Staa wa soka la kimataifa wa Rwanda, Hamad Ndikumana ‘Kataut’ amesema kuwa anaondoka Bongo akiwa na mengi ya kujifunza.
Kataut amesema kuwa anakwenda Cyprus, lakini anamuacha nchini, mkewe, Irene Uwoya Ndikumana na mwanaye Krish.
Safari ya Kataut, inakuja baada ya mtifuano wa nguvu uliotokea kati yake na mkewe mpaka kusababisha wakaachana kabla ya kurudiana kutokana na jitihada za wazazi na waandishi wa habari wa Global Publishers.Katika mazungumzo na paparazi wetu juzi, Kataut alisema kuwa hana siku nyingi nchini kabla ya kutimkia Cyprus kwa ajili ya kuendelea na shughuli zake za kusakata kabumbu la kulipwa.
Alisema, safari hiyo haina dalili za kutokuwa na uelewano na mkewe, isipokuwa ni kwa ajili ya kazi.
“Naishi vizuri na mke wangu, isije ikadhaniwa hii safari imetokana na ugomvi na mke wangu,” alisema Kataut kisha akaongeza:
“Tangu tumesuluhishwa na sisi wenyewe tukakubali kumaliza tofauti zetu, tunaishi vizuri sana na mke wangu. Nimeipenda sana Tanzania, ni nchi nzuri. Nawashukuru Watanzania kwa ukarimu wao.
“Kuhusu kuondoka kwangu, unajua nilikaa muda mrefu hapa kwa sababu ya matatizo ya mtoto. Mke wangu alinilalamikia mtoto alikuwa analia sana usiku, kwa hiyo alishindwa kumlea peke yake.
“Kwa umri wake, haikuwa rahisi kumchukua ili tuwe wote Cyprus. Ikabidi nikatishe mkataba na timu yangu ili nije kushiriki kumlea. Sasa hivi hali ni shwari ndiyo maana naenda Cyprus kuendelea na kazi zangu.”
Alipoulizwa kama anaenda na mkewe pamoja na mwanaye, Kataut alijibu: “Mke wangu na mtoto wanabaki. Hakuna shida, baadaye watakuja mambo yakikaa sawa.”
Wiki mbili zilizopita, Kataut alisema kuwa Uwoya na Krish, ilishindikana kuungana naye Cyprus kwa sababu mtoto alikuwa hajatimiza umri wa miezi mitatu ambao ndiyo huruhusiwa kisheria kumkatia ‘pasipoti’ na kusafiri angani.Hivi sasa, mtoto anaelekea kutimiza miezi saba, hivyo hakuna kizuizi cha kusafiri naye kwenda Cyprus kama ilivyokuwa hapo kabla.
Hata hivyo, Kataut hakutaka kuzungumza sababu ya kumuacha Uwoya na mtoto, badala yake alisisitiza kwamba anakwenda Cyuprus kwa sababu za kikazi.
“Nakwenda kwa ajili ya kazi, mke wangu na mtoto wataungana na mimi wakati mwingine,” alisema.
Kwa upande wa Uwoya, alisema kuwa maisha yake na mumewe ni raha tupu tangu walipomaliza tofauti zao.
Alisema, mume wake anasafiri kwa sababu za kikazi na kwamba haimaanishi kuwa wamegombana.
“Kama ni mambo ya ugomvi yaliisha. Tena kwa kipindi hiki sitaki kuongea sana, muulizeni Hamad (Kataut) anaweza kuwaambia ni jinsi gani tunavyoelewana ndani ya nyumba,” alisema Uwoya.
Pamoja na yote hayo, si Uwoya wala Kataut aliyesema siku rasmi ya mwanasoka huyo kutimka, isipokuwa walisisitiza kwamba isingezidi siku mbili kuanzia juzi (Alhamisi).
Klabu ya mwisho Kataut kuichezea ni APOP Kinyras Peyias ambayo alivunja nayo mkataba mwaka huu, hivyo anarudi Cyprus kusaka timu mpya ya kuichezea.