KATIKA kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadiki ametangaza mkesha utakaoanza leo kuamkia kesho; siku ya kilele katika wilaya zote za mkoa huo.

Kwa mujibu wa Sadiki, mkesha huo utafanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja kwa wakazi wa Wilaya ya Ilala, Kawe kwa wakazi wa Wilaya ya Kinondoni na Mbagala Zakhem kwa wakazi wa wilaya ya Temeke.

Sadiki alitangaza hayo jana alipozungumzia maadhimisho hayo yanayofikia kilele kesho katika Uwanja wa Uhuru ambako mgeni rasmi atakuwa Rais Jakaya Kikwete.

Ili kuruhusu wananchi kushiriki vyema, Sadiki aliwaomba waajiri na wakuu wa taasisi zote za Serikali kuwaruhusu watumishi na waajiriwa wao ili wafike katika uwanja huo na kuungana na Watanzania wote kuhitimisha sherehe hiyo kubwa.

Pia aliwaomba wamiliki wa daladala kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra) kuelekeza mabasi yote Uwanja wa Uhuru ili kufanikisha sherehe hizo kwa kuwawezesha wananchi kufika kwa urahisi.

Mafataki salama
Leo usiku katika mkesha kwa mujibu wa Sadiki, kutakuwepo na vikundi mbalimbali vya burudani na upigaji wa fataki ifikapo saa 6 usiku katika maeneo yote matatu ambako amewataka wakazi wa maeneo hayo kujitokeza kwa wingi.

“Hivyo katika Uwanja wa Uhuru hakutakuwa na mkesha na pia napenda kuwatoa wasiwasi wananchi juu ya milipuko ya fataki kwani hizi huwa ni salama na hazina madhara yoyote kwa wananchi,” alisema Sadiki.

Kilele
Alisema katika siku ya kilele cha maadhimisho hayo, kutakuwa na burudani za aina mbalimbali vikiwemo vikundi vya sanaa, tarumbeta ambapo sherehe itapambwa na vijana wa halaiki na gwaride maalumu la Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

“Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa nchi yetu ni tukio kubwa na la kihistoria, hivyo natoa mwito kwa wakazi wote wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Uhuru ili kushuhudia tukio hilo kubwa na la kihistoria ambalo huenda wengi wetu hatutapata bahati ya kuliona tena,” alisema.

Kwa takriban wiki moja sasa wizara, taasisi na mashirika mbalimbali ya Serikali na kampuni binafsi zilishaanza kufanya maonesho ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru tangu Desemba Mosi katika viwanja vya Mwalimu Nyerere ili kuwaonesha wananchi shughuli mbalimbali wanazozifanya.

JK azindua jengo la Jubilee
Wakati maadhimisho hayo yakiendelea kusubiri kilele, jana Rais Kikwete alizindua jengo jipya la Golden Jubilee Tower lenye mgahawa unaozunguka linalomilikiwa na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF).

Mgahawa wa aina hiyo ni wa kwanza nchini na utatoa fursa kwa wateja kuburudika huku akiangalia mandhari ya pande zote za Jiji la Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi wa PSPF, George Yambesi alisema jengo hilo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru na litatumika kama kitega uchumi na makao makuu ya mfuko huo.

Alisema jengo hilo lina ukubwa wa meta za mraba zipatazo 56,257 likiwa na kumbi mbili za mikutano na migahawa miwili mikubwa ukiwamo unaozunguka na limegharimu kiasi cha Sh bilioni 64.7.

Alisema jengo hilo lina matawi matatu la kwanza lina ghorofa 22 na litatumika kwa ajili ya ofisi za kupangisha, tawi la pili lina ghorofa 13 litatumika kwa ofisi za mfuko wa PSPF na kupangisha.

Yambesi alisema tawi la tatu lenye ghorofa sita litakuwa la maegesho ya magari takribani 300 huku wakitarajia kuingiza mapato ya Sh bilioni 8.27 kwa mwaka wa kwanza na yakizidi kuongezeka kwa kila mwaka.

Alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza rasmi Septemba mwaka 2008 na kukamilika Novemba mwaka huu chini ya wataalamu washauri na makandarasi wa ndani ya nchi.

Akifungua jengo hilo, Rais Kikwete alipongeza mfuko huo kwa kujenga jengo lililozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu na kutaka wengine wanaojenga kuwafikiria wenye ulemavu ili iwe rahisi kwao kutumia majengo hayo.

Pinda akagua Uwanja wa Uhuru
Wakati huo huo, jana Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipata fursa ya kukagua uwanja huo na kukagua maandalizi ya sherehe hizo likiwemo Gwaride Maalumu la Vikosi vya Ulinzi na Usalama na vijana wa halaiki.

Gwaride hilo lilisindikizwa na ndege vita, helikopta za kijeshi, magari yenye mizinga, vifaru na magari yaliyotengenezwa na Shirika la Jeshi la Nyumbu.

Pinda alifika uwanjani hapo saa 4 asubuhi na kukagua maandalizi ya gwaride hilo na hatimae halaiki ya watoto 4,550 kutoka shule mbalimbali nchini walioonesha sura sita ikiwemo ya afya, uchumi na utamaduni.

Baadae alijionea maandamano ya farasi waliofunzwa na Polisi, wakifuatiwa na wananchi waliozaliwa Desemba 9, 1961 wakifuatiwa na maandamano ya baiskeli na pikipiki.

Pia alishuhudia ndege za usafirishaji zikipita angani pamoja na helikopta ambapo pia yalifanyika maonesho ya mbwa waliofunzwa na Polisi na hatimae kuhitimishwa na ngoma za asili kutoka Zanzibar, Mwanza, Pwani na Mtwara.