ASAMEHE WAFUNGWA 3000, WABAKAJI WAENDELEA KUSOTA
VIONGOZI mbalimbali wa ndani na nje ya nchi jana, waliungana na Watanzania kusherehekea kumbukumbu ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania bara kwenye tukio la kihistoria lililofanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.Sherehe hizo zilihudhuriwa na marais kutoka nchi mbalimbali, mawaziri wakuu, mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na viongozi mbalimbali wa dini na vyama vya siasa.
Uwanja wa Uhuru ulielemewa na idadi kubwa ya watu walioanza kumiminika kuanzia saa 11.00 alfajiri, hali iliyosababisha mamlaka zilizoandaa sherehe hizo, kuwahamishia baadhi yao katika Uwanja mpya wa Taifa
Kikwete asisitiza mshikamano
Katika hotuba yake fupi aliyoanza kuitoa kuanzia saa 7:40 hadi 8:00 mchana, Rais Kikwete alisisitiza mshikamano kwa Watanzania na kueleza kuwa wana kila sababu ya kusherehekea Miaka 50 ya Uhuru kutokanana mafanikio yaliyopatikana.

“Haya ndio matunda ya TANU na ASP chini ya viongozi uongozi wa Mwalimu Nyerere na Karume, tangu mwaka 1961 tumeweza kupambana na maadui watatu, ujinga, umasikini na maradhi” alisema Kikwete.
Alisema wakati Tanganyika ikipata uhuru wake kulikuwa na barabara tatu tu za lami ambazo ni barabara ya Dar es Salaam-Morogoro, Tanga-Korogwe na Moshi-Arusha, lakini hivi sasa barabara za lami zipo kwa kiwango kikubwa.
Rais ambaye alitumia muda wake kuelezea mafanikio, aliwataka Watanzania kutovunjika moyo na kwamba licha ya mafanikio yaliyopatikana tangu uhuru bado kuna changamoto nyingi.
“Wakoloni walituachia misingi dhaifu hivyo safari yetu bado ni ndefu, sherehe hizi za uhuru ni zetu wote na huwezi kuzungumzia uhuru wa Tanganyika bila kumtaja Mwalimu Nyerere na wenzake,” alisema Kikwete
Kikwete awasili Uwanjani
Rais Jakaya Kikwete alifika uwanjani hapo saa 4:17 asubuhi akiwa katika gari la wazi pamoja na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange.

Baada ya kuwasili, Rais Kikwete alikagua gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama na baadaye alipigiwa mizinga 26, ambayo 21 ni kwa ajili ya Rais na mitano ni maalumu kwa ajili ya Miaka 50 ya Uhuru.
Kufuatia kupigwa kwa mizinga hiyo, baadhi ya watu walionekana kupoteza fahamu na kusababisha kutoweka utulivu uwanjani hapo. Gazeti hili lilishuhudia wahudumu wa Kikosi cha Msalaba Mwekundu wakihangaika kubeba watu waliokuwa wakianguka na kupoteza fahamu wakati mizinga hiyo ikipigwa. Walioonekana kukumbwa zaidi na mshtuko wa milio mikali ya mizinga hiyo ni wanafunzi.
Pia, askari mgambo wanne na polisi mmoja waliokuwa katika vikosi vilivyokaguliwa na Rais nao walianguka na kutolewa na wahudumu wa msalaba mwekundu.

Tofauti na ilivyozoeleka katika sherehe za kumbukumbu ya Uhuru wa Tanganyika, safari hii licha ya vikosi hivyo kufanya gwaride la heshima kwa Rais, pia vilifanya maonyesho ya zana mbalimbali za kivita ikiwa ni pamoja na vifaru, mabomu, magari ya deraya, ndege za kivita na makombora ya kutungulia ndege.
Kivutio kikubwa kwa wananchi waliofurika katika uwanja huo ni jinsi vifaru vya kivita vilivyokuwa vikiendeshwa kwa ustadi pamoja na ndege za kivita tano, zilizokuwa zikipita angani kwa mtindo wa aina yake.
Kivutio kingine kilikuwa halaiki iliyochezwa na watoto 4,550 kutoka shule mbalimbali za msingi kwa kujipanga uwanjani na kuonyesha ishara na alama mbalimbali za mafanikio ya Tanzania katika nyanja za kiuchumi, kilimo, elimu, utamaduni na afya.
Watoto hao waliokuwa wamevalia sare za rangi mbalimbali walitoa burudani ya aina yake na kuwafanya wananchi waliohudhuria sherehe hizo kuwashangilia na kutojali jua kali lililokuwa likiwaka uwanjani hapo. Mbali na watoto hao, pia kulikuwa na burudani mbalimbali za ngoma kutoka mikoa ya Mbeya, Pwani, Mwanza na Mtwara.

