NA RICHARD MAKORE
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekanusha madai kuwa kinafadhiliwa kwa kupatiwa fedha na Ujerumani.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alikanusha madai hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha ya kujadili masuala ya mabadiliko ya tabia nchi kwa viongozi na wanachama wa chama hicho.
Alisema sio kweli kwamba Chadema kinapata ufadhili wa fedha nyingi kama inavyovumishwa na baadhi ya watu.
Alisema kuwa Ujerumani imekuwa mfadhili mkubwa kwa serikali, lakini inapotokea ikatoa fedha kidogo kwa Chadema inakuwa nongwa.



Akizungumzia warsha hiyo, Dk Slaa alisema masuala ya mabadiliko ya tabia nchi yanamgusa kila mtu na kwamba hayajali itikadi ya chama chochote.
Aliwataka wanachama na viongozi wa Chadema kuhakikisha wanatoa elimu ya utunzaji mazingira ili kulinda uoto wa asili uliopo hapa nchini.
Mkurugenzi wa shirika la Konrad Adenauer Stiffing la (KAS) la Ujerumani, Stefan Reith, alisema, utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Alisema nchi yake imekuwa na uhusiano wa kirafiki kwa muda mrefu na Chadema na kwamba ushirikiano huo utaendelea kuwepo.
Aliwataka viongozi wa Chadema na wanachama wao kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutunza mazingira kwani yanamsaidia mwanadamu katika maisha yake ya kawaida ya kila siku.