Alipokuwa akiingia uwanja wa Taifa rais Kikwete kila mmoja alisimama na ilikuwa ni kelele za furaha uwanjani hapo.
Yani usije ukathubutu kuota ndoto ya kupigana na wanajeshi wa Tanzania mmmh nakuonea hurumaa.
Rais alipita kukagua gwaride za vikosi mbalimbali uwanjani hapo.

MAMBO YALIYOJIRI UWANJANI
SHEREHE za kilele cha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara zimeadhimishwa kwa burudani za aina yake na kukonga nyoyo za maelfu ya watu waliozihudhuria katika uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kiasi cha kumfanya Rais Jakaya Kiwete atamke hadharani kuwa haijawahi kutokea.

Idadi kubwa ya wananchi wa ndani na nje walianza kuingia katika uwanja huo alfajiri ya saa 12:00 wakati mabalozi,viongozi wa dini, vyama vya siasa, wabunge na wageni waalikwa kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania waliingia kwa utaratibu maalum, kabla ya viongozi wastaafu na wapya wa Tanzania kuingia kwautaratibu huo.

Katika safu ya viongozi wa kitaifa, Rais ndiye aliyekuwa wa mwisho kuingia uwanjani hapo akiwa katika gari la wazi, huku akishangiliwa na wananchi aliokuwa akiwapungia mkono kuwasalimia.

Akiwa katika jukwaa maalum, Rais alipokea kiapo cha utii kwa kupigiwa mizinga 21 kabla ya kukagua gwaride la miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara, lilliochangia kupendezesha sherehe hizo kwa kiasi kikubwa.

Mbali ya mizingi hiyo, ilipigwa mingine mitano iliyoashiria miaka 50 ya uhuru, kwa kila mmoja kusimama badala ya muongo mmoja, yaani miaka 10 ya uhuru.

Mizinga hiyo ilienda sambamba na wimbo “Tanzania nakupenda kwa moyo wote…”.
Kama ilivyo ada, gwaride lililojumuisha vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama nchini lilipita mbele ya jukwaa kuu alipokuwa Rais na kutoa heshima kwa mwendo wa pole na haraka.

Hata hivyo, ukimya wa nidhamu uliokuwa umetawala wakati shughuli hizo za kiitifaki zikiendelea ulibadilika kuwa vicheko vya furaha, kelele za shangwe na tabasamu
zisizokwisha baada ya wanajeshi wa Tanzania kuuonyesha umma sehemu ndogo ya silaha za kivita zilizopo nchini, kwa mtindo uliojaa mbwembwe zilizoonyesha uwezo na kujiamini kwao katika masuala ya ulinzi na usalama.

“Wajaribuni muone”, hayo ndiyo maneno yaliyokuwa yakisemwa na baadhi ya watu waliokuwa wamejaa katika uwanja huo wakiwatazama, kumaanisha kuwa walinzi hao wa
usalama wapo ‘fiti’ katika shughuli hiyo.




Ndege sita za kivita ziliruka angani kwa staili tofauti zikiwemo mbili zilizotumia mtindo wa kujiviringisha, kama ishara ya heshima kwa Rais.

Wakati wote huo, kelele za shangwe zilisikika kutoka kwa umati uliokuwepo uwanjani hapo na
zilizidi baada ya mtangazaji aliyekuwa akitoa maelezo uwanjani hapo kuueleza umma huo kuwa moja ya ndege hizo mbili ilikuwa inarushwa na mwanajeshi mwanamke.

Kadhalika, watanzania walifurahia kuonyeshwa magari ya jeshi yaliyotengenezwa nchini na wanajeshi wa Tanzania wanaounda kikosi kinachoitwa Nyumbu. Nderemo, vifijo na hoi hoi
vilichukua sura mpya baada ya halaiki ya watoto wa shule za msingi watoto wa shule za msingi wapatao 4,550 walionesha uwezo wao katika halaiki ambayo ilionesha taswira ya mambo mbalimbali yaliyofanyika katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru.

Kwanza watoto hao walianza kwa kuonesha masuala yanayohusu ulinzi, kabla ya kuhamia katika afya wakionesha ongezeko la zahanati na hospitali, masuala ya mazingira na baadaye masuala ya uchumi kama vile kilimo na uvuvi.

Sura ya mwisho iliyooneshwa na vijana hao ni ile ya utamaduni wakirejea kauli ya Mwalimu Nyerere kuwa ‘Taifa lisilo na utamduni ni Taifa mfu’ kwa kuonesha umahiri katika ngoma za makabila mbalimbali na sarakasi.

Palikuwepo pia na burudani za ngoma za asili kutoka mikoa ya Mwanza, Mtwara, Pemba Kaskazini, Pwani, Mbeya na wimbo maalumu wa injili ulioimbwa na baadhi ya wasanii wa muziki wa Injili hapa nchini.

Viongozi wa serikali, mataifa, nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa pia walinogesha sherehe hizo kutokana na kuwa kivutio.

