Na Brighton Masalu
BAADA ya kunusurika kifo mara mbili, msanii mwenye jina kubwa katika tasnia ya filamu za Kibongo, Blandina Chagula ‘Johari’, amesema kwa sasa hataki tena kuendesha magari, chanzo cha habari kinanukuu.
Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa gazeti hili katikati ya wiki hii, Johari aliweka wazi kuwa kutokana na kunusurika huko kifo, sasa hataki tena kuendesha magari na badala yake atakuwa anamtumia dereva wake mwenye utaalamu.
Msanii huyo aliyasema hayo baada ya hivi karibuni kupata ajali ya gari iliyotokea Ubungo, Dar katika Barabara ya Mandela huku kumbukumbu zikionesha kuwa aliwahi kupata ajali ya aina hiyo katika barabara hiyohiyo siku za nyuma.
Alipoulizwa kama anafikiri ajali hiyo ina mkono wa mtu, Johari aliyefanya makamuzi kwenye filamu nyingi ikiwemo ya The Shell alikiri kuwa na maadui wengi ambao kwa namna moja ama nyingine wanaweza kuwa chanzo.
“Hebu fikiria, kwa sasa ni mara mbili napata ajali ya gari tena barabara ileile, hivyo, kwa sasa sitaki kuendesha nitamtumia dereva wangu na kama hayupo nitatumia njia nyingine lakini si kuendesha mimi,” alisema.
Akaongeza:“Sitaki kuamini hivyo japo kweli maadui ni wengi, lakini kwa sasa hakuna usafiri ninaouchukia kama wa gari.”
0 Comments