HUDUMA MOI ZASITISHWA, WAGONJWA WARUDISHWA NYUMBANI, UONGOZI WADAI HALI NI SHWARI
HUDUMA katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili juzi zilizorota kutwa nzima kutokana na mgomo wa madaktari nchi nzima uliotangazwa juzi jioni na kuanza jana huku uongozi wa hospitali hiyo ukisisitiza kuwa huduma zilikuwa zikiendelea kama kawaida.
Mbali na hospitali hiyo, mgomo huo pia uliripotiwa kuathiri utoaji wa huduma katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road huku huduma zikiendelea kama kawaida katika hospitali nyingine karibu zote nchini.
Idara zilizoathirika zaidi na mgomo huo Muhimbili ni katika kitengo cha Tiba ya Mifupa (Moi) na Idara ya Wagonjwa wa Nje (OPD).
Tangu saa 12:30 asubuhi, idara hizo na wodi mbalimbali zilikuwa na msongamano wa wagonjwa hasa Moi, huku wagonjwa wa nje waliokuwa wamepokewa, wakiendelea kusubiri huduma ambayo hata hivyo, haikutolewa.
Huduma katika Idara ya Wagonjwa wa Dharura ziliendelea kama kawaida.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wagonjwa waliilani hatua ya madaktari hao kugoma huku wengine wakiitupia lawama Serikali kwa kile walichoeleza kuwa ndiyo chanzo cha adha hiyo.
Mmoja wa wagonjwa walioathirika, Damian Mselea ambaye kwa sasa anaishi Kimara, Dar es Salaam alisema alikuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi kabla ya kuhamishiwa Moi.
“Nimesafiri kutoka Moshi nikiwa na ndugu zangu na nilipofika leo (jana), wakalazimika kuniwahisha ili niweze kupata huduma ya matibabu, lakini hadi sasa sielewi nini kinaendelea,” alisema Mselea akiwa ndani ya gari la ndugu yake akiwa ameshakaa humo kwa zaidi ya saa saba bila ya kupata huduma.
Mgonjwa mwingine, Salome Raphael (64), mkazi wa Kinyerezi, Dar es Salaam ambaye alifika Moi kupata tiba ya mguu wake uliovunjika alisema: “Nimefika asubuhi na kuambiwa na watu wa mapokezi niende ofisi ya madaktari nikaangalie kama wapo kisha nirudi mapokezi ili waniandikie niende kumuona daktari.”
Alisema kwa kawaida, mgonjwa kabla ya kumuona daktari huanzia mapokezi na baada ya kuandikisha maelezo ndipo huelekezwa chumba cha daktari.
Kwa upande wake, Rehema Mohamed wa Madale, Dar es Salaam ambaye alifika Moi kutolewa nyuzi katika jeraha lake la mguu alisema licha ya kukaa wodini kwa muda mrefu hakuweza kumwona daktari na wala hakukuwa na dalili yoyote ya kuonana naye.
Vurugu OPD
Wakati wagonjwa hao wakiendelea kusubiri huduma, eneo la OPD nusura ligeuke uwanja wa mapambano baada ya wagonjwa waliofika kupata huduma za kliniki, kukosa tiba na kuanza kudai fedha zao.
Wagonjwa hao na ndugu zao walisema kuwa wanapaswa kurudishiwa fedha zao walizolipa kujiandikisha kwa kuwa hawakuwaona madaktari.
Hata hivyo, wagonjwa na watendaji katika eneo hilo walifikia mwafaka baada ya kukubaliana kupangiana tarehe nyingine za kwenda kuonana na daktari kwa fedha walizokuwa wameshatoa.
Mmoja wa wagonjwa hao, Willy Rwehumbiza alisema mgomo huo umemuathiri kwa ametokea mbali kufuata huduma za kliniki ambazo ni kila baada ya miezi sita.
“Sina ndugu, nimetoka Bukoba Mkoa wa Kagera, ni mfanyakazi katika Idara ya Elimu na nina matatizo ya moyo, kitendo hiki kimeniathiri sana, sijui itakuwaje” alisema akiwa kwenye foleni ya kwenda kupangiwa tarehe nyingine.
Mgonjwa mwingine, Flora Roman alilalamikia kupangiwa kurejea Machi 27, mwaka huu... “Hii ni hatari, sisi tutakufa sasa, leo nimekuja nimekosa huduma napangiwa Machi 27, hii si hatari! Tutafika kweli?.”
