Kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya kimataifa ua Jinai,ICC, iliyoko mjini The Hague Louis Moreno Ocampo anasema atawasilisha ushahidi zaidi kutaka mashtaka yathibitishwe dhidi ya wakenya wawili mashuhuri, ambao majaji katika mahakama hiyo walikataa kuthibitisha mashtaka dhidi yao kuhusiana na ghasia za baada ya uchagzui wa mwaka 2007 nchini Kenya.
Siku ya jumatatu mahakama ya ICC ilithibitisha mashtaka dhidi ya washukiwa wanne akiwemo naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta, lakini majaji wakasema hawakuridhishwa na ushahidi ulitoloewa na kiongozi wa mashtaka dhidi ya aliyekuwa mkuu wa Polisi Major Generali Hussein Ali na waziri wa zamani Bwana Henry Kosgey, na kwa hivyo wakakataa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.Wengine ambao mashtaka yao yalithibitishwa ni mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura, aliyekuwa waziri wa elimu ya juu William Ruto na mtangazaji wa redio Joshua Arap Sang.
Akihutubia waandishi wa habari katika mahakama ya ICC, Bwana Ocampo amesema hatakata rufaa dhidi ya uamuzi wa majaji, lakini ataendelea kukusanya ushahidi zaidi kutoka waathirika na kuuwasilisha tena mbele ya jopo la majaji watatu walioshughulikia kesi hiyo ya washukiwa wa ghasia za Kenya.
Amesema atafanya uchunguzi zaidi juu ya Bwana Ali na Bwana Kosgey wakati kesi dhidi ya watuhumiwa wanne ambao mashtaka dhidi yao yalithibitishwa itakapoanza.
Wakati wa kutoa uamuzi siku ya Jumatatu, jaji kiongozi Ekaterina Trendafilova alisema hawakushawishika na ushahidi uliotolewa wa kumhusisha Bwana Kosgey na ghasia dhidi ya wafuasi wa chama cha PNU katika maeneo kadhaa mkoani Rift Valley.
Alielezea kwamba kiongozi wa mashtaka alitegemea shahidi mmoja tu dhidi ya Bwana Kosgey, na ambaye hakuthibitishwa.
Pia aliongeza kwamba upande wa mashtaka ulibana tarehe ambazo inadaiwa Bwana Kosgey alihudhuria mikutano ya kupanga ghasia, na hivyo kumkosesha fursa ya kuandaa utetezi.
Jaji huyo pia alisema ushahidi uliowasilishwa haukuwa na misingi ya kutosha kuonyesha kwamba Polisi walishiriki kwenye ghasia katika maeneo ya Nakuru na Naivasha.
Kuhusu uamuzi huo, Bwana Ocampo amesema atafanya uchunguzi zaidi katika sehemu za Kisumu na Kibera mjini Nairobi, ambako anadai Polisi walishiriki kwenye ghasia.
Amesema atatafuta ushahidi zaidi kuthibitisha kwamba Bwana Kosgey alihusika kwenye ghasia pamoja na Bwana Ruto na Bwana Sang. BBC
0 Comments