Waandishi wetu
LICHA ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa amri kwa madaktari wote wenye mikataba na Serikali kurejea kazini, bado wanataaluma hao jana waliendeleza mgomo baada ya kutia saini vitabu vya mahudhurio na kutoweka kusikojulikana huku wauguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wakitoa msimamo mpya kwamba hawako tayari kufanya kazi na madaktari kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ).
Juzi, Waziri Mkuu Pinda alitoa onyo kwa madaktari hao akiwataka kurejea kazini kufikia jana kinyume chake ambaye angeshindwa angekuwa amejifukuzisha kazi na kwamba madaktari wa JWTZ wangechukua nafasi zao.
Agizo hilo la kwamba wangewatumia madaktari kutoka JWTZ jana liliamsha hasira za wauguzi Muhimbili ambao walitangaza msimamo wao wa kutofanya kazi nao.
Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi Tanzania, Tawi la MHN, Paul Magesa alisema madaktari hao hawana uwezo wa kufanya kazi katika hospitali hiyo ya taifa ambayo ndiyo kubwa nchini kwa kuwa inahudumia wagonjwa walioshindikana katika hospitali wanazotoka.
“Ifahamike kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni ya rufaa na inapotokea wagonjwa walioshindikana katika hospitali nyingine inakuwaje leo wakaletwa madaktari kutoka katika hospitali hizo kuja kutibu?” alihoji Magesa na kuongeza:
“Sisi tulishafanya kazi nao mwaka 2005 na tunawafahamu wengi hawajui mambo mengi, watakuja kutuuliza na kutuongezea kazi za kufanya... tunaomba katika hili Serikali isikwepe tatizo, ilishughulikie kwa maslahi ya taifa,” alisema.
Hali mbaya
Hali katika hospitali hiyo kuu ya nchini imezidi kuwa mbaya, kutokana na kuendelea kwa mgomo wa madaktari hao huku kukiwa na dalili nyingine za mgomo wa wauguzi kupinga kufanya kazi na madaktari kutoka jeshini.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na uongozi wa hospitali hiyo, zilisema kwamba madaktari wengi walifika na kusaini katika kitabu cha mahudhurio na kuondoka.
Mmoja wa madaktari katika hospitali hiyo, Dk Azizi Keto aliyekuwa katika wodi ya Mwaisela alisema kauli ya Pinda dhidi ya madaktari imewakatisha tamaa na kuwavunja moyo wa kufanya kazi. Alisema hali ni mbaya ndiyo sababu hata waliofika asubuhi hawakujisikia kufanya kazi.
Katika hospitali hiyo madaktari walioendelea na kazi ni wale washauri, wanaotarajia kustaafu na walioingia mkataba na Serikali mwaka 2005, walipoitwa wakati madaktari walipogoma.
Vilio vilitawala jana katika eneo la nje ya Wodi ya Mwaisela huku waombolezaji wakidai kuwa kama si mgomo huo wa madaktari, ndugu zao wasingepoteza maisha.
Mmoja wa waombolezaji alikaririwa akisema ndugu yake alipoteza maisha bila ya kupata huduma hospitalini hapo.
Baadhi ya wagongwa waliowasili katika hospitali hiyo wakitokea hospitali mbalimbali, walirudishwa bila ya huduma.
Muhimbili yakiri
Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mgomo huo, uongozi wa MNH umekiri kwamba hali ya upatikanaji wa huduma katika hospitali hiyo imezidi kuzorota.
Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Hospitali hiyo, Aminael Aligaesha aliwaambia waandishi wa habari kuwa madaktari walio wengi wamefika na kujiorodhesha kwenye daftari la mahudhurio lakini wakagoma kufanya kazi.
Hospitali za Dar
Kwa upande wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, madaktari wamegawanyika wengine waliendelea na mgomo na wengine walionekana wakitoa huduma kwa wagonjwa.
“Pamoja na kwamba wagonjwa wanahudumiwa lakini, inachukua muda mrefu kuipata huduma jambo linaloonyesha kuwa mgomo upo,” alisema mmoja wa wagonjwa hospitalini hapo.
Taarifa hizo ziliongeza kwamba madaktari waliogoma, jana asubuhi walifika hospitalini hapo na kusaini majina yao kisha kuondoka.
Habari zilisema maofisa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, walifika hospitalini hapo kuhakiki majina ya madaktari hao lakini walipoondoka na wao wakaondoka.
Katika Hospitali ya Amana, Ilala nako baadhi ya madaktari walifika kazini wakasaini mahudhurio na kuondoka bila kufanya kazi yeyote.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Shimwela Meshack alisema hali ni mbaya katika hospitali hiyo kutokana na madaktari wote kufika kazini lakini wakagoma kutoa huduma.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk Sophinias Ngonyani alisema mgomo huo ulifanywa na madaktari ambao hawajaajiriwa tu.
“Mgomo huu upo kwa wale wasioajiriwa ila tunachokifanya kwa sasa ni kuhakiki waliokuwepo na wasiokuwepo kujua idadi ilio sahihi,” alisema.
Ofisa Afya wa Manispaa ya Kinondoni, Dk Gunini Kamba alisema hospitali hiyo ina wataalamu wa afya 58, kati yao 42 ni madaktari, watano wako katika kitengo cha wafamasia, watano wengine maabara na sita katika kitengo meno.
Hospitali mikoani
Mkoani Morogoro, madaktari walifika kazini kama kawaida lakini hawakutoa huduma hali iliyofanya wagonjwa wasote kwa muda mrefu bila huduma.
Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Frida Mokiti alisema madaktari wote wameripoti kwenye maeneo yao ya kazi na kwamba taarifa zaidi angezitoa baada ya muda wa kazi.
Hali kama hiyo pia iliripotiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru ambako madaktari waliingia kazini lakini baada ya kusaini daftari la mahudhurio waliendelea na mgomo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo jana asubuhi alifanya ziara ya ghafla katika hospitali hiyo na kuonana na uongozi. Hata hivyo, hakuna taarifa ambayo ilitolewa juu ya nini kilichozungumzwa.
Madaktari wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, waliendelea na mgomo huku baadhi yao wakisisitiza kuwa hawawezi kurejea kazini hadi Serikali itakapoamua kutekeleza madai yao.
“Sisi tunachokitaka ni kutekelezewa madai yetu, hiyo kauli ya Waziri Mkuu ya kututishia kutufukaza kazi kama hatutarejea kazi kuanzia leo (jana) wala hatuiogopi hata kidogo, tunachotaka ni haki yetu itendeke,” alisema mmoja wa madaktari kwa sharti la kutotajwa jina.
Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk Eleuter Samky alisema hadi saa 7:00 mchana jana kulikuwa na madaktari watano tu kati ya 75 waliokuwa wamefika kazini.
Katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi, hali pia imekuwa ya kusuasua. Jana kulikuwa na msururu mkubwa wa wagonjwa wa nje waliokuwa mapokezi, wakisubiri huduma kwa zaidi ya saa nane huku wengi wakilalamikia uchache wa madaktari kwani aliyekuwapo zamu alikuwa mmoja tu.
Baadhi ya madaktari ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini walisema mgomo wa sasa ni mbaya kuliko ule wa awali kwani kwa sasa wanaandika majina yao kwenye daftari la mahudhurio lakini hawatoi huduma kwa wagonjwa.
Wanasiasa waingilia kati
Baadhi ya wanasiasa wameingilia kati mgomo huo wakiwataka madaktari hao kurejea kazini kama walivyoagizwa na Pinda ili kuokoa maisha ya Watanzania.
“Uhai wa mtu ni kitu kikubwa sana… Mimi naona ni vyema busara ikatumika ili kuokoa maisha ya Watanzania yanayopotea,” alisema Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Hata hivyo, alisema madaktari hao wanayo madai ya msingi lakini akawataka watekeleze wajibu wao huku wakifanya mazungumzo na Serikali.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema madaktari wanapaswa kufahamu kwamba kuendelea kugoma ni kuchezea maisha ya wananchi.
Alisema kitu cha muhimu ni madaktari hao kurudi kazini kama walivyoagizwa na Waziri Mkuu na wasifikiri kwamba, Serikali itaendelea kuwavumilia huku ikiona maisha ya Watanzania yanapotea.
Aliwataka wajifunze kwa kilichotokea mwaka 2004 wakati wa utawala wa Rais Benjamini Mkapa, ambako waligoma na Serikali ikaamua kutumia madaktari kutoka vikosi vya jeshi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alimtaka Pinda kuacha vitisho na matumizi makubwa ya vyombo vya dola kwa madaktari wanapotumia uhuru wao wa kikatiba wa kukusanyika huku akisema chama hicho kinaunga mkono madai ya msingi ya madaktari.
Tucta yawageuka
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limesema haliwaungi mkono madaktari hao kutokana na kushindwa kufuata utaratibu wa mgomo.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Nicholaus Mgaya alisema sababu ya kutounga mkono mgomo huo ni baada ya madaktari hao kukaidi wito wa kukutana na Serikali jambo ambalo alisema ni kinyume na taratibu za kazi.
“Kwa hali hii madaktari wamepotea maboya. Kitendo cha kuitwa na Waziri Mkuu ili kufanya mazungumzo na kukataa ni dhahiri kuwa mgomo huo si halali maana walitakiwa kusikiliza Serikali inasemaje baada ya hapo wangeweza kukataa kama wangeona bado madai yao hayajafanyiwa kazi lakini kitendo cha kugoma bila kufanya mazungumzo ni kosa,” alisema Mgaya.
Habari hii imeandaliwa na Geofrey Nyang'oro, Gedius Rwiza, Leon Bahati, , Raymond Kaminyoge na Joseph Zablon, Dar; Godfrey Kahango, Mbeya; Mussa Juma, Arusha na Rehema Matowo, Moshi.
0 Comments