Moja ya matrekta yaliyokopeshwa kwa wanachama wa Idodi Saccos, likifanyiwa majaribio kwa ajili ya msimu huu wa kilimo.

AWAMU ya pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA II) ni mwendelezo wa jitihada za serikali katika kuharakisha ukuaji wa uchumi na kupambana na umasikini nchini.

Moja ya maeneo ambayo mkakati huu unasisitiza ni kutilia mkazo maeneo ya kipaumbele katika ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini. Mwaka 2010/11, Serikali ilibainisha maeneo ya kipaumbele ya Kitaifa kwa kuwekeza katika shughuli za kiuchumi na kijamii zenye kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi kwa upana zaidi.

Maeneo hayo ni Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Miundombinu, Ardhi, Nishati, Viwanda na vitambulisho vya kitaifa. Sekta za kijamii (elimu, afya na maji) zitaendelea kupewa umuhimu katika mgawo wa fedha.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ina malengo ya kuwaletea wananchi maisha bora na mazuri, kuwa na uongozi bora na utawala wa kisheria, na kujenga uchumi imara wenye uwezo wa kukabiliana na ushindani.

Katika makala haya nitazungumzia taarifa ya maendeleo ya sekta ya kilimo mkoani Iringa
pamoja na mchango wake katika maendeleo ya mkoa na watu wake kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Hivi sasa sekta ya kilimo na mifugo inaajiri asilimia 85 ya wakazi wa mkoa huu na inachangia zaidi ya asilimia 50 ya pato la mkoa. Sekta hii ndiyo inayotegemewa kwa uhakika wa chakula na lishe bora kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa, na kuongeza kipato cha kaya na mkoa.



Mkoa wa Iringa una wakazi zaidi ya milioni 1.7 (pamoja na Mkoa wa Njombe) na una hekta milioni 4.1 zinazofaa kwa kilimo. Hata hivyo eneo linalotumika hadi hivi sana kwa shughuli za kilimo yaani mazao, mifugo, upandaji miti, ufugaji nyuki na uvuvi likakadiriwa kuwa hekta
milioni 1 tu ambayo ni sawa na asilimia 24.3 ya eneo linalofaa.

Mkoa una hekta 67,705 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na zinazotumika hadi sasa ni hekta 25,784 tu, sawa na asilimia 38 ya eneo lote linalofaa. Hiyo inaonesha fursa kubwa iliyopo mkoani Iringa ya uwekezaji katika kuendeleza kilimo na sekta ya maliasili, japokuwa haitumiki vizuri.

Kwa wastani uzalishaji wa mazao ya chakula, biashara na mazao ya mifugo na hata maliasili, bado ni wa kiwango cha chini, ukilinganisha na kiwango kinachoweza kufikiwa iwapo utaalamu utatumika kwa kufuata kanuni za kilimo na ufugaji bora.

Taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa msimu huu wa 2011/12, inaeleza kuwa mvua kwa ukanda wa Kusini, zitakuwa za wastani hadi juu ya wastani katika baadhi ya maeneo.

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa (Huduma za Uchumi), Adam Swai, anasema msimu wa kilimo wa 2011/12 ulianza mwezi Julai 2011 kwa kuwepo kwa mvua chache mwezi Novemba, ikilinganishwa na msimu uliopita ambapo mvua zilianza Desemba.

Dalili za maeneo mengi mkoani Iringa kukumbwa na njaa, zimeanza kupungua, baada ya mvua kuanza kunyesha mfululizo kuanzia mwezi Novemba mwaka huu. Anasema kutokana na taarifa za halmashauri zote mkoani Iringa, hadi sasa asilimia 20 ya maeneo yanayotarajiwa
kulimwa , yameshalimwa na asilimia tano ya mashamba hayo yamepandwa mazao ya aina mbalimbali.

Mazao yanayoendelea kupandwa kwa kipindi hiki ni pamoja na mahindi, maharage, alizeti, mtama na viazi. Swai anasema mkoa una jumla ya mawakala 514, wanaofanya kazi ya
kusambaza pembejeo za kilimo.

