MFANYAKAZI wa ndani, Therezia Thomas (12) na mkazi wa Kijenge katika Jiji la Arusha, amekatwakwatwa na kisu katika viganja vyake na mwajiri wake, Hawa Shaban (32) baada ya kuchelewa kupika makande aliyoagizwa.

Mashuhuda wa ajali hiyo, wamedai kuwa Therezia alifanyiwa unyama huo Jumamosi iliyopita jioni nyumbani kwa mtuhumiwa huyo mara baada ya mwajiri huyo kurejea nyumbani kwake na kukuta makande hayo hayajaiva.

Akizungumza huku akitokwa machozi, binti huyo mwenye umri mdogo alidai kuwa tajiri yake huyo alimchukua kutoka kwao Singida ili amsaidie kazi za ndani kwa malipo ya Sh 10,000 kwa mwezi.

Alidai kuwa siku ya tukio alipewa maelekezo ya kupika makande na kuondoka, lakini tajiri aliporudi jioni alikuta makande hayo bado hayajaiva akamgombeza na kumpiga na baadaye alipoona haitoshi alichukua kisu na kuanza kumcharanga sehemu mbalimbali za mikono yote miwili.  
Alidai kuwa wakati akipigwa alikuwa amemziba mdomo na kufungiwa chumbani kwa komeo na alipotosheka, alimwacha katika chumba hicho bila msaada wowote kwa muda wa siku mbili mfululizo.

Baada ya majirani kutomuona, na kuhoji alipo inadaiwa mmoja wa majirani alidai kusikia akilia wakaamua kuingia ndani ya nyumba hiyo na kumkuta akiwa amejilaza sakafuni huku damu zikimchuruzika na kuamua kumchukua na kutoa taarifa katika kituo cha polisi.

Polisi baada ya kufika eneo la tukio, walimtia mbaroni mtuhumiwa na kumfungulia jalada lenye kumbukumbu namba AR/RB/680/2012, huku mtoto huyo akipelekwa na kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,Thobias Andengenye alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.