLP Mkoa wa Mbeya, Sharifa Lema, alisema anapinga kitendo cha wabunge kuongezwa posho kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 200,000 kwani ni kiwango kikubwa sana wakati hali ya uchumi wa Tanzania inazidi kuporomoka.
Lema alisema wapo watumishi ambao wanafanya kazi kubwa kuliko hata wabunge kama vile walimu lakini baadhi yao mishahara yao haizidi Sh. 200,000 kwa mwezi kwa hiyo kitendo cha wabunge kuongezewa posho kitasababisha hata kupanda kwa bei za bidhaa na watakaoathirika ni wananchi wa kawaida.
Alisema wananchi walichukulie suala la wabunge kuongezewa posho kama ajenda muhimu ambapo uchaguzi mkuu wa 2015 wasikubali kuchagua wabunge ambao watakwenda bungeni kwa ajili ya kujenga hoja za kuongezewa posho badala ya kufikiria kuwaletea maendeleo wananchi.
Naye Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Wilaya ya Rungwe, Anyimike Mwasakilali, alisema kitendo cha wabunge kuongezewa posho huo ni sawa na usaliti kwa wapiga kura wao kwa sababu hawakuwachagua kwenda bungeni wakaishinikize serikali kuwaongezea posho.
Mwasakilali ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kawetele Tukuyu mjini, alisema wananchi wawahoji wabunge wao watakapokwenda majimboni kwenye ziara ni kwanini wametetea suala la wao kuongezewa posho wakati hadi sasa baadhi yao hakuna maendeleo yoyote waliyoyafanya katika kipindi hiki.
0 Comments