Kati yao mawakala 390 ndio wanaofanya kazi ya kusambaza pembejeo katika ngazi ya vijiji na kata, kwa utaratibu wa mfumo wa ruzuku ya pembejeo. Mahitaji ya mbolea kimkoa ni tani 89,820.

Katika msimu huu wa kilimo wa 2012/12, mkoa umepokea mgawo wa vocha 693,000 za mbolea za kupandia na kukuzia na mbegu zenye ruzuku ya serikali, ambapo jumla ya kaya 231,000 watanufaika na utaratibu huo.

Kuhusu bei za vocha za ruzuku, Swai anasema vocha ya mbolea ya kupandia (DAP) ina thamani ya Sh 28,000, ya mbolea ya kukuzia (UREA) ina thamani ya Sh 18,500, ya mbegu za mahindi chotara ina thamani ya Sh 20,000 na ya mbegu za mpunga thamani yake ni Sh 12,000.

“Nakala za vocha zote 693,000 zilizopokelewa mkoani zimeshagawanywa kwa kamati za vocha za wilaya na kamati za vocha za vijiji zinaendelea na ugawaji wa nakala hizo za vocha kwa wakulima walengwa ili waweze kupata pembejeo kutoka kwa mawakala husika baada ya kutoa kiasi wanachotakiwa kuchangia,” alisisitiza.

Akizungumzia utekelezaji wa malengo ya kilimo kwa mazao ya chakula na biashara kwa msimu
huu, Swai anasema mkoa una malengo ya kulima jumla ya hekta 975,567 na matarajio ya mavuno yanakisiwa kufikia tani 2,474,991.

“Tofauti na msimu uliopita ambapo mkoa ulifanikiwa kulima jumla ya hekta 858,838 zilizotoa mavuno ya tani 1,439,217 ambazo kati yake tani 873,510 zilikuwa za mazao ya chakula ambayo ni pamoja na mahindi na mpunga,” anasema.

Kuhusu hali ya chakula mkoani Iringa, Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Iringa, Shanel Nyoni, anasema
mahitaji ya chakula kwa wakazi wote mkoani Iringa ni wastani wa tani 455,000, hivyo kuufanya mkoa ujitosheleze kwa chakula kwa kuwa na ziada ya zaidi ya tani 400,000.

Hata hivyo, anasema katika msimu wa kilimo uliopita, yapo maeneo yaliyokumbwa na ukame na hivyo kusababisha yawe na upungufu mkubwa wa chakula. “Maeneo hayo ni pamoja Kata ya Malengamakali na Kihorogota katika Tarafa ya Isimani wilayani Iringa na Tarafa ya Mahenge wilayani Kilolo,” anasema.

Anasema hadi kufikia Desemba mwaka huu, mkoa umeshapokea jumla ya tani 5,375 za mahindi ya msaada kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, zilizogawanywa kwenye maeneo yenye upungufu wa chakula.

Akizungumzia mafanikio katika kuboresha kilimo cha mazao ya biashara, Nyoni anasema juhudi za kufufua na kupanua kilimo cha Pareto, zinaonekana kufanikiwa baada ya kiwanda cha Pareto Mafinga kupata mbia kutoka Marekani McLaughlin Gormley King (MGK).

Kabla ya kupatikana kwa mwekezaji huyo, soko la Pareto Tanzania liliwahi kuyumba kati ya
mwaka 1998 na 2005, baada ya wawekezaji wa awali kushindwa kununua zao hilo, na
kuwasababishia hasara wakulima ambao hivi sasa wameanza tena kulima zao hilo, baada ya kuhamasishwa na Serikali, kufuatia soko kurejea Mwaka 2006 wakati Kampuni ya MGK ikinunua kiwanda cha Mafinga, bei ya pareto ilikuwa Sh 100 tu kwa kilo moja na hivi sasa bei hiyo ni kati ya Sh 1800 na 2100 kwa mujibu wa taarifa za bodi ya zao hilo.

