ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema angependelea mchakato wa Katiba mpya uendelee haraka ili iweze kutumika katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.
Amewataka Watanzania kutambua umuhimu wa suala hilo ili iweze kupatikana haraka kwa lengo la kuepusha vurugu zinazoweza kujitokeza.
“Kama inawezekana ni vyema tukatumia hata muda wa kipindi cha mwaka mmoja ujao ili tuweze kuipata Katiba hiyo, miaka minne ijayo tunatarajia kuingia katika Uchaguzi Mkuu, hivyo kama tutachelewa kuipata inaweza ikaleta hali isiyo ya kawaida,” alisema Pengo.
Alikuwa akizungumza wakati akitoa salamu za Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya wakati
alipozungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
Tayari Muswada wa Marekebisho ya Katiba wa Mwaka 2011 umepitishwa na Bunge lililopita na umeshatiwa saini na Rais Jakaya Kikwete ili kuwa sheria, tayari kuanza mchakato wa
kupata Katiba mpya.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Katiba mpya inatarajiwa kuwa imepatikana mwaka 2014, mwaka mmoja kabla ya Tanzania kuingia katika Uchaguzi Mkuu wa tano tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.
Kumekuwapo na vuguvugu kubwa kuhusu mchakato huo wa Katiba tangu Rais Kikwete alipotangaza kuwa anataka kuwepo na mchakato wa kuandika Katiba mpya na hatimaye
muswada huo ukapelekwa bungeni, ambako mara ya kwanza Aprili mwaka huu, ulipata upinzani mkubwa kwa wabunge.
Serikali ilisikia kilio na maoni ya wabunge na wadau wengine na kwenda kuurekebisha kabla ya kuuwasilisha katika Bunge lililopita Novemba mwaka huu, ambako ulipitishwa Novemba 18, mwaka huu, tayari kumwezesha Rais kuunda Tume ya kukusanya maoni kuhusu mchakato huu wa kuunda Katiba mpya.
Aidha, katika hatua nyingine, Kardinali Pengo amechukizwa na viongozi wanaojifikiria wenyewe kwa kutaka kujiongezea posho, huku wananchi walio chini yao wakiendelea kuandamwa na umasikini.
Kauli yake imekuja wakati umma wa Tanzania ukiwa umekasirishwa na taarifa za wabunge kuongezewa posho kutoka Sh 70,000 hadi Sh 200,000 kwa vikao vyao, hali ambayo imezusha malalamiko makubwa.
Kardinali Pengo alisema, “tabia hiyo haifai kwa taifa letu ambalo linajivunia jubilee ya miaka 50 ya Uhuru uliopatikana kutoka kwa Mwingereza mwaka 1961.”
Alisema inashangaza kuona licha ya mishahara na marupurupu wanayoyapata viongozi hao, bado wanaendelea kung’ang’ania ongezeko la posho badala ya kufikiria namna ya kumwokoa kimaisha mwananchi masikini zaidi aliye chini yao.
“Hivi kama mtu unapata mshahara kama wa mbunge na maslahi mengine anayoyapata katika kazi yake, unawezaje kuona maisha magumu, inapaswa waache kujifikiria wenyewe ili kumuokoa mwananchi wa chini,” alisema Pengo akitoa salamu hizo wakati alipozungumza na vyombo vya habari.
Aidha, amewataka wananchi kuacha kufikiria kuwa maisha ni kubahatisha na badala yake wajitume katika kufanya kazi ili kujikomboa kimasha huku akitolea mfano falsafa ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa Uhuru ni Kazi.
Alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali kutokana na msimamo wake wa kutounga mkono suala la ushoga, aliosema hauna tofauti na uendawazimu kwa kuwa unakwenda kinyume cha maagizo ya Mwenyezi Mungu.
Pia alisema vurugu za vyama vya siasa na maandamano yanayoendelea kutokea nchini, inaonesha kutoelewa vyema mfumo wa vyama vingi kutokana na kuathiriwa na mfumo wa
chama kimoja, suala aliloeleza kuwa linaweza kupata suluhisho pindi Katiba mpya itakapopatikana.
Kuhusu maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu, alisema umefika wakati kwa wanafunzi hao kutafuta namna ya kufikisha madai yao badala ya vurugu zinazisababisha uharibifu wa mali.
Pia aliitaka Serikali kutafakari nini chanzo cha maandamano hayo na kuondoa uonevu palipo na uonevu huku ikitambua kuwa vurugu haziwezi kuzimwa kwa silaha.
“Kama mtoto wa mkulima ananyimwa mkopo huku wa mbunge anapewa mkopo, kwa vyovyote lazima utakuwa unatengeneza mazingira ya kutokea vurugu,” alieleza Pengo.
|
0 Comments