ALIYEKUWA mgombea urais chama cha upinzani nchini Burundi, Alexis Sinduhije (46) (Pichani juu).
anashikiliwa na Jeshi la Polisi nchini kwa tuhuma za mauaji aliyofanya nchini kwake.

Akizungumza na chanzo cha habari hizi Jumapili kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi wa Mashitaka ya
Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, alisema kuwa Sinduhije atafikishwa mahakamani kesho na kusomewa mashitaka ya mauaji aliyofanya Burundi.

“Ni taratibu tu za kisheria, amekamatwa hapa nchini baada ya kupokea maombi kutoka nchini
kwake na atafikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka yake,” alisema Manumba akithibitisha kukamatwa kwa muasisi huyo wa chama cha siasa cha Movement for
Solidarity Development.

Manumba alisema ni jambo la kawaida ambaye sio raia wa hapa nchini kusomewa mashitaka hapa nchini hata kama hakufanya makosa hayo hapa na kesi itaweza kuhamishiwa nchini kwake.



Aidha Manumba alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa hapa nchini Januari 12 mwaka huu na yuko mahabusu ya Polisi Kituo cha Kati baada ya juzi kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kushindwa kusomewa mashitaka yake kwa kuwa mambo kadhaa ya kisheria yaliyohitajika hayakuwa yamekamilika. Juzi Sinduhije, mtangazaji wa zamani wa mashirika ya habari ya Uingereza, Reuters na BBC akiwa mwakilishi wa nchi za Rwanda na Burundi alifikishwa katika Mahakama ya Kisutu hata hivyo hakusomewa mashitaka yake aliishia mahabusu ya Mahakama hiyo na baadaye kuondolewa na gari la Polisi.

Mwendesha Mashtaka Kiongozi wa Mahakama hiyo, Elizabeth Kaganda alipohojiwa na
waandishi wa habari naye alisema kuwa Sinduhije alirejeshwa mahakamani kwasababu kuna mambo kadhaa ya kisheria hayajakamilishwa ndio maana ilishindikana kumsomea mashitaka yake ingawa hakufafanua ni mashitaka gani.

Kaganda alisema amewaambia polisi waondoke na mtuhumiwa mpaka watakapokamilisha mapungufu ndio aletwe kusomewa mashitaka yanayomkabili.