WATU watano wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka yaliyokuwa yakiwakabili ya wizi wa kutumia silaha kwenye duka la kubadilishia fedha jijini Dar es Salaam.

Washitakiwa hao ni wakazi wa jijini Dar es Salaam, Mussa Mmuiba (30), mkazi wa Yombo, Yohana Keyela (25) mkazi wa Keko, Hadis Said (29) na Richard Tawete (30) wakazi wa Kigogo na Michael Sangu (32) mkazi wa Mbeya.

Akitoa hukumu hiyo jana hakimu wa mahakama hiyo, Hellen Liwa alisema ameridhishwa na ushahidi wa upande wa mashitaka na washitakiwa watatumikia kifungo hicho jela ili iwe fundisho kwao na wengine wenye tabia kama hiyo.

Alisema katika wizi huo washitakiwa walimsababishia ulemavu askari aliyekuwa hapo ambaye ni Koplo Edwin kwa hiyo watu hao ni hatari kwa jamii kutokana na matendo yao.



Katika mashitaka yao washitakiwa hao walidaiwa kula njama ya kutenda kosa la wizi wa kutumia silaha, shitaka la pili walidaiwa kufanya kosa la wizi wa kutumia silaha ambapo maelezo ya kosa walidaiwa, Mei 8, 2009 katika duka la kubadilishia fedha la Kifene lililoko Mchikichini jijini Dar es Salaam waliiba vitu vyenye thamani ya Sh 424,000 zikiwemo simu za mkononi mali ya Oliver Mujuni na kwamba walimtishia kwa silaha ili kutimiza azma yao. Shitaka la tatu walidaiwa pia kufanya wizi wa kutumia silaha katika duka hilo na siku hiyo hiyo waliiba Sh milioni 12, mali ya Omary Ally na kwamba walimtishia kwa silaha Mujuni ili kupata fedha hizo.

Shitaka jingine walidaiwa kumjeruhi askari Koplo Edwin kwa kumpiga kwa risasi begani kwa kutumia bunduki submachine gun na kumsababishia maumivu makali. Mahakama hiyo iliamuru vielelezo ambavyo ni fedha, simu na pochi warudishiwe wenye navyo na kuamuru askari aliyejeruhiwa kulipwa fidia na Jamhuri.