USHAHIDI wa watoto mahakamani kuhusu ugomvi wa baba na mama, umesababisha Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kumhukumu baba wa watoto hao, Julius Mwakalonge (55) kwenda jela miaka saba.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mfawidhi Joyce Minde alisema amefikia uamuzi huo baada
ya kuridhika na vielelezo pamoja na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi wanne wa upande wa mashitaka wakiwemo watoto wake wawili (majina yamehifadhiwa).
Katika ushahidi huo, mtoto wa Mwakalonge alidai kuwa mama yake, Niendewe Safiel alipigwa
huku akishuhudia, na baba yake alimwambia asifuatilie kilichotokea badala yake aende shule.
Mtoto huyo alidai kuwa baada ya kipigo hicho kwa mama yake, baba yake alimuita dada yake ili ampeleke mama yao hospitali.
Naye Mwendesha Mashitaka Mkuu, Naima Mwanga, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa
mshitakiwa kwa kuwa maazimio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yanasisitiza juu ya haki za
binadamu na kupinga unyanyasaji wa kijinsia.
Naima alidai kuwa Juni 2, 2005 saa moja jioni katika eneo la Mazizini, Mwakalonge alimjeruhi
mkewe kwa kumpiga na kumvunja mguu wake wa kulia, jambo lililomsababishia maumivu na majeraha.
Alidai kuwa chanzo cha ugomvi huo ni ugomvi wa kifamilia na unyanyasaji ambapo Mwakalonge alimpiga na kumjeruhi mkewe mbele ya watoto wake.
Mwakalonge alipopewa nafasi ya kujitetea, aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa
familia inamtegemea na anasumbuliwa na maradhi ambayo kama atafungwa, maisha yake yataishia jela.
“Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa hasa na watoto wa mshitakiwa. Aidha, mahakama inamuaru mlalamikaji afungue kesi ya kudai fidia,” alisema hakimu Minde na kuongeza: “Kwa kuzingatia utetezi wa mshitakiwa hasa kutegemewa na watoto, mahakama imempunguzia adhabu na inamhukumu kifungo cha miaka minne jela badala ya miaka saba kama sheria inavyosema.”
Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mlalamikaji Niendewe alitoka nje ya mahakama huku akisema “Haleluya”.
Adai kutaka kulawitiwa na polisi
Katika kesi nyingine, Abby Nkungu anaripoti kuwa katika Mahakama ya Mwanzo Utemini mjini Singida, mshitakiwa Ayub Yusufu (26) alidai kuwa alitishiwa kulawitiwa na askari wapatao sita ili akiri kumshambulia askari wa usalama barabarani, Abihud Kasonde.
Mshitakiwa huyo alidai mbele ya Hakimu Ferdinand Njau kuwa alitiwa mbaroni na Polisi
Ijumaa iliyopita akiwa mahakamani hapo akisubiri kumdhamini mwenzake mmoja na kisha kuunganishwa katika kesi hiyo.
Alidai kuwa alifika mahakamani ili kumwekea dhamana mmoja wa wafanyabiashara wa kuku, lakini alikamatwa na askari waliokuwepo mahakamani hapo wakiongozwa na mlalamikaji,
Abihud.
Yusufu alidai kuwa baada ya kukamatwa, aliingizwa katika gari la polisi lililokuwa limeegeshwa
mahakamani na kupelekwa nje kidogo ya mji, eneo la Ziwa Kindai ambako alipigwa na kutishiwa kuwa lazima wamlawiti.
“Walinivua shati na viatu na kunipiga miguunihuku wakinilazimisha nivue suruali. Nikakataa
hadi ikachanika lakini sikuivua, nikasema niueni tu….wakasema leo lazima tukulawiti….(kicheko mahakamani), baadaye wakanipeleka Kituo cha Polisi,” alidai Yusufu.
Alidai kuwa miongoni mwa waliomfanyia kisa hicho walikuwemo askari wawili wa kike na
wanaume wanne, lakini walioshiriki ni askari wa kike mmoja na wengine wanaume.
Katika shauri hilo, mlalamikaji askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Konstebo Abihud anadai kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake na kuibiwa simu ya mkononi.
Anadai kufanyiwa vitendo hivyo baada ya kukamata lori lililobeba matenga yenye kuku
waliokuwa wakisafirishwa na wafanyabiashara hao kwenda jijini Dar es Salaam.
PC Abihud alidai kuwa alilisimamisha lori hilo baada ya kuombwa na mgambo na watumishi
wa Manispaa kwa kile walichodai wafanyabiashara hao walikwepa kulipa ushuru.
Washitakiwa wote walikana mashitaka na wapo nje kwa dhamana hadi Jumanne ijayo.
Mkuu wa Shule adaiwa kumbaka mwanafunzi
Mkoani Kigoma, Fadhil Abdalla anaripoti kuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Chumvi katika Mji Mdogo wa Uvinza, Wilaya ya Kigoma, Laurent Ninga amepandishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Mkoa Kigoma na kusomewa mashitaka ya kumbaka mwanafunzi wake.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Amon Challe alidai jana kuwa Agosti 26, mwaka huu katika
Hoteli ya Zanzibar Lodge iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji, mshitakiwa alimbaka mwanafunzi
wake (jina limehifadhiwa).
Kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa Kigoma, Emmanuel Mrangu na baada ya kusomewa mashitaka, Amon alikana mashitaka hayo na amerudishwa rumande hadi Desemba 22, mwaka huu baada ya wadhamini wake kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
0 Comments