MJUMBE wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Tanzania Islamic Centre (TIC), Muhidin Ndolanga amenusurika kupigwa na waumini wa msikiti wa Kichangani, Magomeni Dar es Salaam, kwa kilichodaiwa ni kutaka kuingilia masuala ya msikiti huo.

Tukio hilo lililotokea jana baada ya swala ya mchana iliyofanyika msikitini hapo, lilisababisha
Ndolanga achaniwe koti na baadhi ya waumini walio upande wake, kupigwa na mmoja kujeruhiwa.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya waumini walisema chanzo cha mtafaruku huo ni ujumbe uliotolewa na TIC wa kuwasimamisha baadhi ya viongozi wa msikiti huo, suala ambalohawakukubaliana nalo.

Walisema kitendo cha taasisi hiyo kuwasimamisha maimamu wasaidizi wa msikiti huo kimeonesha kuingiliwa kwa madaraka ya msikiti bila waumini kushirikishwa.

Waumini hao ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini, walidai taasisi hiyo mara kwa mara imekuwa ikiingilia masuala ya msikiti huo na kuvuruga utaratibu wa uendeshaji wake.“Hivi karibuni walimsimamisha Imam Mkuu wa Msikiti kwa kisa kisichojulikana, leo wametangaza kumrudisha na kuwafukuza wasaidizi wake, masuala ambayo sisi waumini hatuwezi kuyavumilia,” alisema mmoja wao.

Walimtaja Imam aliyesimamishwa jana kuwa ni Warid Alhad, huku wasaidizi wake wakitajwa kwa jina moja moja la Jaffar na Mulisalina.




Alidai vurugu hizo zilitokea ndani ya msikiti huo zikiambatana na matusi mazito kwa kiongozi
huyo, pamoja na taasisi yake, baada ya baadhi ya waumini kumnusuru kwa kumtoa nje chini ya ulinzi mkali wa polisi na kuelekea kituo cha Polisi Magomeni.

Mwandishi wa gazeti hili alifika kituoni hapo na kumshuhudia Ndolanga na wenzake, wakitoa
maelezo juu ya kilichotokea.

Alipoulizwa na gazeti hili, kiongozi huyo hakuwa tayari kuzungumza chochote kwa madai kuwa suala hilo ameliacha mikononi mwa sheria.

”Siwezi kusema lolote kwa kuwa tayari nimeshafika hapa wao ndio watalishughulikia,” alisema
Ndolanga ambaye alipata kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) na Mkurugenzi wa Wanyamapori katika Serikali ya Awamu wa Pili.
Mmoja wa viongozi wa taasisi hiyo waliopatwa na makasa huo pamoja na Ndolanga ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutaja jina lake kwa madai kwamba si mzungumzaji wa suala hilo, alidai kwamba vurugu hizo zilisababishwa na kundi la waumini wachache waliowaita wahuni, wanaotaka kuifanya taasisi hiyo sehemu ya kujichumia fedha.

Alisema msikiti huo pamoja na vitega uchumi vingine yakiwamo maduka, shule na zahanati ni mali ya taasisi hiyo na vinaendeshwa kwa utaratibu maalumu uliopangwa.

Hadi mwandishi wa habari hii anaondoka eneo hilo la kituo hicho saa moja kamili, Ndolanga na viongozi wenzake, bado walikuwa wakiendelea kutoa maelezo kituoni hapo ambapo Mkuu wa Kituo hicho, Omary Chambo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
                                               
                                  CHANZO CHA HABARI NI HAPA