Makazi ya Nelson Mandela yaidaiwa kurekodiwa.
Polisi wa Afrika Kusini wameharibu kamera ambazo wanasema zilikuwa zikirekodi makazi ya Nelson Mandela katika kijiji cha Qunu Eastern Cape kinyume cha sheria.
Msemaji wa polisi Vishnu Naidoo ameiambia BBC kuwa vyombo viwili vya habari vinafanyiwa uchunguzi.Kamera hizo zilikuwa nyumba jirani na zimekuwa zikiendelea kurekodi moja kwa moja makazi ya Rais huyo wa zamani, alisema.
Kiongozi huyo mashuhuri wakati wa vita vya ubaguzi wa rangi mwenye umri wa miaka 93, amekuwa akionekana mdhaifu tangu alipostaafu shughuli za umma mwaka 2004.
Kanali Naidoo amesema kwa sheria za Afrika Kusini, ni kosa kupiga picha au video makazi ya marais na marais wa zamani kwa kuwa wanachukuliwa kuwa ‘ni nguzo muhimu za taifa’
Polisi walipewa taarifa kuhusu kamera hizo karibu wiki moja iliyopita, alisema.
"Polisi wetu walipofika pale waligundua kuwa kweli kamera zilikuwepo na makazi hayo yakirekodiwa moja kwa moja," alisema Naidoo.
'Hazikuwa zikifanya upelelezi'
Jirani ambaye anaishi mkabala na Bw Mandela, Nokwanele Balizulu, alisema aliwaruhusu mashirika mawili ya habari ya kimataifa kuweka kamera zake kwenye nyumba yake, shirika la habari la Afrika Kusini la Times Live limeripoti."Nilikubali kamera hizo ziwekwe, lakini siwezi kusema chochote kingine," alinukuliwa akisema.
Baada ya uchunguzi kukamilika polisi watampelekea mwendesha mashtaka "kujua iwapo kuna kinachofuata ", alisema kanali Naidoo.
Amekataa kutaja majina ya vyombo vya habari vinavyoshukiwa kuweka kamera hizo kijijini Qunu, alikokulia Bw Mandela.
Lakini shirika la habari lenye makao yake makuu nchini Marekani AP limethibitisha kuwa ni mojawapo ya vyombo hivyo vya habari.
"Kamera za video za AP moja ilikuwekwa kitambo huku mamlaka husika zikiwa zinafahamu. Lakini sasa kamera hiyo imeondolewa ," Mkurugenzi wa AP wa Uhusiano na habari Paul Colford alisema katika taarifa.
"Haikuwa inafanya kazi, haikuwa inachunguza na kurekodi makazi ya Bw Mandela kama baadhi ya watu walivyotafsiri. Ni desturi ya AP na vyombo vingine vikubwa vya habari kufuatilia habari zinazohusu viongozi maarufu duniani."
Bw Mandela aliachia madaraka kama Rais wa Afrika Kusini mwaka 1999 baada ya kutumikia muhula mmoja na kumuachia Thabo Mbeki.
0 Comments