Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wametapika nyongo na kuieleza Serikali wanapinga vikali nyongeza ya posho ya vikao kwa wabunge kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 200,000 kwa siku, pamoja na kuigeuza hospitali hiyo kuwa kituo cha kusafirishia vigogo kwa ajili ya kwenda nje ya nchi kutibiwa.
Madaktari hao ambao waliungana na wafanyakazi wengine wa hospitali hiyo, walisema hayo jana mbele ya Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya, ambapo walisema wao kama Madaktari Bingwa wanaona vitendo hivyo ni udhalilishaji mkubwa wanaofanyiwa na serikali.
Dk. Nkya alikuwa na ziara ya kutembelea hospitali hiyo na kuzungumza na wafanyakazi wakati akitekeleza ratiba yake ya kutembelea hospitali mbalimbali jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuangalia utendaji wa kazi.
Akizungumza kwa niaba yao, Dk. Prim Saidia, alisema kwa ujumla wafanyakazi wa hospitali hiyo hasa Madaktari Bingwa hawakubaliani na hatua ya kuwarundikia posho wabunge, huku wao wakiendelea kutaabika.
Alisema kitu cha kusikitisha ni kwamba daktari ambaye amesoma na kupata shahada zaidi ya mbili anaendelea kupata posho ya Sh. 10,000 wakati katika ustawi wa nchi ndiye mtu muhimu na anayepaswa kuangaliwa kwa makini.
“Mheshimiwa Waziri, leo tutakwambia ukweli, sisi madaktari tumechoshwa na hali hii, kama hali ngumu ya uchumi ni wote na hakuna kundi la watu. Haiwezekani Daktari Bingwa analipwa posho shilingi elfu kumi eti wabunge wameongezewa maradufu,” alisema Dk. Saidia.
Aliongeza kuwa kitendo cha kuwapa wabunge Sh. 200,000 huku madaktari na wafanyakazi wa hospitali wanalipwa kiasi kidogo na wengine hawalipwi kitu, ni kitendo cha kuwadharau.
Alieleza kwa ujumla madaktari wanaofanya kazi kwenye hospitali hiyo wanafanya kazi kwa ukwasi mkubwa kwani wengi wao wanashindwa hata kufika hospitalini hapo kutokana na kukosa pesa ya usafiri.
“Hapa Muhimbili hatuna posho ya usafiri wala ile ya nyumba, daktari akihitajiwa inambidi atumie usafiri wake ili afike hapa, lakini Serikali haimjali na kuona wabunge ni bora zaidi ya wengine, huu ni udhalilishaji mkubwa,” aliongeza Dk. Saidia.
Dk. Saidia alieleza kuwa kitu kingine wanachokipinga ni kitendo cha Serikali kutumia hospitali hiyo kubwa nchini kuwa kituo cha kuwapumzisha viongozi wanaopata matatizo ya kiafya kabla ya kuwapeleka nchini India kupatiwa matibabu.
Alisema hakuna maana kwa Serikali kuendelea kutumia pesa nyingi kwa ajili ya kuwasomesha wataalamu wa tiba ikiwa haiwaamini na badala yake inawapeleka nje viongozi kutibiwa hata kama magonjwa yao yangeweza kutibiwa nchini.
Alieleza jambo hilo linawasikitisha kwa kiasi kikubwa na kwamba viongozi wengi sasa wanaona hospitali hiyo ni kama sehemu ya kufanyiwa uchunguzi wa awali tu, kisha matibabu yote yanafanyika India, kitu ambacho alisema kinakatisha tamaa.
“Serikali inawasomesha wataalamu wengi nje ya nchi, wengi tumesoma ili kuwatumikia wananchi, sasa kama viongozi wetu hawatuthamini wanatudharau na kuona hatufai kuwatibu kuna maana gani ya kutusomesha?” alihoji huku akishangiliwa na wafanyakazi wenzake.
Aliendelea: “Tunachotaka wao wawe watu wa mfano kwa kupenda kutibiwa hapa hapa Muhimbili, uwezo tunao wa kutoa tiba.”
Mfanyakazi mwingine, Amisita Lungu, alisema wakati umefika kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuangalia utaratibu wa kuwaruhusu wafanyakazi hao kutafuta mfuko wa hifadhi ya jamii wenye mafao mazuri kutokana wengi wao waliostafu kuwa masikini kutokana na kupata mafao madogo.
Alisema wakati wanafanyakazi kwenye mazingira magumu, wanatarajia wanapomaliza muda wao wa ajira kuwa na maisha mazuri, lakini ndoto hiyo imeyeyuka baada ya uongozi wa hospitali kushindwa kufanyia kazi.
Aidha, kitu kingine ambacho wafanyakazi hao wamelalamikia ni tofauti za mishahara kwa baadhi ya wafanyakazi ambao wanafanya kazi ya aina moja pamoja na kupewa huduma duni ya Bima ya Afya ambayo walieleza kuwa hailingani na michango wanayotoa.
NAIBU WAZIRI: NIMEWASIKIA
Hata hivyo, wakati akijibu hoja hizo, Dk. Nkya alionekana kuwa na tahadhari kubwa. Hoja kuhusu posho za wabunge haikuigusia, badala yake alisema kuna baadhi ya malalamiko atayapeleka ngazi za juu ili wayafanyie kazi.
“Nimewasikia ndugu zangu wafanyakazi, kuna baadhi ya mambo itabidi niyapeleke kwa wakubwa zangu na mengine nitayajibu hapa,” alisema Dk. Nkya.
Dk. Nya aliwaeleza wafanyakazi hao kwamba atahakikisha anafuatilia kwa makini juu ya posho wanazostahili kupewa madaktari lakini hawapewi, ili angalau kuwafanya wamudu kasi ya kupanda kwa gharama za maisha.
Alisema japokuwa tatizo la posho kwa madaktari ni changamoto kubwa inayoikabili serikali, kwa kushirikiana na wenzake wataweza kulitatua japo sio kwa haraka kama wanavyotaka wafanyakazi hao.
“Nimewasikia kile mnachosema, lakini mimi sio mwamuzi, nitapeleka yote kwa Waziri au kwa Waziri Mkuu atafute ufumbuzi, haya yote mlioniambia,” alisema Dk. Nkya.
Dk. Nkya aliwataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa kujituma wakati Serikali inaendelea kutatua matatizo yao kwa awamu kulingana na uwezo wake wa kifedha.