Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Thomas Laiser akiongoza maelfu ya waombolezaji katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa msanii wa bongo fleva, Abeli Loshilaa Motika maarufu kama Mr. Ebbo (37) aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita na kuzikwa jana nyumbani kwao eneo la Masai Camp, Kata ya Elerai Manispaa ya Arusha.
Na Janeth Mushi, Arusha
NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba Maendeleo na Makazi, Goodluck Ole Medeye, jana ameongoza maelfu ya waombolezaji toka maeneo anuai nchini katika mazishi ya aliyekuwa mwanamuziki maarufu nchini Abel Loshilaa Motika “Mr Ebbo” (37) aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki.
Mr Ebbo aliyefariki dunia baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kansa ya damu kwa muda wa miezi tisa katika hospitali ya Dreams Seminari inayomilikiwa Kanisa Katoliki iliyopo Usa River wilayani Arumeru mkoani hapa.
Aidha katika eneo zima la Masai Camp, nyumbani kwa wazazi wa marehemu kulizizima kwa majonzi na simanzi baada ya mwili wa marehemu kufikishwa nyumbani hapo tayari kwa maziko, toka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Mkoa wa Arusha Mt. Meru.
Awali kuanzia majira ya saa nne asubuhi msafara mkubwa wa magari ulionekana ukitokea katika hospitali hiyo ya Mkoa, msafara uliokuwa ukiongozwa na askari wa Jeshi la Polisi mkoani hapa.
Mwili wa marehemu ulianza kuagwa kuanzia majira ya saa na nusu asubuhi hadi saa saba na nusu mchana, ambapo walilazimika kusitisha zoezi la waombolezaji kutoa heshima za mwisho kutokana na wingi wa watu uliokuwa ukiongezeka.
Viongozi wengine waliokuwepo katika mazishi hayo ni pamoja na Aliyekuwa Mbunge wa Viti maalum na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (mazingira), Dk. Batilda Buriani, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Daniel Ole Njolai, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini Filex Mrema, mbunge wa sasa wa jimbo
hilo Godbless Lema.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, Mkuu wa wilaya ya Arusha, Raymond Mushi, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Akili Mpwapwa pamoja na ‘Mkoloni’ msanii aliyekuwa akishirikiana na Mr Ebbo katika kazi za kisanii. Mr. Ebbo ameacha mjane (Adriana Motika) na watoto watatu. CHANZO CHA HABARI
0 Comments