Aisha Hamisi (kushoto) akifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam akikabiliwa na shitaka la mauaji ya Meja John Tewete.

Makongoro Oging' na Haruni Sanchawa
 MAUAJI ya Meja wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), John Tewete, 57, yaliyotokea saa 2.30 kabla ya mwaka mpya 2012, yametikisa Jiji la Dar es Salaam na kuwaacha watu wengi na huzuni kubwa.
Mauaji hayo ya kikatili yalifanyika Vingunguti Mtakuja, siku ya mkesha wa mwaka mpya na anayetuhumiwa ni mwanamke mmoja aliyetajwa kwa jina la Aisha Hamisi.
Aisha, anadaiwa kutumia kisu kumchoma tumboni na mgongoni meja huyo, hivyo kumsababishia kifo.
Uwazi limebaini kuwa Aisha alimchoma visu meja huyo baada ya kumfumania akiwa na mwanamke mwingine anayeitwa Saada Musa, 20.
MWANAMKE ALIYEFUMWA NAYE ASIMULIA JINSI ALIVYOUAWA
Ili kujua undani wa sakata hilo, gazeti hili lilihojiana na Saada ambaye alisimulia mkasa mzima kama ifuatavyo:
“Nakumbuka siku hiyo alifika hapa nyumbani kwangu saa 7.00 mchana huku akiwa na mizigo, nikampokea na kumkaribisha ndani, niliandaa chakula tukala naye.
“Tuliongea naye hadi saa 3.00 usiku alinieleza kwamba anaondoka kwenda nyumbani kwake. Nilikataa asiende nyumbani usiku ule badala yake alale, akajibu kuwa hawezi kulala kutokana na kwamba nyumbani kwake kuna mgonjwa, yaani kaka yake na hakuna mtu wa kumwangalia, nilimruhusu.


“ Mimi na mfanyakazi wetu wa ndani pamoja na mtoto wa kiume wa dada yangu tulimsindikiza, baada ya hatua kadhaa kutoka nyumbani kwangu tulikutana na mwanamke amebebwa kwenye pikipiki, hatukumjua kuwa ni Aisha Hamisi.

“Tulipishana naye, kabla hatujaenda mbali tulishtukia mtu anaruka toka kwenye pikipiki iliyokuwa nyuma yetu, alitufuata akiwa na kisu mkononi, mtoto wa dada yangu alinisukuma, nikadondoka chini, nilipoamka nikatimua mbio.
“Nikiwa mbali nilimsikia Meja Tewete akilia huku akitoa sauti ya kuomba msaada, kumbe wakati huo ndiyo alikuwa ameshachomwa kisu mgongoni na tumboni hadi utumbo ukaning’inia.
“ Meja aliendelea kuomba msaada, kwa kweli kwa muda huo kila mtu alikuwa muoga nami nikawa natetemeka, watu wakawa wanaogopa kumpokonya kisu mwanamke yule.
“Nilipatwa na uoga nikakimbia hadi kwangu, nikajifungia, nilimuacha meja akiendelea kulia huku akiomba msaada. Tangu niwe na uhusiano na Tewete sasa yapata mwaka moja. Tulifahamiana naye wakati tunafanya kazi pamoja na Aisha katika jiko la chakula huko Mgulani JKT.
“Meja alikuwa mpenzi wa Aisha, ni jambo lililokuwa wazi kwani hata mwenyewe (Aisha) hakunificha kwa kuwa tulikuwa marafiki sana.
“Mapenzi kati ya Aisha na meja yalipungua kwa kiasi kikubwa yakahamia kwangu, rafiki yangu huyo alikuja kugundua baadaye kwamba nina uhusiano wa kimapenzi na Tewete, akaanza kunichukia na kinitishia kuniua nikawa ninamweleza meja naye akawa ananishauri nimpuuze kwani hana jeuri hiyo.
“Penzi letu liliendelea na meja, alinihadi kuwa tutafunga ndoa hivi karibuni. Nilimkubalia akaniachisha kazi kule Mgulani JKT ili kuondoa mgogoro kati yangu na Aisha.Nikawa nyumbani na akawa ananihudumia kila kitu,” alisema Saada.
 MFANYAKAZI WA NDANI
Naye mfanyakazi wa ndani wa Saada alikuwa na haya ya kusema: “Wakati meja anashambuliwa tulishindwa kumuokoa kwa sababu Aisha alishika kisu. Baada ya mzee kuchomwa kisu alikimbia kama hatua kumi hivi huku utumbo ukining’inia, aliishiwa nguvu na kuanguka kando ya mtaro.
“Watu walianza kutoka majumbani na kuja katika eneo la tukio, walimkuta Aisha akiwa amesimama, akatokea mwanaume mmoja ambaye alimkwida (Aisha) na kumnyang’anya kisu, baadaye polisi walitokea na kumkamata.
“Polisi walimkuta meja akikoroma, walimchukua Aisha na majeruhi wakamkimbiza Hospitali ya Amana.”
NI PENGO KUBWA
Ofisa huyo alikuwa tegemeo kubwa ndani ya JWTZ hasa katika fani ya ufundi ndege, katika Kikosi cha Anga cha 603, Air Wing Ukonga Dar es Salaam.
Ameacha pengo kubwa kwani alikuwa anategemewa sana na taasisi hiyo nyeti nchini hususan kwenye ufundi wa ndege.

VINGUNGUTI WANASEMAJE?
Baadhi ya wakazi wa Vingunguti Mtakuja walilieleza gazeti hili kuwa Kamanda Tewele siku hiyo ya tukio saa 6.30 mchana aliwapita akiwa amebeba kifurushi cha maembe na mzigo mwingine uliofungwa kwenye kiboksi na karatasi za kung’ara ulioonekana kuwa ni zawadi.
Wananchi hao ambao hawakupenda majina yao kuandikwa gazetini walisema kwamba kamanda huyo alikuwa akipita eneo lao mara kwa mara na kuwasalimia wakati akienda kwa Saada.

POLISI WALIOMKAMATA AISHA
Mmoja wa askari polisi waliomchukua Meja Tewete aliyezungumza na mwandishi wetu (Jina linahifadhiwa kwa kuwa siyo msemaji wa jeshi) alisema kwamba wakati wanamkimbiza Hospitali ya Amana kuokoa maisha yake, alikata roho njiani saa 3.30 usiku kutokana na kuvuja damu nyingi .
Polisi huyo alisema, akili ya Aisha ilibadilika ghafla akawa anazungumza maneno yasiyokuwa na mpangilio huku akiwa amevua nguo zake zote na kubakia na chupi tu.
“Tulijaribu kumshauri avae nguo zake, alikataa na akawa hivyo hadi tulipofika Kituo Kidogo cha Polisi cha Vingunguti Mtakuja,”alisema polisi huyo.
Taratibu za mazishi zilifanyika kijeshi na mwili wa marehemu ulisafirishwa Januari 3 mwaka huu na kuzikwa Januari 4, 2012 nyumbani kwao Tanga.