Viongozi kama Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili Balozi Seif Idd, Spika Anne Makinda na viongozi wa
vyama vya siasa walikuwepo.

Marais waliokuwepo uwanjani hapo ni Rais Hifikepunye Pohamba wa Namibia, Rais Armando Guebuza wa Msumbiji, Rais Bingu wa Mutharika (Malawi), Rais Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania na Rais wa Comoro, Ikhililou Dhoinine na mkewe Hadidja Ikililou.

Katika sherehe hizo, Kenya iliwakililishwa na Makamu wa Rais, Kalonzo Musyoka. Pia Rais mstaafu wa Comoro Abdallah Sambi, Waziri Mkuu wa Rwanda Pierre Habumuremyi
na Waziri Mkuu wa Lesotho Paralitha Mosisili walihudhuria.

Viongozi wa kitaifa hawakuwa nyuma katika kuadhimisha miaka hiyo 50 ya Uhuru kwani Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassani Mwinyi, Awamu ya Tatu, Benjamini William Mkapa,
Viongozi waadilifu wapewa nishani Katika kusherehekea Miaka 50 ya Uhuru, Rais Jakaya Kikwete jana amewatunukia marais wastaafu, mawaziri wakuu wastaafu, wakuu wa majeshi wastaafu na wananchi mbalimbali nishani ya mchango wao katika kupata uhuru na kulitumikia
Taifa kwa uadilifu mkubwa.

Tuzo hizo zilizotolewa kwenye Viwanja vya Ikulu, ni nishani ya Julius Kambarage Nyerere, liyokwenda kwake kutokana na kushika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini na kulitumikia Taifa kwa uadilifu ikiwa ni pamoja na kuwa muasisi wa Taifa, kiongozi wa mapambano ya kupigania Uhuru na Rais wa Kwanza wa Tanganyika na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Kikwete pia alimtunukia nishani hiyo Rais wa Awamu wa Pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye
pamoja na fani yake ya ualimu, amewahi kuwa Balozi, kushika nyadhifa mbalimbali katika wizara mbalimbali na hata alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa mfano wa
uwajibikaji baada ya kujiuzulu kwa kutokea vifo vya mahabusu mkoani Shinyanga, na pia kuiongoza nchi kwa uadilifu.

Nishani ya tatu ilikwenda kwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye pamoja na kuwa Balozi , kushika nyadhifa katika wizara mbalimbali, lakini akiwa Rais aliweza kuinua uchumi wa nchi na ukusanyaji kodi na kuliongoza Taifa kwa uadilifu wakati wa majanga makubwa kama yale ya ajali ya mv. Bukoba, ajali ya treni ya TRC, mafuriko ya Elininyo na kifo
cha Baba wa Taifa, Nyerere.

Waliopewa tuzo za Mwenge wa Uhuru daraja la Pili ni Dk. Ali Mohamedi Shein, hayati Sheikh Abeid Amaan Karume, hayati Rashid Mfaume Kawawa, Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba, hayati Idrisa Abdul Wakili, Dk. Salim Ahmed Salim, Frederick Sumaye, hayati Dk. Omary Ali Juma, na hayati Edward Moringe Sokoine.

Waliopewa nishani ya Uhuru daraja la nne kwa watendaji wa Serikali, Bunge na Jeshi ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema, Mkuu wa Magereza Agustino Nanyaro na Spika wa Bunge Anne Makinda.

Wengine ni Spika mstaafu Pius Msekwa, Jaji Mark Bomani, Jenerali mstaafu Mrisho Sarakikya, hayati Jenerali Abdalah Twalipo, Jenerali mstaafu David Musuguri, Jenerali mstaafu Ernest Mwita Kyaro, marehemu Luteni Kanal Alexander Nyirenda, Inspekta Jenerali Msangi Shaidi, Kamishna wa Magereza mstaafu Obedia Rugimbana, Dk .Wilbert Chabula na mwanamke wa
kwanza kusoma sheria Jaji Julie Manning.

Nishani ya Mwenge wa Uhuru daraja la nne kwa wananchi waliosaidia mchango wa upatikanaji wa Uhuru ni Omary Suleimani, Aisha Kanduru, Maria Nyerere, marehemu Sofia Kawawa , marehemu John Rupia, marehemu Abdul Sykes, Ally Sykes, Kingunge Ngombare- Mwiru, Job Lusinde, Balozi George Kahama, Constatine Milinga, Brigedia Jenerali mtaafu Hashim Mbita,
marehemu Rajabu Diwani, Kapteni Tony Makinda, marehemu Mendanusi Pacha na marehemu Buku Mussa.

Wengine ni Mama Mpera, Mosi Tambwe, Sued Kagasheki, marehemu Zaituni Matola, Merry Mkoko, marehemu Fatna Mwashambwa , Salum Bakari, Alhaji Mustafa Songambele, Andrew Mateso Ndimbo, Mwanabibi Forodhani, Rashid Liganga, Mustafa Mwangwenyuka na Omary Suleimani.