Na Richard Bukos
KATI ya matukio ya mastaa wa kike yaliyotia aibu katika msiba wa mkongwe wa sanaa za maigizo Bongo, Fundi Said ‘Mzee Kipara’ ni pamoja na vicheko vya kishambenga vya hapa na pale kutoka kwa wasanii, Ijumaa Wikienda lilishuhudia.
Wasanii hao waliokuwa sehemu ya umati uliofika kwenye mazishi ya mzee huyo yaliyochukua nafasi Kigogo jijini Dar es Salaam, Alhamis iliyopita, mara kadhaa walionekana wakicheka licha ya kuwepo kwenye tukio la kuhuzunisha.
Miongoni mwa wasanii walionaswa na kamera yetu wakiwa na sura za tabasamu na wengine wakiangua vicheko kabisa kana kwamba walikuwa kwenye sherehe ni Wema Sepetu, Ummy Wenslaus ’Dokii’, Mayasa Mrisho ‘Maya’, Nuru Nassoro ‘Nora,’ Blandina Chagula ‘Johari,’ Sabrina Rupia ‘Cathy’, Rachel Haule ‘Recho’ na wengineo.
Hata hivyo, licha ya baadhi ya watu kushangazwa na kituko hicho, wapo waliowatetea wakieleza kuwa si kila anayekuwa msibani lazima muda wote awe amenuna.
“Yaweza kuwa aibu kama mtu atakuwa anachekacheka ovyo tena kwa sauti msibani kama walivyokuwa wakifanya baadhi yao lakini pia siyo kwamba ukiwa msibani muda wote lazima unune.
“Kuna wakati utajikuta ‘automatikale’ umecheka lakini si kwamba inaonesha kutoguswa na msiba husika,” alisema Maria Said aliyehudhuria mazishi hayo.
Mzee Kipara alifariki dunia Jumatano alfajiri na kuzikwa Alhamisi iliyopita katika makaburi ya Kigogo.
0 Comments