Shirika la ndege la Zimbabwe linalomilikiwa na serikali limesitisha safari zake nchi jirani ya Afrika Kusini kwa hofu ya ndege zake kuzuiliwa kutokana na madeni linalodaiwa.
Inaripotiwa kuwa shirika hilo linadaiwa $500,000 (£320,000) na msambazaji wake wa ndani wa vipuri na vifaa vya ndege.

Mapema wiki hii ndege ya Air Zimbabwe ilizuiliwa mjini London mpaka deni kama hilo lilipwe.
Shirika hilo inaripotiwa kuwa linahangaika kushughulikia deni lake linafikia jumla ya $140m na inasemekana kuwa linakaribia kufilisika
"Hatusafiri kwenda Afrika Kusini. Tunajaribu kupata fedha za kulipa madeni yetu Afrika Kusini," Innocent Mavhunga, kaimu Afisa Mkuu wa Air Zimbabwe ameliambia gazeti la serikali la Herald.
Amesema, hata hivyo, kuwa shirika hilo litaendelea na safari zake nchini Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Makampuni mengine kama South African Airways la Afrika Kusini na British Airways' Comair,yataendelea kufanya safari zake kati ya mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, na Afrika Kusini.