Viongozi waliokuwepo
Baadhi ya viongozi waliokuwepo katika sherehe hizo ni pamoja na Mawaziri Wakuu wastaafu, Dk Salim Ahmed Salim, Joseph Warioba, Fredereck Sumaye na Edward Lowassa.
Wengine ni Mama Maria Nyerere, Spika wa Bunge Anne Makinda, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri Mkuu wa Uganda, Amama Mbabazi, Waziri Mkuu wa Rwanda, Pierre Damien Habumuremyi, Waziri Mkuu wa Lesotho, Pakalitha Mosisili.


Pia walikuwepo Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk Gharib Bilal, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ Balozi Seif Iddi na mwenzake wa kwanza Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo
Wengine ni wenyeviti wa Chadema, Freeman Mbowe, Augustino Mrema wa TLP, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume na Waziri Mkuu wa Rwanda, Bernard Makuza.
Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Rais wa Comoro, Dk Ikililou Dhoinine, Rais wa Msumbiji, Armando Guebuza, Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika, Rais wa Mauritania, Muhammad Ould Abdul Aziz, Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba na Rais wa Bunge la Korea, Kim Jong Nam.
Mbowe aiponda Serikali
Kwa upande wake, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe, alisema maandalizi ya sherehe hizo ni makubwa na kwamba fedha zilizotumika katika sherehe hizo zingeweza kufanyia kitu kingine cha msingi.
“Walioona umuhimu wa kufanya shughuli hii ni serikali ya CCM sio wananchi…, hata kama kuna nchi zinaadhimisha miaka kadhaa ya uhuru wao hatutakiwi kujilinganisha nazo,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema ni jambo la kushangaza katika maadhimisho hayo viongozi wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki wameshindwa kuhudhuria wakati Tanzania ipo katika mchakato wa kuingia katika Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki.
“Hii ni ajabu pengine serikali inaweza kulijibu hili…, sijawaona viongozi wakuu wa serikali ya Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Afrika Kusini, Zimbabwe na Zambia,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema kuwa licha ya kuwa kuna mambo ya kujivunia ndani ya miaka 50 ya uhuru, lakini inasikitisha kuona serikali ikipima maendeleo ya elimu kwa idadi ya wingi wa wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu.
Mkesha
Usiku wa kuamkia jana ulifanyika mkesha wa sherehe hizo katika viwanja vya mnazi mmoja na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo, Dk Bilal na Waziri Mkuu Pinda.

Mamia ya watu wa kada mbalimbali walianza kufika katika viwanja hivyo kuanzia saa 1 usiku na kupata burudani iliyokuwa ikitolewa na vikundi mbalimbali.
Akizungumza katika mkesha huo, Dk Bilal aliwataka Watanzania kudumisha amani hata kama wana tofauti za kiitikadi.
Leon Bahati anaripoti kuwa, Rais Jakaya Kikwete jana amewatunuku nishati watu 57 waliolitumikia taifa kwa uadilifu na kutoa mchango katika shughuli mbalimbali za serikali.
Shughuli hiyo ilifanyika Ikulu jana jioni katika maadhimisho ya kilele cha sherehe za Uhuru.Waliopewa nishani hizo ni wale waliolitumikia taifa kwa uadilifu bila kuwa na kashfa yoyote.

Miongoni mwa nishani zilizotolewa ni za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mwenge wa Uhuru daraja la pili na la nne.
Miongoni mwa watu waliopewa nishani ya Mwalimu Nyerere ni marais watatu, awamu ya kwanza Mwalimu Nyerere, ya pili Ali Hassan Mwinyi na ya tatu, Benjamin Mkapa.

Nishani ya Uhuru daraja la pili ilitolewa kwa watu waliokwisha alitumikia taifa katika nafasi za makamu wa rais na waziri mkuu.
Waliopewa nishani hizo ni pamoja na Marehemu Rashid Kawawa, Idrisa Abdul Wakil, Omary Ali Juma, Dk Mohamed Shein, Cleopa Msuya, Joseph Warioba, Marehemu Edward Sokoine, Dk Salim Ahmed Salim na Frederick Sumaye.
Waliopewa nishati ya mwenge wa uhuru daraja la nne ni pamoja na Spika wa Bunge Anne Makinda na Spika wa Bunge mstaafu Pius Msekwa.

