MAPYA yameibuka kwa wakazi wa mabondeni jijini Dar es Salaam waliorudi kwenye maeneo yao licha ya mafuriko makubwa na kunusurika kufa; imebainika wengi wao wanajihusisha na uuzaji wa pombe haramu ya gongo, wanalea vijiwe vya wavuta bangi na dawa za kulevya.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika maeneo ya Jangwani na Mchikichini, katika Bonde la Msimbazi, Dar es Salaam, umebaini kuwa kundi kubwa la vijana wanaotumia dawa za kulevya, bangi wameweka makazi eneo hilo hali kadhalika wauza gongo wengi wanaendesha shughuli zao humo.
Aidha, uchunguzi huo ulioshirikisha uchunguzi mwingine wa habari iliyowahi kuandikwa na gazeti hili wiki kadhaa zilizopita katika maeneo ya Jangwani, umedhihirisha hilo baada ya wahusika kueleza wazi kuwa wanaendesha biashara hizo hivyo wakihama watapoteza wateja.
Mmoja wa waathirika ambaye hakuwa tayari kutaja jina gazetini, alisema mapema wiki hii kuwa, ana kundi kubwa la vijana walioathirika na dawa za kulevya anaowasaidia chakula na malazi na kuuza gongo inayompa kipato hivyo si rahisi kuhama.
“Huku hakuna usumbufu wa polisi wala kamatakamata ya mgambo, vijana wakikimbizwa huko juu na polisi wanakimbilia huku, na maisha yalivyo magumu hivi sasa wengine wanakula unga na tunawahifadhi huku, wana vijiwe vyao maalumu sasa waende wapi? Na pia tuna biashara nyingine ya pombe,” alisema mama huyo.
Alipoulizwa aina ya pombe anayouza, alisita kidogo na kudai, “Nauza pombe za kienyeji za kawaida…hata majirani zangu wengi hapa wanauza….nyie mtaita gongo, wateja wa bia huku hakuna, wengi wanatumia hiyo”.
Katika kuthibitisha hilo, gazeti hili lilifika maeneo hayo mara kadhaa na kukuta vijana wengine wanaofahamika kwa jina la ‘mateja’ walioathirika kwa bangi na dawa za kulevya, wakiweka makazi na vijiwe maeneo hayo ya Jangwani.
Mafuriko makubwa yalilikumba Jiji la Dar es Salaam pamoja na mikoa kadhaa nchini na
kwa Dar es Salaam ilisababisha watu zaidi ya 40 kuripotiwa kufa na wengine zaidi ya 5,000
kukosa makazi baada ya nyumba na mali zao kukumbwa na mafuriko.
Miundombinu kama madaraja na barabara nayo pia iliharibiwa vibaya.
Mkoa wa Dar es Salaam hivi sasa umeandaa viwanja 2,800 katika eneo la ekari 2,000 huko Mabwepande wilayani Kinondoni ambapo tayari viwanja 700 vimekamilika tayari kugawiwa waathirika hao walioko katika makambi mbalimbali yaliyoandaliwa na Serikali baada ya maafa.
Rais Jakaya Kikwete alipowatembelea waathirika hao katika kambi mbalimbali jijini, aliwaambia kwamba maisha wanayoishi ni ya hatari, na kwamba licha ya Serikali kuwasaidia kila kitu katika wakati huu mgumu, lazima wahame katika maeneo hayo ya mabondeni haraka.
Juzi, Mkuu wa Mkoa, Said Mecky Sadiki alirejea agizo hilo la Rais na kueleza kwamba baada ya mwezi mmoja wa kukamilisha kugawa viwanja kwa waathirika hao, Serikali ya Mkoa haitapenda kuona mtu yeyote anakuwepo katika maeneo hayo ya mabondeni, ambayo tayari baadhi yao wamerejea na wanaendesha maisha yao kama kawaida, licha ya tishio la kunyesha kwa mvua zaidi mwishoni mwa wiki hii.
CHANZO CHA HABARI
0 Comments