KUTOKA BBC
Msikiti na shule moja ya Kiislam zimeshambuliwa na kuchomwa moto katika mji wa kusini wa Benin, polisi wamesema.
Polisi wameiambia BBC kuwa mtu mmoja ameuawa, 10 wamekamatwa na kuwa sehemu ya msikiti ilikuwa bado inaungua.
Hii inatokea baada ya shambulio jingine kutokea katika msikiti mwingine jijini humo siku ya Jumatatu.

Boko Haram

Katika wiki za hivi karibuni, watu wa upande wa kusini, ambao wengi wao ni Wakristo au wasio na dini, wamekuwa wakishambuliwa na kundi la Waislam wenye itikadi kali la Boko Haram. Kundi hilo linafanya shughuli zake zaidi upande wa kaskazini.
Kiongozi wa kabila la Hausa mjini Benin ameiambia BBC Idhaa ya Kihausa kuwa watu wa kaskazini wapatao 7,000 wanatafuta hifadhi katika vituo vya polisi na kambi za wanajeshi mjini humo.
Chama cha Msalaba Mwekundu cha Nigeria kimethibitisha kwa BBC kuwa kinawaandikisha watu wa kaskazini katika vituo vya polisi na kambi za kijeshi.
Magari mawili yaliyokuwa katika eneo ambalo kuna msikiti na shule yalichomwa moto, wamesema polisi.

Vijana

Shambulio hilo ni la hivi karibuni katika mfululizo wa mashambulio ya kidini ambayo yamesababisha watu wengi wa kusini wanaoishi kaskazini kukimbia makazi yao.
Mwandishi wa BBC mjini Abuja Naziru Mikailu, amesema ghasia hizi mpya zilianza siku ya Jumatatu wakati kundi la watu liliposhambulia msikiti mmoja, na kujeruhi watu 10.
Halikadhalika, Gisau, mji mkuu wa jimbo la kaskazini la Zamfara, vijana walishambulia kanisa. Polisi walikamata watu 19, anasema mwandishi wetu.
Kundi la vijana lilijaribu kumshambulia kiongozi wa jamii ya Wahausa, lakini kiongozi huyo alisaidiwa na vijana wa Kihausa na baadaye polisi kuingilia kati, anasema mwandishi wetu.
Mwandishi wa vitabu na mshindi wa tuzo ya Nobel Wole Soyinka amelaumu ghasia hizo za miezi ya hivi karibuni, viongozi ambao huweka dini zao mbele kuliko umoja wa kitaifa.
"Unapokuwa kwenye hali ambapo kundi la watu wanaweza kwenda mahala pa kuabudu na kushambulia kwa bunduki kupitia madirisha, basi umefikia wakati mbaya wa kumwaga damu katika maisha ya taifa hilo," amesema katika mahojiano na BBC