Rais asamehe wafungwa
Katika hatua nyingine, Rais ametoa msamaha kwa wafungwa 3,803 katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara huku wafungwa wa dawa za kulevya, rushwa, wizi, kubaka na kulawiti wakikosa msamaha huo. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, ilisema msamaha huo utawahusu wafungwa wenye sifa mbalimbali.

Taarifa hiyo iliwataja wafungwa walionufaika na msamaha huo ni pamoja na wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi, ambao umri huo ni lazima uthibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya.
Wengine ni wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili na ulemavu huo ni lazima nao uthibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya.
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba, wengine ambao ni wafungwa wenye magonjwa kama Ukimwi, Kifua Kikuu na Kansa ambao wako kwenye hatua ya mwisho ya ugonjwa ambao watathibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya.
Ilitaja wafungwa wengine ambao ni wa kike walioingia na mimba gerezani na walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonyesha ambao wote watanufaika na msamaha huo.
Kundi la mwisho la wafungwa wanaohusika na msamaha huo ni wafungwa wanaotumikia kifungo kisichozidi miaka 5, ambao hadi siku ya msamaha (jana) walikuwa wametumikia robo ya vifungo vyao.
Taarifa hiyo ilisema ni mategemeo ya serikali kwamba wafungwa waliopata msamaha huo watarejea katika jamii na kushirikia na wenzao katika ujenzi wa taifa na kuwaasa wajiepushe na kutenda makosa ili wasirejee gerezani.
Rais ametoa msamaha huo kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45 kifungu cha kwanza (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wazanzibar walia kutelekezwa
Hamisi Mwesi na Ibrahim Yamola wanaripoti kuwa, wakati wengine wakifurahia, Wazanzibar zaidi ya 300 ambao walitakiwa kuhudhuria maadhimisho hayo walishindwa kushiriki na kuamua kuondoka kutokana na uwanja kufurika .

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana jijini Dar es Salaam katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mgulani walikofikia, Wazanzibar hao walisema, toka wafike wamekuwa hawapati ushirikiano toka uongozi wa Serikali ya Tanzania bara zaidi ya kuwapelekea chakula tu.
“Tumefika hapa jana mchana lakini hakuna mapokezi mazuri ambayo tumeyapata na kutufanya kuishi katika mazingira magumu kana kwamba hatuna kwetu, kweli wametutesa sana,” alisema Mzee mmoja ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake.
Mzee huyo aliongeza kwamba, waliamka asubuhi na kujiandaa kwenda katika sherehe hizo lakini cha kusikitisha baada ya kufika uwanjani, waliambiwa nafasi zimejaa na kutakiwa kwenda mlango namba tatu ambako nako waliambiwa ndiko nafasi zao zilikokuwa lakini nako waliambiwa kumejaa hivyo kuamua kuondoka.
“Kwa kuwa wametuleta hapa kuja kutudhalilisha hivi, ilitubidi tuondoke tu ili tusije kuwaharibia sherehe yao lakini kweli hatujapenda hata kidogo kwa kutufanya kama watoto wa mitaani kutuzungusha huku na huko,” kilisema chanzo chetu ambacho nacho kiliomba hifadhi ya jina lake.
“Tunalazwa chini, tunatandika mikeka sasa upepo unapo vuma tunalowa mchanga yaani hata kutuandalia magodoro wameshindwa kweli wametudhalilisha na kwa upande wangu sitorudia tena kuja kwani hii ni mara ya nne nakuja lakini hali ya malazi inakuwa hairidhishi hata kidogo,” Alilalamika mwananchi huyo.
Mkuu wa Mkoa
Alipotafutwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecky Sadiki kutolea ufafanuzi tuhuma hizo za kuwatelekeza na kuwaweka katika mazingira magumu wageni hao, alisema, yeye sio msemaji wala hahusiki na lolote kuhusu sherehe hizo.
“Mimi sio mhusika wa aina yoyote wa maadhimisho haya wewe watafute waandaaji wa shughuli hii watakueleza,” alisema Sadiki

Rais Jakaya Kikwete akikagua gwaride la heshima wakati wa sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru zilizofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana.