JUMLA ya wanafunzi 10 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wanashikiliwa na polisi baada ya kukamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya bangi, wengine wakikutwa wanaivuta.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ACP Fulgence C. Ngonyani amethibitisha kuwa wanafunzi hao walikamatwa Desemba 20, mwaka huu, majira ya saa 11.00 jioni katika maeneo ya Kitivo cha Elimu chuoni hapo baada ya kufanyika msako wa kuwasaka wanafunzi wahalifu.

Alisema katika msako huo jumla ya wanafunzi 10 walikamatwa wakivuta dawa za kulevya aina ya bangi katika maeneo ya kitivo hicho.

Kaimu kamanda aliwataja waliokamatwa katika maeneo ya kitivo cha elimu kuwa ni Joseph Jona (27), Mwakasitu Ikwisa (29), Chabae Mussa (25), Hamisi Issaka (25), Shaban Said (25), wanafunzi kitivo cha Elimu mwaka wa tatu na Stambuli Rahim (22), mwanafunzi wa kitivo cha
Elimu mwaka wa pili.


Alisema kuwa, mbali na wanafunzi hao sita, wanafunzi wengine wanne (4) walikamatwa
Desemba 15, mwaka huu katika kitivo cha Sayansi ya Jamii, Sanaa na Lugha kwa kosa la uvutaji
wa bangi ambao walipekuliwa katika eneo la tukio na kukutwa na misokoto 16 ya bangi.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Mutongore Filbert (27), mwanafunzi mwaka wa tatu, Samwel Seiboko (24), Ahmed Abdulaziz (20) na Nkembo Boniface (24), mwaka wa tatu wa shahada ya
uhasibu.

Alisema kuwa, wanafunzi hawa tayari wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Kaimu Kamanda alisema kuwa, msako huo ni endelevu katika vitivo vyote ili kuhakikisha vitendo kama hivyo vinakoma katika eneo lote la chuo cha UDOM.

Katika hatua nyingine, Kaimu kamanda aliwataka madereva na watumiaji wote wa barabara kuwa waangalifu kwa kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha.

Pia, aliwatakia wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma heri ya Krismasi na Mwaka Mpya kwani Jeshi la Polisi linawahakikishia wananchi wote kuwa ulinzi utaimarishwa ili kuwawezesha kusherehekea sikukuu kwa amani na utulivu.

“Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma anawaasa wakazi wote wa Dodoma kutumia haki ya kusherehekea vema sikukuu ya Krismasi na wananchi wakumbuke wajibu wa kuhakikisha kwamba usalama unadumishwa na kutii sheria zote,” alisema.

Pia aliwataka wenye kumbi za starehe na burudani kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa, vilevile wananchi wanaaswa wanapokwenda kwenye nyumba za ibada na kumbi za starehe kuhakikisha nyumba zao zipo katika hali ya usalama kwa kufunga milango, madirisha au kuwaacha baadhi ya watu kwa ulinzi wa makazi yao.