Waangalizi wa Afrika wamesema uchaguzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umekuwa na "mafanikio", licha ya wito wa upinzani kutaka uchaguzi huo ufutwe.

Makundi matano ya waangalizi yamesema licha ya kuwepo matatizo ya kufikisha vifaa kwa muda muafaka, vyama vya kisiasa ni lazima vikubaliane na matokeo.

Awali, wagombea wanne wa upinzani walisema uchaguzi wa Jumatatu lazima uahirishwe kwasababu ya kufanyiwa hila maeneo mengine.

Upigaji kura umeongezewa muda hadi Jumatano katika baadhi ya maeneo ambapo watu hawakuweza kupiga kura.

Mwandishi wa BBC Christophe Pons aliyopo mji mkuu, Kinshasa, amesema kuongezwa huko ni pamoja na ngome ya upinzani mjini hapo, ambapo makaratasi ya kupigia kura yalikuwa hayajafika mpaka Jumanne jioni.
Rais Joseph Kabila alikuwa na upinzani wa wagombea 10, akiwemo mshirika wake wa karibu Vital Kamerhe, ambaye ni miongoni mwa wagombea waliotaka uchaguzi ufutwe.


Zaidi ya wagombea 18,000 wamewania nafasi 500 za ubunge.

Kura zimehesabiwa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, huku matokeo rasmi ya urais yakitarajiwa kutolewa wiki ijayo na ya ubunge mwezi Januari, mwandishi wetu amesema.

Baada ya miongo mingi ya migogoro na ubadhirifu, Kongo, nchi ambayo ni theluthi mbili ya ukubwa wa Ulaya Magharibi, haina barabara wala reli.

Majeshi ya kutunza amani ya Umoja wa Mataifa nchini humo yamekuwa yakisaidia kupeleka vifaa vya upigaji kura kwa njia ya anga kwenye maeneo ambayo bado hawakupiga kura, shirika la habari la Reuters limeripoti.

Katika taarifa ya pamoja, waangalizi wa Umoja wa Afrika, SADC na makundi mengine matatu yalisema yaligundua matatizo hayo ya vifaa lakini wamefurahishwa na "mafanikio makubwa ya uchaguzi huo".