BONDIA Karama Nyilawila(pichani kushoto) huenda akanyang’anywa Ubingwa wa Dunia unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi Ulimwenguni (WBF) endapo atazipiga na bondia Francis Cheka.
Taarifa ambazo zimetolewa na viongozi wa Shirikisho la ngumu nchini, zinasema Nyilawila atapokonywa ubingwa alionao endapo atang’ang’ania kuzipiga na Cheka kabla ya pambano lake la WBF linalotarajiwa kufanyika Februari 11, 2012.
Bondia Nyilawila alitaka kupanda uringoni kuzipiga na bondia Cheka Januari 28, pambano ambalo tayari limepata mdhamini licha ya kuibuka vikwazo hivyo.
Nyilawila anatakiwa kuzipiga na bondia Ermis Cagri ikiwa ni pambano la kutetea ubingwa anaoshikilia unaotambulika na WBF, na hatakiwi kufanya pambano lolote hadi hapo atakapomaliza mpambano huo mkubwa.
Hata hivyo PST tayari imegoma kutoa kibali cha kupambana kwa Nyilawila kuogopa lawama za bondia huyo kunyang’anywa ubingwa, endapo pambano hilo la kirafiki na Cheka litapigwa.
“PST haiwezi kutoa kibali cha pambano kati ya Cheka na Nyilawila kwani kufanya hivyo ni sawa na kuidhinisha Nyilawila kuvuliwa ubingwa wa dunia unaotambuliwa na WBF,” imesema taarifa hiyo.“PST pia inashangazwa na kitendo cha promota anayedhamini pambano la Nylawila na Cheka kung’ang’ania wakati kufanya hivyo anampotezea ubingwa unaotambulika duniani,” ilihoji taarifa hiyo kutoka PST.
0 Comments