HAPA NI ISEVYA-TABORA
Ndugu zangu,
Baada ya safari ndefu ya kutoka Iringa, Mtera, Mpwapwa, Dodoma na Singida, hatimaye mchana wa leo nimewasili Mboka- Manyema- hivi ndivyo Mji wa Tabora ulivyojulikana na wageni kutoka Mashariki ya Congo DRC.
Nilikuwa sijafika mji wa Tabora kabla. Hakika, nimebahatika kutembelea miji yote ya mikoa ya Tanzania Bara, na mji wa Tabora umekuwa ni mji wa mwisho wa mikoa ya nchi hii ambayo nimebahatika kuitembelea.
Turudi Mboka- Manyema. Wamanyema wana historia katika mji wa Tabora. Wamechangia kwenye kuujenga mji huu. Athari chanya za uwepo wa Wamanyema katika Tabora ni pamoja na kwenye muziki. Kuna mnaokumbuka Nyanyembe Jazz na Tabora Jazz, kulikuwa pia na Kiko Kids. Wimbo kama ' rangi ya chungwa' umepigwa na Tabora Jazz. Kulikuwa na Mmanyema Shem Kalenga aliyewika sana enzi hizo. Ni kwa kucharaza gitaa la solo na kuimba. Mwingine aliyetokea Tabora Jazz ni mpiga gitaa la Solo aitwaye Rashid Hanzurun ambaye hata Mzee Lwambo Makiadi alipata kumvulia kofia.

Lakini, hata klabu yangu ya Simba imenufaika sana na uwepo wa watani zangu Wanayamwezi. Tuna kina Samwel Sitta, Othman Kapuya na Aden Rage. Lakini, Mnyamwezi pekee aliyeifanyia makubwa klabu yangu ya Simba ni Athuman Mambosasa. Achana na Mmanyema Juma Kaseja na Mnyamwezi wa Urambo Juma Pondamali aliyepotea njia na kuishia Yanga ya kwenye bonde la Msimbazi kwa kudanganywa kuwa ni Jangwani! Tangu lini jangwa likakumbwa na mafuriko?! Naamini, Mambosasa ndiye golikipa bora aliyepata kutokea katika nchi hii.

Wanyamwezi wengine waliopotea njia mjini Dar es Salaam na kuishia bonde la Msimbazi kwenye klabu ya Yanga ni pamoja na Ahmed Amasha na Yussuf Ismail Bana,

Tabora pia imewatoa Watanzania mahiri waliowika kwenye siasa na hata siasa za upinzani. Tunazungumzia majina kama Julius Nyerere aliyetokea Tabora Boys na ambaye ustaarabu wa Waswahili ikiwamo kunywa kahawa na kucheza bao alijifunzia Tabora. Ikamsaidia sana alipofika kwa Waswahili wa Dar. Kuna majina kama Kasela Bantu, Kasanga Tumbo, Chifu Abdalah Fundikira na James Mapalala.

Naam, huwezi kuisimulia historia ya ukombozi wa nchi hii ikakamilika bila kuutaja mkoa wa Tabora.
Ndugu zangu,
Ngoja nikanyoshe miguu kwenye mitaa ya Tabora Mjini. Na bila shaka nitafika kwenye moja ya vijiwe vya kahawa vya mji huu. Na ukitaka kujua yanayoendelea mjini, basi, ni kwenye vijiwe kama hivyo utazikuta habari ambazo hata magazetini huwezi kuzisoma.

Maggid ,
Mboka- Manyema- Tabora