Na Rhobi Chacha.
NDANI ya takribani miaka miwili, tayari mwigizaji wa filamu za Kibongo, Blandina Chagula ‘Johari’ amenusa kifo mara mbili baada ya kupata ajali mbaya.
TUKIO BICHI
Tukio bichi kwenye makabrasha yetu ni lile lililojiri mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo Johari alipata ajali maeneo ya Ubungo kwenye mataa, Dar es Salaam na kusababisha gari lake aina ya Toyota Opa lenye namba za usajili T 178 BKU kubondeka, ni Mungu tu aliyemkwepesha na kifo.
NI UBUNGO MATAA
Kwa mujibu wa chanzo makini, Johari alikuwa akitokea Barabara ya Mandela na alipofika Ubungo kwenye mataa, alisubiri kidogo kabla ya taa kuruhusu magari yanayofuata Barabara ya Sam Nujoma aliyokuwa akielekea.
Chanzo kilisema kuwa kabla ya kuvuka, mbele yake kulikuwa na gari aina ya Toyota Prado ambalo ghafla lilirudi nyuma na kugonga gari lake.
NI VIGUMU KUAMINI
Kikiwa eneo la tukio, chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa ni vigumu kwa mtu yeyote kuamini kama Johari alitoka salama kufuatia gari hilo kuwa nyang’anyang’a.
Hata hivyo, chanzo hicho kilisema Johari hakuumia sehemu yoyote ila alipata maruweruwe, akionekana kama aliyechanganyikiwa kwani muda wote alikuwa akiongea vitu visivyoeleweka.
HUYU HAPA JOHARI
Baada ya kupata habari hiyo, mwandishi wetu alifika eneo hilo na kukuta gari hilo limeondolewa ambapo alipuzungumza na Johari, alikiri kukutwa na mkasa huo huku akimshukuru Mungu kwa kutoka salama.
“Sipati picha nikilitazama gari langu na nikijiona mimi mwenyewe nimenusurika, kweli ni Mungu tu,” alisema Johari.
KWA NINI BARABARA HIYO?
Staa huyo nguli katika muvi za Kibongo, mwishoni mwa mwaka juzi alipata ajali mbaya katika barabara hiyohiyo ya Mandela, eneo la External na kusababisha gari lake kuharibika vibaya huku akiokolewa na wasamaria wema.
ATAKIWA KUWA MAKINI
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo, Johari anapaswa kuwa makini na vyombo vya moto kwani inawezekana vikakatisha uhai wake.
Johari alipoulizwa na mwandishi wetu kuwa anahisi ajali zote zinatokana na nini na kwa nini hutokea kwenye barabara hiyo, alisema hajui kuna nini lakini akakubaliana na ushauri wa kuwa makini anapoendesha gari barabarani.
0 Comments