MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, amemtaka Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, kuendeleza makali yake katika utendaji kazi huku akiwataka wananchi kumwunga mkono katika juhudi zake kwa alichodai kuwa ni mpambanaji wa kweli.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa utiaji saini mkataba wa ujenzi wa daraja la Kigamboni kati ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Kampuni ya CRCEG ya China, Sadiki alisema utendaji wa Magufuli umelenga katika usimamizi wa sheria na yote yanayojitokeza, ni kwa sababu ya kuzisimamia na kuzitekeleza vyema sheria hizo.

Alisema Waziri huyo alipotamka kauli ya kupiga mbizi, inawezekana aliitoa kutokana na mazoea ya utani na kwamba inawezekana pia dhamira kuhusu kauli hiyo hakuwa nayo.

“Hatukatai hata kama ana upungufu wake, basi apewe sifa katika yale mazuri anayoyafanya, lakini ukweli ni wazi kuwa Magufuli ni kiongozi mchapakazi na msimamizi mzuri wa sheria na hilo halipingiki,” alisema Sadiki.




Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alisema siku zote utendaji kazi wa Magufuli unafuata sheria na taratibu, ambapo alimtaka kuendelea na moyo alionao kama anavyofanya siku zote kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo.
“Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, wengi tunamtambua Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya, tunakuomba uendelee kufanya hivyo hivyo wala hutofeli na ukiendelea na moyo huo sote hatutafeli,” aliongeza Kabaka.

Kwa upande wake, Magufuli alisema mambo mengi yanayofanyika ni utekelezaji wa sheria na ili kila kitu kifanyike kikamilifu, ni lazima siasa ziwekwe pembeni kwa ajili ya kufikia malengo hayo.

Kuhusu ujenzi wa daraja hilo utakaogharimu Sh bilioni 214.6 Magufuli alisema hatua ya kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wake ni mafanikio yanayokuja kutokana na ahadi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa kwa Watanzania wakati wa kampeni za urais mwaka 2010.

“Katika hili, Ilani ya Rais Kikwete katika uchaguzi imetimia, kwa hili vyama vyote vya siasa na
dini zote zitamkumbuka kwa ujenzi wake, ninamwomba Mungu likamilike haraka, ili aweze kulizindua akiwa bado rais wa nchi hii,” alisema Magufuli.

Alimtaka Mkandarasi anayelijenga, kuhakikisha anamaliza ujenzi wake kabla ya miezi 36 aliyopanga kutumia kwa kuwa fedha za ujenzi tayari zipo, hivyo hakuna sababu ya kutumia muda wote huo.

Aidha, alisema mipango ya Serikali kuhusu Jiji la Dar es Salaam katika siku zijazo, ni kujenga
barabara za kuvutia katika maeneo yote zitakazofanya wananchi kutoka mikoa mingine kufunga safari kwa ajili ya kuja kuzishangaa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa NSSF, Ramadhan Dau, Shirika lake limetoa asilimia 60 ya
fedha za ujenzi wa daraja hilo, huku Serikali ikichangia asilimia 40 na mchakato wa kumpata
mkandarasi ulipitia hatua mbalimbali stahiki.
                                                                       Habari Leo.