POLISI mkoani Rukwa inamsaka askari wake kwa tuhuma ya kumpa ujauzito mwanafunzi wa
kidato cha pili mwenye umri wa miaka 15 wa sekondari ya Msakila mjini hapa.

Inadaiwa mtuhumiwa alichukua uamuzi wa kutoroka na kujificha kusikojulikana baada ya askari rafiki yake kumtapeli Sh 800,000 alizompa ampelekee mama mzazi wa mwanafunzi huyo na kiasi kingine apewe msichana huyo ili atoe ujauzito huo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage jana alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa
ni G3402 Joshua Gabriel wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mjini hapa.

“Nasema hatua za kijeshi tutakazozichukua ni pamoja na hii ya kumsaka, siwezi kusema zaidi
ya hapo. Narudia ni kweli ametoroka, lakini kumtafuta ni moja ya mikakati yetu, sina maelezo
zaidi ya hayo,” alisema Kamanda.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi ulibaini kuwa mtuhumiwa ameoa na
ana mtoto mmoja wa kike ambaye anadaiwa kuwa na umri wa miaka miwili na walikuwa
wanaishi katika nyumba ya kupanga eneo la Jangwani mjini hapa.Kwa mujibu wa baadhi ya wapangaji wa nyumba hiyo, mtuhumiwa alitoweka nyumbani hapo
Desemba 20 mwaka jana.



Walidai kuwa mkewe ambaye ni mama wa nyumbani anayedaiwa kutelekezwa na mumewe aliondoka akidai anarudi kwa wazazi wake Nachingwea, Lindi.

Inadaiwa ameondoka mjini hapa tangu Desemba 25 mwaka jana akiwa na mwanawe huyo wa
kike.

Kwa mujibu wa mlezi wa mwanafunzi huyo ambaye alijitambulisha kama mjomba wake,
ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, baada ya kuona mabadiliko ya mwili na tabia ya mpwawe huyo Desemba mosi mwaka jana alimsafirisha Musoma mkoani Mara, mama yake amchunguze kwa undani.

“Wakati huo mpwa wangu alikuwa likizo za Krismasi na Mwaka Mpya, hivyo baaada ya
kubaini mabadiliko kimwili na kitabia alianza kurudi nyumbani usiku kwa pikipiki, hivyo niliamua nimsafirishe kwetu Musoma ili mama yake amchunguze.

‘’Dada yangu huyo Desemba 10 mwaka jana alinitaarifu kuwa binti yake amebainika kuwa
mjamzito wa miezi mitano na siku kadhaa, nikamtaka aje naye hapa kwangu … waliwasili
hapa Desemba 15,“ alisema mjomba.

Alidai kuwa aliporejea alipimwa tena na matokeo yakabaki yale yale na alipoulizwa akakiri
kupewa ujauzito na askari Polisi.
Alidai kuwa aliporejea alipimwa tena na matokeo yakabaki yale yale na alipoulizwa akakiri
kupewa ujauzito na askari Polisi.

Mjomba aliripoti tukio hilo Polisi mjini hapa lakini mtuhumiwa alipoitwa, mwanafunzi alimkana kuwa siye tukabaini kuwa mpenzi wake alikuwa amemdanganya.

“Lakini baada ya kumfuatilia kwa muda tulibaini binti yetu alituelekeza chumba ambacho
walikuwa wakikutania, kumbe kilikuwa ni cha askari mwenzake aitwaye Joshua na alikuwa akimwazima chumba kwa ajili ya kukutana na mwanafunzi huyo.

“Hata hivyo askari huyo alituelekeza anakoishi mtuhumiwa na tulipofika mpwa wangu alimtambua mara moja,“ alisema na kuongeza kuwa alifungua jalada namba Sum/RB/8260/2011 na kumtaarifu Mkuu wa Shule.

Lakini wakati hayo yakiendelea kwa mujibu wa mlezi huyo, mtuhumiwa alimtuma rafiki yake (askari mwenziwe) aliyekutana na mama wa mwanafunzi huyo na kumwomba wayamalize nje ya Mahakama.

“Mie sikuwapo nyumbani, ndipo dada akanijulisha kuhusu ugeni huo uliofika kutoa pole ya Sh 800,000 ili mambo yaishie nje ya Mahakama pia alidai sehemu ya pesa hizo apewe binti ili akatoe mimba … nilikataa na kumwagiza dada asizipokee,“ alisema.

Lakini habari kupitia kwa rafiki wa karibu wa mtuhumiwa zinadai baada mjomba mtu kukataa pesa hizo rafiki huyo aliamua kuzitumia fedha hizo kwa manufaa yake, ndipo mtuhumiwa alipoamua kutoroka.

Mkuu wa Sekondari ya Msakila, Damas Songoro, alikiri kutaarifiwa juu ya ujauzito wa
mwanafunzi huyo.
                                                      Picha haihusianni na maandishi hayo hapo juu.