Kwa upande wake, mgonjwa Theresia Mapunda wa Kimara, Temboni Dar es Salaam, alisema alifanyiwa operesheni Septemba mwaka jana na alipangiwa na daktari kurejea kwa uchunguzi kila mwezi lakini.
“Nimeshangazwa na hutua hii. Kila mwezi nakuja kufanyiwa uchunguzi, leo nimekuja Sh5,000 wamechukua na nimepangiwa kurudi Machi 27,” alisema Mapunda.
Waokoa jahazi
Wakati madaktari wakiwa katika mgomo, habari zilizopatikana zimesema waliokuwa wanaendelea kufanya kazi katika vitengo mbalimbali hospitalini hapo ni madaktari walio kwenye mkataba na wanafunzi waliotoka chuoni.
Hata hivyo, eneo lililokuwa likiendelea kutoa huduma katika Taasisi ya Moi ni la wagonjwa wa dharura pekee ambalo mmoja wa madaktari alisema wameona ni vyema kutoa huduma hapo kwa sababu wanaofikishwa ni wagonjwa wenye mahitaji ya haraka.
Licha ya kuwapo kwa hali hiyo, Ofisa Habari Mwandamizi wa Hospitali hiyo, Aminiel Aligaeshi aliwaambia waandishi kuwa madaktari wanaendelea na kazi na hakuna hata mmoja anayegoma.
“Hapa kazi zinaendelea kama kawaida, wagonjwa wanatibiwa oneni wenyewe” alisema Aligaeshi.
Alisema hospitali hiyo ya taifa ina madaktari 248 na madaktari walio katika mafunzo ya vitendo 174 na kwamba wote wako kazini.
Ofisa huyo aliwatembeza waandishi wa habari katika moja ya wodi hospitalini hapo kujionea hali halisi.
Hata hivyo, ofisa huyo alikataa kuwapeleka waandishi katika kitengo cha OPD ambako ndiko kulikokuwa na idadi kubwa ya wagonjwa waliokuwa wakisubiri huduma akisema: “Muda umekwisha si mmeshaona watu wanafanya kazi!”
Mgomo wayeyuka
Hata hivyo, wakati mgomo huo ukifanikiwa Muhimbili, huduma katika hospitali nyingine kubwa nchini zikiwamo Temeke, Ilala, Mwananyamala na Hospitali za mikoa ya Tanga, Dodoma, Iringa, Shinyanga, Arusha, Mara na Kilimanjaro ziliendelea kama kawaida.
Madaktari katika Hospitali za Mount Meru, Bugando, Bombo, Hospitali Teule ya Muheza, Korogwe na Bunda waliendelea na kazi. Madaktari katika Hospitali za Magunga na Bombo mkoani Tanga walisema wanasubiri kwa hamu maagizo kutoka kwa viongozi wao ili nao wagome kuishinikiza Serikali ili isikilize kero zao.
Katibu Mkuu wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda, Billy Kinyaha alisema hakuna mgomo wowote kauli iliyothibitishwa pia na baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Samson Winani alisema hakuna mgomo wowote uliofanyika: “Sisi huku hatujagoma. Wanaogoma ni wa huko Dar es Salaam.”
Katika Hospitali ya Mount Meru, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo ya Mkoa wa Arusha, Dk Omar Chande amesema madaktari wote jana walikuwa wakichapa kazi. Hata hivyo, hakuna daktari aliyekuwa tayari kueleza ni kwa nini hawakutekeleza maagizo ya kugoma kuanzia jana.
CUF walia na mawaziri
Katika hatua nyingine, Chama Cha Wananchi (CUF), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwawajibisha Waziri wa Afya, Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya kwa kile kilichodai kuwa wameshindwa kutatua tatizo hilo.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, chama hicho kilisema mbali na viongozi hao wa kisiasa, Rais pia anapaswa kuwawajibisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa.
“CUF tunamtaka Rais Kikwete kuwawajibisha wote kuanzia waziri, naibu waziri, katibu mkuu, mganga mkuu wa Serikali, ambao wote ni wahusika wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwa kufanya kazi kwa dharau,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Haki za Binadamu, Amina Mwidau.
Habari hii imeandikwa na Geofrey Nyang’oro, Aidan Mhando, Gedius Rwiza, Burhani Yakub na Raisa Said, Tanga; Ahmed Makongo, Bunda; Mussa Juma, Arusha na Sheilla Sezzy, Mwanza.
0 Comments