Kupanda kwa bei hiyo ni matokeo ya uwekezaji wa pamoja baina ya Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) na Serikali, ambayo ilitoa kiasi cha Sh1.4 bilioni kupitia mikopo ya kibenki, hivyo kumwezesha mwekezaji huyo kulipa madeni yote ya wakulima na wanunuzi, huku
akiendelea na ununuzi mpya.

“Mtazamo ulipo sasa ni kuendesha kilimo cha mkataba kati ya kiwanda na mkulima, wakulima
wanashauri kuendelea kujiunga kwenye vikundi na kuuza pareto yao kupitia vyama vyao vya ushirika”, anasema.

Kilimo cha zao la chai Nyoni anasema uzalishaji wa zao hilo linalolimwa zaidi katika wilaya
za Mufindi na Njombe umeanza kupanuliwa wilayani Kilolo baada ya kampuni ya chai Kilolo kuanzishwa.

Kwa upande za zao la kahawa Mkoa una maeneo mengi yafaayo kwa zao hilo, hata hivyo anasema lipo tatizo la wakulima kuwa na maeneo madogo yanayolimwa na vile vile uzalishaji upo chini sana ikilinganishwa na viwango vya kitaalamu.

Anasema maeneo mengi yanazalisha kiasi cha gramu 400 kwa mti, ikilinganishwa na kiasi cha kilo 2.5 hadi 3.0 kwa mti kitaalamu.

“Kuwepo kwa kiwanda cha Kahawa katika mji mdogo wa Makambako kutaongeza ari ya kilimo cha zao hili. Kiwanda kina uwezo wa kukoboa tani 9,600 za kahawa kwa mwaka lakini uzalishaji wa kahawa ni chini ya tani 430 kwa mwaka,” Nyoni anasema.

Dan Associates Limited (DAE Ltd), yenye makao makuu yake mjini Mbinga, ni moja ya kampuni kubwa kabisa za ununuzi wa kahawa hapa nchini. Kampuni imekuwa inanunua kahawa kutoka kwa wakulima tangu 2002.

Mbali na DAE Ltd kujenga kiwanda chake cha kisasa cha kukoboa kahawa chenye uwezo wa kukoboa tani 5 kwa saa huko Mbinga, kampuni hiyo ndiyo inayomiliki maghala kwa ajili ya kuhifadhia kahawa safi kabla ya kuipeleka mnadani na imenunua mashine za kuchanganyia kahawa na za kukokota ambazo zimefungwa kwenye ghala la Makambako.

Kuhusu zao la Pamba Pamba inalimwa wilayani Iringa katika kijiji cha Malengamakali, katika
kipindi cha miaka mitatu iliyopita uzalishaji wake uliathirika kutokana na ukame ulioikumba kata hiyo.

Alizeti mkoani Iringa hulimwa katika maeneo yaliyo na mvua za wastani. Zao hili ni chanzo kikubwa cha mapato kwa wakulima walio katika maeneo ya ukame. Nyoni anasema katika msimu uliopita jumla ya tani 6,347 zilipatikana na kuuzwa ndani na nje ya mkoa na kulifanya zao hilo liwe chanzo kikubwa cha mapato kwa wakulima walio katika maeneo ya ukame.

Ili kuongeza eneo linalotumika kwa kilimo, Nyoni anasema mkoa unaendelea kuandaa mpango
wa matumizi bora ya ardhi kwa kila kijiji, kuhamasisha wawekezaji binafsi kuwekeza katika sekta ya kilimo.

Kuhusu changamoto katika sekta hiyo ya kilimo, Nyoni anazitaja baadhi kuwa ni pamoja na ukosefu wa taarifa za masoko na bei ndogo ya mazao ya wakulima, uhaba wa watumishi wa ugani, miundombinu duni hasa barabara za kwenda vijijini, vyama vya ushirika vinavyosinzia,
bajeti ndogo na baadhi ya mawakala kutokuwa waaminifu.