Habari Leo

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi ameteua Kamati Maalumu ili kukamilisha mchakato wa kupendekeza vazi la Taifa ambalo litakuwa miongoni mwa vitambulisho mbalimbali vinavyotambulisha utaifa wa Tanzania.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana ilisema kuwa kamati hiyo itaanza kazi kesho na itatakiwa kukabidhi taarifa yake Februari 28, 2012 kwa Dk. Nchimbi.

Alisema hatua inayofuata sasa ni kuwashirikisha wananchi kuhusu mapendekezo yaliyopo na hatimaye kupendekeza vazi mahususi linalotambulisha utaifa wa Watanzania.

Wajumbe waliochaguliwa katika kamati hiyo ni pamoja na Joseph Kusaga ambaye atakuwa Mwenyekiti; Angela Ngowi Katibu; wajumbe ni Habibu Gunze, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali, Absalom Kibanda, Makwaia Kuhenga, na Ndesambuka Merinyo.

“Mchakato wa kupata vazi la taifa umeshapiga hatua kubwa, wabunifu wazalendo wa mitindo ya mavazi wameshashirikikishwa na kutoa mapendekezo yao,” alisema Waziri Nchimbi kwenye taarifa hiyo.

Alisema utafiti wa namna mataifa mengine yalivyoweza kuteua mavazi yao ya kitaifa ulishafanyika.

“Madhumuni ya kuwa na vazi la taifa ni kuongeza vitambulisho vya utaifa wa Watanzania, vikiwemo Ngao ya Taifa, Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa, Lugha ya Taifa-Kiswahili, Mlima Kilimanjaro, Twiga, na Mwenge wa Uhuru,” alisema Dk. Nchimbi.

Alisema vazi hilo litakuwa rasmi kwa wanaume na wanawake na linatarajiwa kuongeza utambulisho zaidi kwa taifa kama ilivyo kwa mataifa mengine yakiwemo ya Swaziland, Ghana, Nigeria, Sudan, Ethiopia na Mali.

Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Utamaduni ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilianzisha mchakato wa kupata vazi la taifa mwaka 2004.