JUMUIYA ya Ulaya (EU) imetoa Sh bilioni 97 (sawa na Euro milioni 48) kuwezesha Bajeti ya Serikali katika mwaka wa fedha 2011/12 chini ya Msaada wa Pamoja kwa Bajeti ya Serikali (GBS).
Msaada huo umeelekezwa kuisaidia Tanzania katika Mpango wa Kupunguza Umasikini kupitia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs).
Taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na Jumuiya ya Ulaya, imeeleza kwamba pia EU imeieleza Serikali kuridhishwa na hitimisho la mapitio ya ripoti ya mwaka ya GBS na kuahidi kuwa itaendelea kuisaidia Tanzania katika bajeti zijazo katika mwaka 2012 na 2013.
Washirika wa Maendeleo wa Tanzania wapatao 12 ikiwemo Jumuiya ya Ulaya ambayo ni mwenyekiti wa washirika hao, walijizatiti kuchangia Dola za Marekani milioni 453 kuisaidia Bajeti ya Serikali kwa 2011/12.
EU imekuwa ikisaidia Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (Mkukuta) na kwa kushirikiana na washirika na wahisani wengine kupitia Mpango wa Pamoja wa Kuisaidia Tanzania.
Lengo kuu ni kuwezesha Serikali kutekeleza programu ya kupunguza umasikini hasa kupitia kuwezesha bajeti, ujenzi wa barabara, maji, sheria na mabadiliko yake, afya na elimu.
Awamu ya sasa iliyoanza 2008 hadi 2013 imeainisha kiasi cha Euro milioni 555 kwa Tanzania na sehemu ya fedha hizo (Euro milioni 305) zimetolewa kusaidia bajeti ya serikali katika mpango wa kupunguza umasikini.
Euro milioni 139 zimeelekezwa katika bajeti za kisekta ambazo ni katika barabara (Euro milioni 55.5), biashara na maendeleo ya kikanda.
0 Comments