Tukio la kwanza la ajali lilitokea jana majira ya saa 6.15 usiku katika eneo la Chigongwe Manispaa ya Dodoma Barabara kuu ya Dodoma-Manyoni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Fulgence Ngonyani, gari lenye namba za usajili T.492 BTJ Toyota Noah likitokea jijini Dar es Saalam likielekea mkoani Shinyanga likiendeshwa na dereva ambaye hajafahamika jina lake aligonga kingo za barabara na kupinduka na kusababisha vifo vya watu wanne.
Aliwataja waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Hindu Abdarahamani(52) Mkazi wa Dar es Salaam, Mwajuma Abdarahamani (50) Mkazi wa Dar es Salaam, Hamisa Abdarahamani (40) Mkazi wa Dar es Salaam na Neema Ntandu(29) ambaye ni muuguzi katika Hospitali ya Muhimbili, mkazi wa Mbagala Dar es Salaam.
Pia aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Mwanaidi Zuberi(23), mkazi wa Temeke Dar es Salaam, Amina Ramadhani(10), mwanafunzi Shule ya Msingi Maganzo – Shinyanga, Zainabu Mazira (30), mkazi wa ukonga Dar es Salaam.
Wengine ni Suraiha Sadick (mwaka mmoja na miezi mitatu), Mkazi wa Ukonga Dar es Salaam, Rahma Abdarahamani(2), Mohamed Abdarahamani(2) na Abdarahamani Mohamed. Kaimu kamanda huyo alisema uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kuendesha kwa mwendo kasi na kushindwa kulimudu gari na kusababisha ajali hiyo.
Alisema dereva alikimbia baada ya kusababisha ajali hiyo na jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linaendelea kumtafuta.
Katika hatua nyingine aliwataka wenye kumbi za starehe na burudani kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa, vilevile wananchi wanaaswa wanapokwenda kwenye nyumba za ibada na kumbi za starehe kuhakikisha nyumba zao zipo katika
hali ya usalama kwa kufunga milango, madirisha au kuwaacha baadhi ya watu kwa ulinzi wa makazi yao.
Katika ajali nyingine watu wawili wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka na familia moja ya kanali wa jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ikinusurika kifo.
Katika ajali hiyo iliyohusisha gari la JWTZ aina ya Land Rover 110 lenye namba ya usajili 2495 JWTZ 97 lilipinduka eneo la Ikuzi wilayani Bukombe na kusababisha kifo cha askari mmoja Koplo Ache Said (27), kutoka Zanzibar na dereva wa gari hilo Allan Maulid waliofariki papo hapo.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani, jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa ajali hiyo ilitokea eneo hilo majira ya saa 2 usiku juzi wakati gari hilo lililokuwa limembeba Kanali wa Jeshi hilo Kamugisha (57) na familia yake lilitokea mjini Singida kuelekea mjini Bukoba mkoani Kagera.
Kamanda Athumani alisema watu sita wamejeruhiwa akiwemo Kanali Kamugisha ambaye pia ni mshauri wa mgambo wa mkoa wa Singida ameumia kiuno na miguu yote miwili na Revina Kamugisha (40) ameumia sehemu mbalimbali za mwili wake.
Wengine ni Paulina Kamugisha (18) ambaye ameumia kichwani na mbavu, Joshua Kamugisha (17), ambaye ameumia kifua, Doreene Kamugisha (8), ameumia shemu mbalimbali za mwili, Stephania Kamugisha (4) ameumia mbavu.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa mkoa majeruhi wote wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Bukombe na hali zao zinaendelea viuri.
Chanzo cha ajali hiyo hakijajulikana na polisi inaendelea na uchuguzi juu ya ajali hiyo huku kamanda wa polisi wa mkoa wa Shinyanga akitoa wito kwa madereva wote wa vyombo vya moto kuwa makini katika uendeshaji wao na kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Taarifa hii imeandikwa na Anceth Nyahore, Bukombe na Augusta Njoji, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments